TUNDU Lissu, mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amewaacha njia panda wanachama wa chama hicho Jimbo la Kigoma Mjini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kigoma … (endelea).
Tofauti na maeneo mengine aliyopita kwenye kampeni zake za urais, akiwa kwenye eneo la Mwanga, Kigoma Mjini amewaambia wanachama wake, kwamba wampigie kura mgombea yeyote wanayemuona ana nguvu ya kuking’oa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani.
“Kama mgombea wa Chadema katika jimbo hili ana nguvu, mchagueni huyo na kama mgombea wa Chama cha ACT-Wazalendo ana nguvu, muungeni mkono, yeyote mwenye nguvu ndio mgombea wangu,” ameeleza Lissu.
Kwenye jimbo hilo, Chadema imemsimamisha Francis Mangu ambaye anapambana na Zitto Kabwe, kiongozi wa ACT-Wazalendo anayepigania kuongoza jimbo kwa mara ya pili.

Lissu amesema, lengo la upinzani ni kuing’oa CCM hivyo, uamuzi wa nani anapaswa kupewa kura kwenye jimbo hilo ameuacha kwenye ‘mikono’ ya wakazi wa jimbo hilo.
Hata hivyo, Omary Gindi ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Kigoma Mjini, amewataka wananchi wachague wagombea wa chama hicho ili watekeleze ilani ya chama hicho.
Miongoni mwa mambo aliyoahidi kuyafanya endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, ni kufanya mabadiliko ya Katiba ili yaendane na mazingira ya sasa.
Amesema, atakuwa kiongozi tofauti na wale waliopita kwa kuwa, wameongoza nchi kwa kutumia Katiba ya mwaka 1977 ambayo haikidhi matakwa ya mazingira ya sasa. Ameahidi kupunguza mamlaka ya rais ambayo yanaweza kutumika vibaya.

“Viongozi wote hawa wameongoza nchi kwa kutumia Katiba ya mwaka 1977 iliyotungwa baada ya Tanganyika kupata Uhuru, ndio chanzo cha mateso wanayopata wananchi, lazima tuandike Katiba mpya ili tuondokane na marais wasio waadilifu,” amesema.
Akiwa katika Kata ya Chiungutwa wilayani Masasi, Mtwara tarehe 19 Septemba 2020, Zitto amemnadi Frank John, mgombea udiwani wa kata hiyo kupitia Chadema.
“Tunachotaka ni kuhakikisha tunapata diwani wa upiznani hapa, inatakiwa mumpe kura. Tunachokitaka ni kufanya kazi kwa maslahi ya watu sio maslahi ya vyama hivi, tunamuunga mkono huyu wa Chdema,” amesema.
Leave a comment