December 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lissu apigilia msumali wabunge viti maalum Chadema

Spread the love

TUNDU Lissu, aliyekuwa mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ameendelea kupinga chama hicho kupeleka wabunge wa viti maalum bungeni. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaan … (endelea). 

Lissu ni miongoni mwa viongozi wa Chadema, wanaopinga suala hilo kwa madai, kufanya hivyo ni sawa na kuwasaliti wananchi waliowapigia kura katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020.

Katika uchaguzi huo, chama tawala- Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilitangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuibuka na ushindi mkubwa wa madiwani, wabunge na urais ambao haujawahi kutokea tangu mwaka 1995 ulipoanza uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi.

Hata hivyo, Chadema na ACT-Wazalendo ni miongoni mwa vyama vya siasa, vilivyopinga matokeo hayo kwa madai, uchaguzi huo uligubikwa na udanganyifu mkubwa wa sheria, kanuni na taratibu.

Kutokana na hali hiyo, Chadema ambacho kwa mujibu wa sheria, kimejipatia viti 19 vya wabunge wa viti maalum, kumekuwa na mjadala mzito ndani na nje ya chama hicho kuhusu je, wapeleke majina NEC ili yateuliwe au wasifanye hivyo kwani wamekwisha kusema haukuwa uchaguzi halali?

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema

Lissu ambaye ni makamu mwenyekiti wa Chadema (Bara), amekuwa akipinga waziwazi chama hicho kupeleka wabunge wa viti maalum bungeni au madiwani akisema “haukuwa uchaguzi, ulikuwa uchaguzi.”

Mwansiasa huyo aliyeondoka juzi Jumanne tarehe 10 Novemba 2020 kwenda nchini Ubelgiji kwa kile alichodai “kuendelea kubaki Tanzania, maisha yangu yangekuwa hatarini” ametoa waraka wa kusisitiza chama hicho kutokubali kuteua majina ya viti maalum.

Lissu ametoa waraka huo kipindi ambacho, taarifa za ndani ya chama hicho zinaeleza, Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), limekuwa likishinikiza kupelekwa kwa majina hayo NEC.

Halima Mdee

Waraka huo wa Lissu, kama ulivyo huu hapa chini;

Hiki chama hakijarudishwa mwaka ‘95. Chama hiki leo ni kikubwa kuliko chama kingine chochote cha siasa Tanzania (CCM sio chama cha siasa, ni chama-dola).

Chama hiki leo kina wanachama zaidi ya milioni sita walioandikishwa; na uongozi uliochaguliwa katika kila ngazi ya uongozi nchi nzima.

Chama hiki kimedhihirisha kwamba kinaungwa mkono na mamilioni ya Watanzania wa makundi yote na rika zote. Ushahidi ni kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Chama hiki kimedhihirisha pia kwamba bila matumizi ya nguvu za kijeshi za dola chama hiki hakiwezi kushindwa uchaguzi wowote katika nchi hii.

Hakukuwa na chama cha aina hii mwaka ‘95 au katika kipindi kingine chochote cha historia yetu. Sasa kipo, labda mtu asiwe na macho ya kuona au akili ya kutambua.

Kufikiria kwamba chama ni wabunge au madiwani tu ni kukosa kuelewa maana ya chama cha siasa katika mazingira halisi ya nchi yetu.

Tundu Lissu, aliyekuwa Mgombea Urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chadema akiwasili nchini Ubelgiji

Ni kuangalia mambo kwa macho ya maslahi yetu binafsi na kushindwa kuangalia kwa miwani ya maslahi mapana ya wananchi wetu. Na hilo ndio tatizo la baadhi yetu!!!

Kibaya tunachotakiwa kukiepuka ni kuruhusu watu wenye vijimaslahi vyao kukiharibu chama kwa kutuaminisha kwamba bila wao kuwa wabunge au madiwani basi hakuna chama.

Tunachopigania sio nani wawe wabunge au madiwani tu. Kama hiyo ndio ingekuwa lengo letu tungeshapeleka majina ya wabunge na madiwani wa Viti Maalum wote.

Tunachopigania ni wananchi wetu wawe na Uhuru, Haki na Maendeleo ya Watu. Lengo hilo linahitaji tuwe na wabunge na madiwani waliopatikana kwa njia halali, sio wa kupewa zawadi na walioharibu Uchaguzi Mkuu.

Kuwa na wabunge na madiwani katika mazingira ambayo yatahalalisha utawala huu haramu ndio kutakakoumiza na kuharibu chama chetu kuliko kitu kingine chochote.

Ndio maana maCCM na wapambe wao wanataka sana tupeleke wabunge wa Viti Maalum bungeni. Wanajua hilo ndio litakuwa tambara la kudekia na kuhalalisha uharamu wa uchafuzi wao. Na ndio njia itakayoumiza chama chetu kuliko magereza yote ya Magufuli.

error: Content is protected !!