September 25, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Lissu ‘ampeleka’ rumande Katibu Mkuu Bavicha

Spread the love

KATIBU Mkuu wa Baraza la Vijana wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha) Julius Mwita amekamatwa na Jeshi la Polisi mchana huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, anaandika Faki Sosi.

Mwita na vijana wengine watatu ambao hawakufahamika majina yao mara moja wamekamatwa kwa sababu ambazo hazijafahamika mpaka sasa wakati wakisubiri Tundu Lissu Mwanasheria Mkuu wa Chadema kufikishwa mahakamani hapo.

Mwandishi wa mtandao huu ameshuhudia Mwita na vijana wawili wakikamatwa ndani ya eneo la mahakama na kuingizwa ndani ya gari ya polisi yenye namba za usajili PT 1848, ambayo hata hivyo ilishindwa kuondoka mahakamani hapo baada kugoma kuwaka.

Kijana mwingine mmoja amekamatwa akiwa nje ya uzio wa mahakama hiyo ambapo askari waliojihami kwa silaha za moto wameimarisha ulinzi ndani na nje ya mahakama ya Kisutu tangu saa mbili leo asubuhi.

Vijana wote wanne tayari wameondolewa mahakamni hapo na gari ya polisi ambapo inaaminika kuwa watapelekwa Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es salaam kwaajili ya mahojiano.

Tayari Freeman Mbowe Mwenyekiti wa Chadema taifa na Mbunge wa jimbo la Hai pamoja na James Mbatia Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi taifa wameondoka katika eneo la mahakama hiyo ambapo walifika tangu saa tano asubuhi wakisubiri Tundu Lissu kufikishwa kizimbani.

Wabunge wengine akiwemo Halima Mdee wa Jimbo la Kawe, Saed Kubenea (Ubungo), Riziki Ngwali (viti maalum-CUF), Joseph Haule (Mikumi) na wengineo wameendelea kubaki mahakamani hapo, huku sababu za Lissu kuchelewa kufikishwa mahakamani zikiwa hazijulikani.

Dk. Vincent Mashinji Katibu Mkuu wa Chadema naye amewasili katika viunga vya mahakama hiyo.

error: Content is protected !!