August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lissu aponea chupuchupu

Spread the love

HOFU ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kumfutia dhamana Tundu Lissu ambaye ni mtuhumiwa wa kesi ya uchochezi, imetoweka baada ya mahakama hiyo kukubaliana na utetezi wadhamini wake kuwa, Lissu yupo Ujerumani kwa matibabu, anaandika Faki Sosi.

Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Mbunge wa jimbo la Singida Mashariki, alishindwa kuhudhuria mahakamani siku ya jana na hivyo wadhamini wake kutakiwa kujieleza, kwanini mtuhumiwa huyo asifutiwe dhamana.  

Kesi ya uchochezi inayomkabili Lissu ni kesi Na. 208 katika gazeti la MAWIO akiwa ni mtuhumiwa namba nne sambamba na Jabir Idrissa, Simon Mkina, na Ismail Merhaboob.

Jabir ni mwandishi mwandamizi wa MAWIO, Mkina ni mhariri wa gazeti hilo na Merhaboob ni meneja wa kampuni ya uchapishaji magazeti inayojulikana kwa jina la Flint.

Jana baada ya Lissu kutofika mahakamani, upande wa Jamhuri uliibua hoja ya kufutwa kwa dhamana yake, ambapo Kishenyi Mutalemwa, wakili wa Serikali alidai kuwa, kutokuwepo kwa mtuhumiwa huyo mahakamani hapo kutaathiri uendashaji wa kesi hiyo.

Hata hivyo, Peter Kibatala, wakili wa utetezi alisema mteja wake alikuwepo mahakama hapo siku ya kutolewa mamuuzi hayo tarehe 7 Septemba, mwaka huu kabla ya kuahirishwa kwa kesi na kuomba mahakama ivute subira ili wadhamini wa Lissu wafike mahakamani kutoa maelezo ya kwanini Lissu hakufika mahakamani hapo.

Ibrahim Ahmed na Robert Katula, wadhamini wa Lissu, mbele ya Hakimu Thomas Simba, siku ya leo wameieleza mahakama hiyo kuwa mtuhumiwa huyo yupo nchini Ujerumani kwa matibabu na kwamba atarejea nchini hivi karibuni.

Hata hivyo Mutalemwa, wakili wa serikali, ameiomba mahakama kumuongezea masharti ya dhamana Lissu, ikiwemo kuzuia hati yake ya kusafiria huku wakili wake Peter Kibatala akiiomba mahakama hiyo kuwaamini wadhamini wa mtuhumiwa huyo.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza pande zote, amewataka wadhamini wa mtuhumiwa huyo na mawakili wake kuhakikisha kuwa Tundu Lissu anakuwepo mahakamani hapo kila kesi hiyo inapotajwa.

Kesi hiyo itatajwa tena tarehe 4 Oktoba mwaka huu.

 

error: Content is protected !!