Wednesday , 8 February 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Lissu arejea, kufungua ukurasa mpya wa kisiasa nchini
Habari za SiasaTangulizi

Lissu arejea, kufungua ukurasa mpya wa kisiasa nchini

Spread the love

BAADA ya takribani miaka mitano nje ya nchi, hatimaye mwanasiasa wa upinzani, mbunge wa zamani wa Singida Mashariki na mwanasheria nguli, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na aliyepata kuwa rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Antiphas Lissu, amerejea nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Lissu alirejea nyumbani leo, 25 Januari 2023, kutokea uhamishoni nchini Ubelgiji, alikoenda kunusuru maisha yake.

Kwa mujibu wa maelezo yake, kurejea kwake nchini wakati huu, kunalenga kile alichokiita, “kuandika ukurasa mpya” katika safari yake ya kisiasa.

Mjumbe wa kamati kuu Chadema, John Heche akimlaki Tundu Lissu (kulia) katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere leo tarehe 25 Januari, 2023 jijini Dar es salaam. Kushoto ni Mwenyekiti wa Chadema kanda ya Nyasa, Peter Msigwa

Alisema, “hatuwezi kuendelea kuishi uhamishoni bila ukomo. Hivyo basi, ninarejea nyumbani kuendeleza mapambano ya kisiasa na kidemoksasia.”

Aliongeza, “napenda kuwafahamisha kwamba, panapo majaliwa, nitakanyaga udongo wa ardhi ya Tanzania kwa mara nyingine tena siku ya Jumatano ya tarehe 25 Januari 2023, majira ya saa saba na dakika 35 mchana.”

Lissu aliwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), kwa ndege ya kampuni ya Ethiopia Airways, majira ya saa saba mchana na kulakiwa na maelfu ya wananchi, wakiwamo wanachama wa chama chake.

Mwanasiasa huyo wa upinzani, aliingia nchini akitokea Ubelgiji alikokuwa amekimbilia baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, ili kunusuru maisha yake.

Lissu alikuwa akiishi nchini Ubelgiji alikokuwa amepelekwa kwa mara ya kwanza kwa ajili ya matibabu, kufuatia kushambuliwa kwa risasi na wanaoitwa na serikali, “watu wasiofahamika,” tarehe 7 Septemba 2017, wakati akirejea nyumbani kutokea bungeni.

Alifikishwa Ubelgiji kwa safari iliyoratibiwa na “marafiki zake, Januari 2018 na kupatiwa matibabu katika hospitali ya chuo kikuu cha Luvein na madaktari bingwa wa mifupa kwa takribani miezi minane.

Kabla ya kupelekwa Ubelgiji, alipatiwa matibabu katika hospitali kuu ya Nairobi, ambako madaktari zaidi ya 10 walikuwa wanazunguka kitanda chake kila siku kuokoa maisha yake.

Lissu ambaye wakati huo alikuwa Mnadhimu wa Kambi rasmi ya upinzani bungeni na mwanasheria mkuu wa Chadema,  alinusurika kifo, wiki mbili baada ya kunukuliwa akisema, “maisha yangu yako hatarini.”

Alilazimika kurejea tena nchini Ubelgiji baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, na kwamba tangu wakati huo, amekuwa nchini humo.

Mapema kiongozi huyo wa upinzani mwenye miaka 55, ameeleza kuwa amerejea nyumbani, kujadili mambo muhimu yanayowahusu wananchi, huku akiuta mwaka 2023, ni mwaka muhimu katika historia ya taifa lake.

Lissu alitangaza uamuzi wake wa kurejea nyumbani baada ya Rais wa Jamhuri, Samia Suluhu Hassan kuondoa marufuku ya mikutano ya kisiasa mwezi huu iliyokuwa imewekwa na mtangulizi wake, John Magufuli.

Pamoja na kwamba tangu kushambuliwa, amewahi kurejea nchini, lakini yaweza kuwa kurejea kwake safari hii, kwaweza kuwa kwa kudumu.

Katika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam, Lissu ambaye alikuwa mgombea Urais kwa tiketi ya Chadema mwaka 2020, alipokewa kwa shangwe na vikundi vya ngoma na bodaboda ambazo zimepambwa kwa bendera ambazo zinaongoza msafara wake kutoka uwanjani hadi Temeke ambako atakuwa na amkutano wa hadhara.

Jeshi la Polisi limeimarisha ulinzi na kuhakikisha wafuasi na wapenzi hao wa Chadema hawaingii ndani ya uwanja wa ndege ili kuruhusu huduma zingine kuendelea.

Aidha, wamesindikiza msafara wa Lissu ambao una msururu mrefu wa magari, bodaboda na wengine wanaotembea kwa miguu.

Je, baada ya miaka mitano ya kuishi uhamishoni, kurejea kwake, kuna maana gani kwa siasa za Tanzania?

Jibu ni hili: Kwamba, licha ya kuwa nje kwa miaka mitano na ushei, ushawishi wake katika siasa za upinzani bado ungalipo. Kwa lugha nyingine, makovu yake ya kisiasa hayajaondosha mvuto wake wa kisiasa mbele ya wafuasi wa chama chake na wananchi wengine, bali vimezidi kumuongezea umaarufu.

Lissu amesifika kwa ukosoaji dhidi ya serikali ya Magufuli. Hata kabla ya hapo tayari alikuwa ni mwanasiasa maarufu. Harakati zake za wakati wa Magufuli zilizidi kumuweka mstari wa mbele katika siasa za upinzani.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Jaji Biswalo aendelea kung’ang’aniwa fedha za ‘Plea Bargaining’, CUF wataka ajiuzulu

Spread the love  CHAMA cha Wananchi (CUF), kimemtaka aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtaka...

Habari za Siasa

Bunge labaini madudu mfumo ukusanyaji mapato, h’shauri tatu kikaangoni

Spread the love  KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali...

Habari za Siasa

Mkuu wa wilaya ya Rungwe azindua vyumba sita vya madarasa vya thamani ya 64 mil

Spread the love  MKUU wa Wilaya ya Rungwe, Jaffar Haniu amezindua vyumba...

Habari za Siasa

Mbunge afurahia mabilioni ya Samia kutua jimboni

Spread the love  MBUNGE wa Igunga, Nicholas Ngassa ameishukuru Serikali kwa utekelezaji...

error: Content is protected !!