September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lissu amtahadharisha Membe, agusia ushirikiano na ACT-Wazalendo

Spread the love

MWANASIASA machachari wa upinzani nchini Tanzania,Tundu Antipas Lissu, amemuonya kada wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bernard Membe, kuwa upinzani wa sasa nchini, “siyo lelemama.” Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

“Akizungumza kwenye mkutano mkuu wa chama cha ACT- Wazalendo, unaofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jublee, jijini Dar es Salaam, leo Jumatano, Lissu alisema, “Membe karibu kwenye mapambano. Huku ni kigumu sana na kama umeingia naamini uko tayari.”

Aliongeza, “karibu tushirikiane kuondoa maovu. Huku ni kugumu sana, lakini kwa kuwa umekuja, naamini uko sawa sawa.”

Membe, ambaye alikuwa waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa katika serikali ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete, kwa takribani miaka 10, alijiunga na ACT-Wazalendo, tarehe 7 Julai 2020 akitokea chama tawala (CCM).

Kujiunga kwa Membe kwenye upinzani, kulikuja muda mfupi baada ya kutangazwa kuwa amefukuzwa uwanachama wa CCM, kwa kile kilichoitwa, “utovu wa maadili ya chama.”

Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), alipitishwa na mkutano mkuu wa Chadema jana Jumanne, tarehe 4 Agosti 2020, kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Katika uchaguzi huo, Salum Mwalimu, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, amefanywa kuwa mgombea mwenza wa Lissu.

Membe ambaye alifukuzwa CCM, tarehe 28 Februari mwaka huu, anatarajiwa kupitishwa na mkutano kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano, huku Maalim Seif Shariff Hamad, akitarajiwa kutangazwa kuwa mgombea urais wa Zanzibar.

Kuhusu uchaguzi huo, Lissu amesema, utakuwa mgumu mno, lakini akawahakikishia kuwa upinzani utashinda.

Akiongea kwa sauti ya uchungu, Lissu alisema, “…tukikosea kwenye uchaguzi huu, basi tumekwisha. Tukikosea Tanzania hii ya vyama vingi kama tulivyoifahamu tangu 1992 iko rehani. Kwa hiyo, uchaguzi huu hauko sawa na uchaguzi mwingine wowote unaofikiria tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi na kwamba ni sisi ndio tutakaopoteza.”

Alisema, “tuko pamoja na tunataka kushirikiana. Lakini katika kushirikiana, kuna mitego mingi kweli kweli, itabidi kama watu wazima wenye busara zao, tutaangalia wapi kwenye ndoana na wapi kuko salama. Lakini nisehe tutashirikiana na tupo pamoja.”

Akimzungumzia Maalim Seif, Lissu amesema, “mimi nikiwa katika chumba kimoja, niwe kwenye kikao na Maalim Seif, huwa nakuwa mdogo sana na mara nyingi, vijana wanashida zao, ujana una matatizo yake na sisi vijana mara nyingi kwa sababu za ujana wetu hatujui kwamba kuna watu wameacha kuwa watu binafsi au kwa mchango wao kwenye historia ya nchi na jamii wamekuwa ni taasisi.”

“Maalim Seif ni taasisi, umchukie, umpende katika siasa za Zanzibar, kama ni bei ya kupigania haki za Zanzibar amekwisha kulipa zaidi,” amesema Lissu huku akishangiliwa na wajumbe wa mkutano huo

Aliongeza, “Maalim Seif ni taasisi na watu wa aina hii, wanazaliwa wachache katika vipindi vya historia. Tunapaswa kumheshimu sana huyo.”

Lissu amesema, “sisi wa Chadema, hatutafanya jambo lolote la kuhujumu mapinduzi na harakati za miaka mingi za Wazanzibari chini ya uongozi wa Maalim Seif. Sisi wa Chadema na mimi mgombea urais wa Chadema na mgombea wangu mwenza, Salum Mwalimu, hatuwezi kutumika kunyonga maslahi ya Wazanzibari.”

Amesema, tutashirikiana na ACT-Wazalendo, kuikata na kuhakikisha kwamba Zanzibar inaongozwa na viongozi wa Zanzibar.

Lissu urejeo wake nchini baada ya miaka mitatu ya kuwa nje kwa matibabu yaliyotokana na majeraha ya risasi zaidi ya 30 alizoshambuliwa na watu wasiojulikana, umebadili kwa kiasi kikubwa upepo wa kisiasa katika nafasi ya urais.

Licha ya jeshi la polisi kupiga marufuku wafuasi wake kumpokea kwa maandamano, umati mkubwa ulijitokeza tarehe 28 Julai mwaka huu, katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere.

Kura nyingi alizopigiwa na wajumbe wa Baraza Kuu Chadema ni ushahidi mwingine kuwa Lissu anaungwa mkono na wananchi wengi.

Kabla ya urejeo Lissu, mjadala mkubwa kutoka kwenye duru za siasa, uliangazia jina la Rais John Magufuli, mgombea urais wa CCM dhidi ya Kachero na Mwanadiplomasia mashuhuri ulimwenguni, Bernard Kamilliu Membe.

error: Content is protected !!