August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lissu amtaka Wambura, serikali yagoma

Spread the love

CAMILIUS Wambura, Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZCO), ametakiwa kufika mahakamani kama shahidi katika kesi ya uchochezi inayomkabili Tundu Lissu, Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, anaandika Faki Sosi.

Maombi ya kumtaka Wambura kufika mahakamni hapo, yametolewa na Peter Kibatala, wakili wa upande wa utetezi katika kesi hiyo ambayo Lissu anatuhumiwa kutoa maneno ya uchochezi kwa kumuita Rais John Magufuli kuwa ni ‘dikteta Uchwara’.

Lissu anadaiwa kutamka maneno hayo mara baada ya kutoka mahakamani katika kesi nyingine inayomkabili ya kutoa maneno ya uchochezi kupitia gazeti la MAWIO.

Kibatala amedai kuwa, kabla ya mashahidi wengine kutoa ushahidi, ni vyema mahakama imuite Mkuu wa Upelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ili afike mahakamani hapo, kutoka maelezo kama sehemu muhimu ya kesi kutokana na yeye kuwa ndiye mtoa taarifa.

“Tunaiomba Mahakama iwaamuru upande wa mlalamikaji kumleta ZCO kutokana na ukweli kuwa, maelezo yake ni sehemu ya ushahidi hasa katika mashitaka haya yanayohusu sheria ya magazeti. Maelezo yake ni muhimu ili mshitakuwa aweze kujitetea,” amedai Kibatala.

Bernad Kongola, Wakili wa serikali akijibu hoja za Kibatala amedai kuwa, mkuu wa upelelezi sio shahidi katika kesi hiyo hivyo hakuna sababu ya kuitwa mahakamani hapo.

Kongola amesema, upande wa serikali tayari unao mashahidi na kuwataja kwa majina kuwa ni ASP Kimweri, na Sub-Sajenti. Ndege. Yohona Yongola, Hakimu Mkazi Mahakama ya Kisutu, amesema kuwa uamuzi wa hoja zilizotolewa na pande mbili juu ya kuletwa kwa mkuu wa upelelezi kanda maalumu ya Dar, ataufanya tarehe 6 Septemba mwaka huu.

error: Content is protected !!