Tuesday , 21 March 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Lissu alivyopata hati ya kusafiria
Habari za Siasa

Lissu alivyopata hati ya kusafiria

Spread the love

TUNDU Lissu, aliyekuwa mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) amesema, “sikimbii vita, nakwenda kufungua uwanja mwingine wa mapambano nje ya nchi.’Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam…(endelea).

Lissu ameatoa kauli hiyo jana Jumanne tarehe 10 Novemba 2020, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, muda mfupi kabla ya kuondoka kwenda nchini Ubelgiji.

“Naondoka kwa sababu inanibidi kwanza niwe salama, ili tuweze kupambana lazima niwe salama na kuendelee kukaa hapa kwa wakati huu, siwezi kuwa salama,”amesema Lissu ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara) na kuongeza:

“Huko ninakokwenda, lazima shughuli iendelee na itaendelea zaidi, nakwenda kufungua milango mingine ya mapambano.”

Katika uwanja huo wa ndege, Lissu alisindikizwa na maofisa wa Ubalozi wa Ujerumani, Marekani, ndugu, jamaa na marafiki.

Lissu aliishia nyumbani kwa Balozi wa Ujerumani tangu tarehe 4 Novemba 2020, alipokwenda kuomba hifadhi akidai kutishiwa maisha na watu wasiojulikana.

Rais huyo wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alidai kutishiwa maisha mara baada ya kutangazwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020, hivyo kulazimika kutafuta hifadhi.

“Nilianza kupokea vitisho vya maisha yangu, mara baada ya uchaguzi mkuu kumalizika,”alisema Lissu na kuongeza:

“Baada ya vitisho kuzidi kuongezeka, nilitafakari kwa kina taarifa za vitisho hivyo, pamoja na taarifa kutoka kwa wasamalia wema, ndipo nilipoamua kwenda kutafuta hifadhi ya muda sehemu nyingine tofauti na nyumbani kwangu.”

Soma zaidi: Lissu aondoka Tanzania, aacha ujumbe

Akijibu swali aliloulizwa kwamba anakwenda uhamishoni, amejibu “siendi Ubelgiji kuomba hifadhi ya kisiasa, la hasha! Nakwenda kama return resident (mkazi ninayerudi).

“Ninakwenda kujipanga na ninaahidi kuwa nitarudi nyumbani na nitaendeleza haya mapambano,” amesema Lissu.

Amesema, akiwa nchini Ubelgiji pamoja na kutembelea mashirika mbalimbali yaliyopo Jumuiya ya Ulaya, ikiwamo Bunge la Ulaya, pamoja na Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Ulaya, atatembelea pia nchi 33 zilizojifunga kwenye mkataba wa Shengena ambako yeye anaruhusiwa kuingia bila kuwa na Visa.

Kuhusu baadhi ya wanasiasa wenzake ndani na nje ya Chadema, wanaodai ameamua kukimbia nchi kwa kuwa ameogopa mapambano, Lissu amesema, “waambie hivi, sikimbii mapambano. Sijawahi kukimbia. Nakwenda Ulaya ili kujipanga upya.”

Alipoulizwa haoni kwa nafasi yake ya makamu mwenyekiti wa Chadema Bara, hatua yake ya kuondoka nchini, ni kukitelekeza chama chake na hivyo kusababisha kudhoofika, Lissu amesema..

“…Chama siyo gunia linalohitaji kubebwa au gari linalohitaji kuendeshwa. Chama ni wafuasi, wanachama, wapenzi, viongozi na vikao.

“Chama kitaendeshwa na kitafanya maamuzi yake. Hakuhitaji kuwapo nchini au kuwapo kila mahali, ili kuendesha chama. Nimekuwa nje ya nchi kwa takribani miaka mitatu na muda wote huo, nimeshiriki vikao vyote vya maamuzi vya chama na nimesaidia ujenzi wa chama kwa njia mbalimbali.”

Amesema, pamoja na kuondoka kwake, bado ataendelea kushiriki vikao vyote vinavyomhusu kama ambavyo amekuwa akifanya hivyo huko nyuma, ikiwamo kikao cha hivi karibuni cha Kamati Kuu (CC), ambacho alishiriki akiwa tayari yuko ‘hamishoni’ kwenye makazi ya balozi wa Ujerumani.

Amesema, hata vyama vikubwa vya ukombozi, vilivyoendeshwa na kupata mafanikio makubwa ya kisiasa, kuna wakati baadhi ya viongozi wake, walilazimika kuondoka nchini mwao ili kujipanga upya na harakati za kutetea demokrasia katika nchi zao.

Ametolea mfano, Chama cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS), kinachoongozwa na rais wa sasa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Felix Tshisekedi ambaye ni mtoto wa aliyekuwa kiongozi wa upinzani nchini humo, Etienne Tshisekedi.

Kwamba Tshisekedi alikimbilia Kongo na kwenda kuishi Ubelgiji, ili kuendesha harakati zake za kisiasa, lakini baadaye amekuwa rais wa nchi hiyo kubwa na tajiri Afrika Mashariki na Kati.

Alipoulizwa anatoa wito gani kwa wananchi waliompigia kura na Watanzania wengine, Lissu amesema, “kwa wananchi wa Tanzania, ujumbe wangu ni kwamba sikimbii mapambano, ila nakwenda uwanja mwingine mpya wa kudai haki, demokrasia na utu wetu kwa nchi yetu.”

Lissu amesema, kabla ya tishio hilo la maisha yake, alipanga kuondoka nchini kuelekea Ubelgiji, tarehe 18 Desemba 2020 kwa kuwa tayari alikuwa na miadi ya kuonana na daktari wake, katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Luvein, alikokuwa akitibiwa majeraha ya risasi kwa takribani mwaka mmoja, tarehe 20 Desemba.

Majadiliano yalivyokuwa

Kabla ya kuruhusiwa kuondoka Tanzania, Serikali za Ujerumani, Marekani, Uholanzi na Ubelgiji, kupitia kwa balozi wake walioko nchini, walifanya majadiliano marefu na serikali ya Tanzania, kupitia kwa aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi, ili kuwezesha mwanasiasa huyo kurejea nchini Ubelgiji, kwa kuzingatia mikataba ya kimataifa ya Vienna.

Taarifa zinaeleza, kufuatia ruhusa hiyo, ndipo Lissu aliweza kupata hati mpya ya kusafiria, baada ya hati yake ya awali kuisha muda wake, baada ya mabalozi hao kuitaka Serikali kumruhusu kiongozi huyo kuondoka nchini, kutokana na kuwapo kwa tishio kubwa la usalama wake.

Mabalozi hao walitaka hakikisho hilo la serikali la kumruhusu kuondoka nchi kwa salama, kufuatia kuibuka kwa taarifa za tishio la usalama wake.

Ili kuhakikisha Lissu anaondoka salama pasina vikwazo, maofisa ubalozi wa Ujerumani na Marekani, walimsindikiza kutoka Ubalozi wa Ujerumani hadi Uwanja wa Ndege.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Rais Samia aagiza iundwe kamati ya pamoja ya Mawaziri mradi wa BBT

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amewaagiza mawaziri kuunda kamati...

Habari za Siasa

Rais Samia apangua makatibu tawala mikoa, ateua Kamishna DCEA

Spread the loveALIYEKUWA Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Gerald...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

M/kiti bodi ya wadhamini Chadema afariki dunia

Spread the loveMWENYEKITI wa Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Demokrasia na...

Habari za Siasa

Zitto: Nikifa Ado atavaa viatu vyangu

Spread the love  KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe...

error: Content is protected !!