October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lissu aichomea tena Serikali ya JPM

Tundu Lissu, aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki

Spread the love

TUNDU Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ameandika wakala wake kwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, Lazaro Nyalandu juu ya kifo cha Katibu wa Chama Wilaya ya Manyoni, Marehemu Alex Jonas Magubi.

Mheshimiwa Lazaro Nyalandu, MB

Mwenyekiti wa Kanda ya Kati

CHADEMA

Mh. Mwenyekiti Salaam.

Nimepokea taarifa za kuuawa kwa Katibu wetu wa Chama Wilaya ya Manyoni, marehemu Alex Jonas Magubi, kwa masikitiko makubwa.

Taarifa za awali za mauaji hayo nilizozipata zinazua maswali mengi yanayohitaji kujibiwa na vyombo vya usalama vya Serikali hii ya Rais Magufuli.

Inaelekea, kwa mujibu wa taarifa hizo, marehemu alikodiwa na watu wasiojulikana ambao walienda kumkata kata mapanga na kumuua kinyama.

Taarifa hizo zinasema sio piki piki yake au kitu chake kingine kilichochukuliwa na wauaji hao. Hapa ndipo maswali yanayohitaji kujibiwa yanapoanzia.

Kwa mara nyingine tena, Chama chetu na Kanda yetu imepatwa na msiba mkubwa wa kutengenezwa. Kwa mara nyingine tena, familia, ndugu, jamaa na marafiki wamepotelewa na mpendwa wao katika mazingira ya jinai kubwa na ya kutatanisha.

Kwa mara nyingine tena, nchi yetu imekumbwa na mauaji yanayoelekea kuwa ya kisiasa. Na kwa mara nyingine tena, vyombo vya usalama vya Serikali ya Magufuli vinatunyanyulia bango la ‘watu wasiojulikana’ kuhusiana na wauaji wa viongozi wetu wa Chama.

Alfons Mawazo, Mwenyekiti wetu wa Mkoa wa Geita, aliuawa kwa kukatwa katwa mapanga mchana kweupe na kisha kutupwa barabarani. Mpaka leo, karibu miaka mitano baadae, tunaambiwa na vyombo vya usalama aliuawa na ‘watu wasiojulikana.’

Diwani wetu Luena wa Ifakara aliuawa nyumbani kwake kwa kukatwa katwa mapanga usiku na tunaoambiwa ni ‘watu wasiojulikana.’

Katibu wetu wa Kata ya Hananasif, Dar Es Salaam, Daniel John, naye alitekwa nyara na kisha kuuawa na kutupwa kwenye ufukwe wa Bahari ya Hindi na ‘watu wasiojulikana.’

Mauaji haya ni nje ya jaribio la mauaji dhidi yangu la Septemba 7, 2017, ambalo nalo lilikuwa kazi ya ‘watu wasiojulikana.’

Na ni nje ya mashambulio ya kujeruhi,  vipigo vya polisi na waitwao usalama wa taifa, kutekwa nyara na kuteswa, kukamatwa na kufunguliwa kesi za uongo, kufukuzwa kazi, kuharibiwa biashara, vitisho na kila aina ya uovu ambao viongozi na wanachama wetu wamefanyiwa katika kipindi hiki cha Tanzania ya Magufuli.

Lengo la mateso yote haya ni kuvunja nguvu, ari na mwamko wa wa viongozi na wanachama wetu, na kuzima matumaini, matarajio na matazamio ya Watanzania kwa Chama chetu.

Kwenye hili, Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wasiojulikana na wale wanaowatuma, kuwaelekeza, kuwawezesha, kuwalipa na kuwalinda hawajafanikiwa na hawatafanikiwa, kwa sababu historia ya dunia nzima haiko upande wao.

Karibu miaka sabini iliyopita, yaani tarehe 21 Septemba 1953, aliyekuwa Rais mpya wa Chama cha ANC Jimbo la Transvaal, Nelson Rolihlahla Mandela, alihutubia Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama chake kwa njia ya barua. (Alikuwa amepigwa marufuku kukutana mahali popote na zaidi ya watu watano!)

Mandela aliwaambia Wajumbe wa Mkutano Mkuu huo maneno yafuatayo: “Mnaweza kuona sasa kwamba hakuna njia rahisi ya kufikia kwenye ukombozi, na wengi wetu tutapitia katika bonde la uvuli wa mauti tena na tena, kabla ya kufikia kwenye vilele vya milima ya matamanio yetu. Hatari na magumu hayakutuzuia siku za nyuma, hayatatutisha sasa. Lakini lazima tujiandae kukabiliana nayo kama wanaume waliojizatiti, ambao hawapotezi muda wao kwa maneno matupu bila vitendo.”

Mandela aliandika maneno hayo akiwa kijana wa miaka 35, na miaka 11 kabla hajahukumiwa kifungo cha maisha mwaka 1964 kwenye Kesi ya Rivonia.

Mwaka 1994, miaka 41 baada ya kuandika maneno hayo na akiwa mzee wa miaka 76, Mandela aliapishwa kuwa Rais wa kwanza wa Afrika Kusini huru.

Yeye na wenzake wengi walipitishwa kwenye bonde la uvuli wa mauti tena na tena. Lakini hawakukata tamaa mpaka walipofikia kilele cha mlima wa matamanio yao.

Na sisi pia tuko kwenye njia hiyo hiyo ya mapito magumu. Na sisi pia tumepitishwa, tunapitishwa na tutapitishwa tena na tena katika bonde la uvuli wa mauti.

Lakini mauaji na majaribio mauaji ya viongozi wetu; kutekwa nyara na kuteswa kwa wanachama wetu;  kesi za uongo dhidi ya viongozi wetu, na dhulma zote tunazofanyiwa, yote haya hayajatuzima siku za nyuma, na hayatatutisha sasa.

Wakati tunafarijiana na kupeana pole ya msiba huu mkubwa katika Chama chetu, Kanda yetu na Mkoa wetu, tujiandae kikamilifu kukabiliana na haya ya sasa na yale yajayo.

Haki huinua taifa. Mungu wetu ni Mungu wa haki. Atasimama na atawasimamia wale wenye haki.

Naomba, kupitia kwako, niwape pole familia, ndugu, jamaa, marafiki wa marehemu, pamoja na viongozi na wanachama wetu wa Wilaya ya Manyoni, Mkoa wa Singida, Kanda ya Kati na nchi nzima kwa ujumla kwa msiba huu mkubwa.

Mwenyezi Mungu ampe marehemu mapumziko ya amani. Amen.

Tundu AM Lissu, MB

MAKAMU MWENYEKITI

error: Content is protected !!