TUNDU Lissu, mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amemchongea Rais John Magufuli kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera, kwamba alibadilisha matumizi ya fedha za tetemeko la ardhi mkoani humo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kagera … (endelea).
Lissu amewataka wananchi wa Kagera kutomchagua Rais Magufuli, ambaye anatetea wadhifa wake huo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika Uchaguzi Mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020 kwa maelezo, hana nia ya kuwasaidia.
Mgombea huyo wa urais ametoa kauli tarehe 21 Septemba 2020, katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye Jimbo la Kyerwa mkoani humo.
“Maisha yenu yameharibika, rais anasimama hadharani anasema sitawasaidia, amekusanya rambirambi nchi nzima tumepata tetemeko, alivyozipata ameenda kujenga reli, rais anayekula rambirambi mmeona wapi? Sasa hatutaki rais wa namna hiyo,” amesema Lissu.

Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa kipimo cha richa 5.9 lilitokea tarehe 10 Septemba 2016, liliathiri zaidi mkoani Kagera na kuwa watu zaidi ya 15 huku 170 wakijeruhiwa na kubomoa majengo zaidi ya 800 ikiwemo makanisa na shule.
Baadhi ya taasisi za serikali, binafsi pamoja na watu mashughuli na wananchi wa kawaida walitoa fedha za mchango kwa ajili ya kupoza machungu wahanga wa tetemeko hilo.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni za urais mkoani Kagera tarehe 16 Septemba 2020, Rais Magufuli aliwataka wananchi wa mkoa huo kupuuza madai ya kwamba serikali yake imekula hela hizo, kwa kuwa zilitumika kwenye shughuli za kijamii, ikiwemo ujenzi wa shule.
Noah mboma
Noahmboma44@gmail.com