July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lissu ageuzwa mjadala wa CCM bungeni

Mbunge wa jimbo la Mtera, Livingstone Lusinde (CCM) akizungumza kwa hisia bungeni

Spread the love

KAULI ya Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, kwamba Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imechoka inastahili kupumzishwa, imewachoma wabunge wa chama hicho na sasa wameamua kutumia muda mwingi kujibu mapigo badala ya kujadili hoja. Anaandika Edson Kamukara … (endelea).

Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alitoa kauli hiyo jana wakati akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2015/16.

Alisema, “wachovu hawa wa serikali ya CCM, wameshindwa kuipa fedha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili ifanye kazi zake kwa uwazi wakitaka kutengeneza mazingira ya kuongeza muda wa rais.

…hawa wachovu walioshindwa kufanya kura ya maoni ya katiba inayopendekezwa waliyodanganya watu kuwa tungeifanya Aprili 30 mwaka huu, lakini wakashindwa.”

Katika siku ya pili ya mkutano wa 20 wa Bunge leo, wabunge takribani wote wa CCM waliopata nafasi ya kuchangia hotuba hiyo, walitumia muda mwingi kujibu kauli ya Lissu wakidai ni upotoshaji huku nao wakirusha kejeli kwa wapinzani hususani vyama vinavyounda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwamba haviwezi kuingia Ikulu.

Baadhi ya wabunge hao ni Dk. Cyril Chami (Moshi Vijijini), Said Nkumba (Sikonge), Stella Manyanya (Viti Maalum) na Livingstone Lusinde (Mtera) ambaye alitoka kabisa nje ya mjadala na kuamua kuporomosha matusi ya nguoni kwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, kuwa ndiye aliyechoka licha ya Lissu kusema CCM imechoka.

Ukiacha wabunge wachache wa pande zote wanaojielekeza kujadili hoja, wengi wanafanya propaganda za kisiasa ili kujitafutia umaarufu wa kuchaguliwa tena katika uchaguzi ujao na hivyo, kuondoa uhalali wa kazi ya wabunge kuisimamia serikali kutekeleza majukumu yake.

Conchester Rwamlaza na Pauline Gekul (Chadema), wao walijiekeleza kwenye matumizi mabaya ya fedha katika halmashauri na hivyo, kuishauri serikali kuweka usimamizi mzuri ikiwa ni pamoja na kupeleka fedha zilizoidhinishwa kwa wakati.

Rwamlaza alizungumzia mfano wa halmashauri moja katika mkoa wa Njombe, akisema kwa kwa bajeti za miaka mitatu ya 2012/13, 2013/14 na 2014/15 inaendeshwa kwa bakaa na hivyo kudai kwamba wanaposema serikali imechoka sio kwamba wanatukana bali ijitazame upya.

Pia aligusia suala la miundombinu dhaifu ya barabara zinazojengwa chini, suala ambalo pia lilisemewa na Gekul na Eugine Mwaiposa, mbunge wa CCM (Ukonga).

Kuhusu vijana, Gekul na Saburina Sungura (Chadema), walitaka suala la ajira lipewe mkazo badala ya kuwatumia kama ngazi ya wanasiasa kupata uongozi, huku wakisisitiza kwamba waziri mkuu lazima atoe kauli kuhusu haki ya wanafunzi wa vyuo vikuu kushiriki uchaguzi mkuu ujao.

Walisema kuwa wanavyuo hao wamekuwa wakibabaishwa kwa kupangiwa maeneo tofauti ya kujiandikisha na kupiga kura. Kwamba kwa sasa wakati uandikishaji ukiendelea wako vyuoni lakini wakati wa uchaguzi serikali inafunga vyuo na hivyo wanashindwa kupiga kura.

Suala la migogoro isiyokwisha ya ardhi nalo limezungumzwa kwa kirefu na baadhi ya wabunge wakiwemo, Agripina Buyogela wa Kasulu Vijijini (NCCR-Mageuzi), Abdulkarim Shaha wa Mafia (CCM) na Mkiwa Kimwaga wa Viti Maalum CUF.

Walishauri kuwa maeneo ambayo wawekezaji wameshindwa kuyaendeleza, serikali iyachukue na kuyagawa kwa wananchi wasio na ardhi ili kupunguza migogoro pamoja na kuweka vizuri mipaka katika maeneo ambapo Jeshi la Wananchi Tanzania (JWT) linapakana na wananchi.

error: Content is protected !!