Tuesday , 18 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Lissu aifikisha kesi ya Mbowe kwa Rais Samia
Habari za SiasaTangulizi

Lissu aifikisha kesi ya Mbowe kwa Rais Samia

Spread the love

 

MAKAMU Mwenyekiti wa Chadema nchini Tanzania, Tundu Lissu amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameahidi kushughulikia kesi ya ugaidi inayomkabili mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na wenzake watatu, kwenye Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, jijini Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Lissu ametoa kauli hiyo jana Alhamisi tarehe 16 Februari 2022, muda mfupi baada ya kuzungumza na Rais Samia, jijini Brussels nchini Ubelgiji na kuelezea kile walichoteta faragha kwa zaidi ya saa moja.

“Nimemueleza kesi inamuumiza mwenyekiti wetu na familia yake, inawaumiza walinzi wake na familia zao na inazidi kutugawa sisi Watanzania, nimemwambia Rais afanye analoliweza kwa mamlaka yake ahakikishe kwamba hii kesi inaondolewa mahakamani,” amesema Lissu.

Lissu amesema “hakuna sababu yoyote ya kuendelea na kesi ambayo kila mtu anaona na ushahidi unaonesha mahakamani kwamba, ni mambo ya kuunga unga tu na Rais ameahidi atalishughulikia.”

Mwanasiasa huyo amesema, katika mazungumzo yake na Rais Samia, alimueleza kwamba kesi hiyo hailisaidii Taifa, chama chake Cha Mapinduzi (CCM), Serikali yake au Chadema.

“Katika masuala ambayo nimemueleza Rais, la kwanza nimezungumza naye kwa kirefu kuhusiana na kesi ya uongo inayomkabili Mwenyekiti wetu, Freeman Mbowe na walinzi wake watatu. Nimemwambia Rais hiyo kesi haisaidii nchi yetu, Serikali yake na chama chake, haikisaidii chama chetu,” amesema Lissu.

Mbowe na wenzake wanakabiliwa na kesi hiyo ya uhujumu uchumi Na. 16/2021, yenye mashtaka sita ya ugaidi, inayosikilizwa mahakamani hapo mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni waliokuwa makomando wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Kesi hiyo ilifunguliwa tarehe 18 Julai 2020, kisha wenzake Mbowe walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, tarehe 19 Agosti mwaka huo.

Mbowe aliunganishwa katika kesi hiyo tarehe 26 Julai 2021, bada ya upelelezi dhidi ya tuhuma zinazomkabili kukamilika. Ilihamishiwa katika Mahakama ya Uhujumu Uchumi, tarehe 9 Septemba mwaka jana.

Katika kesi hiyo,Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka sita ya ugaidi, likiwemo la kushiriki vikao vya kupanga ugaidi, kupanga njama za kudhuru viongozi wa Serikali akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimankaro, Lengai Ole Sabaya. Kupanga maandamano yasiyo na kikomo nchi nzima.

Shtaka lingine linalowakabili pamoja ni la kutaka kuchoma vituo vya mafuta na mikusanyiko yenye maeneo ya watu.

Pia, Mbowe anakabiliwa na shtaka la kutoa fedha Sh. 699,000 kwa ajili ya kufadhili vitendo hivyo, wakati Kasekwa akikabiliwa na shtaka la kukutwa na silaha aina ya bastola, kinyume cha sheria na dawa za kulevya.

Huku Hassan akikabiliwa na shtaka la kukutwa na sare pamoja na vifaa vya JWTZ na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Julai na Agosti 2020, kwenye mikoa ya Morogoro, Kilimanjaro na Dar es Salaam.

Tayari upande wa mashtaka umefunga ushahidi wake, kwa kuleta mahakamani hapo mashahidi 13 kati ya 24 iliyopanga kuwaita, ukidai tathimini yao imeonesha washtakiwa hao wana kesi ya kujibu.

Jaji Tiganga amepanga kesho Ijumaa, tarehe 18 Februari 2022, kutoa uamuzi mdogo kama Mbowe na wenzake wana hatia au hawana hatia.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Mazingira magumu ya JPM yamechangia ‘Comedy Journalism’

Spread the loveMwenyekiti wa Kamati ya kufuatilia hali ya uchumi wa vyombo...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

RC Chalamila: Nimeacha ubabe

Spread the loveMKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chamalila amemthibishia...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Rais Samia atoa ujumbe mzito Sikukuu Eid Al Adha

Spread the loveKATIKA kusherehekea Sikukuu ya Eid Al Adha, Rais wa Tanzania,...

BiasharaHabari za Siasa

Dk. Biteko aipongeza NMB kwa kuanzisha utoaji wa bima ya mifugo

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

error: Content is protected !!