MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Upinzani, Tanzania- Chadema-Bara, Tundu Lissu, amekosoa uamuzi wa Rais wa nchi hiyo, Samia Suluhu Hassan, kumteua Biswalo Mganga, kuwa Jaji wa Mahakama Kuu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Jana Jumanne, tarehe 11 Mei 2021, Rais Samia aliteua majaji 21 wa Mahakama Kuu ya Tanzania, akiwemo Biswalo, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP).
Mganga, amehudumu nafasi ya DPP kwa takribani miezi sita na miezi saba, tangu tarehe 6 Oktoba 2014, alipoteuliwa na Rais wa wakati huo, Jakaya Mrisho Kikwete.
Mara baada ya uteuzi huo wa Mganga kuwa Jaji Mkuu, Lissu ambaye kitaaluma ni wakili, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter, amesema, Mganga hakustahili kupata uteuzi huo, kwa maelezo uongozi wake katika Ofisi ya DPP ulikuwa na dosari.

Amesema, katika kipindi cha uongozi wa Mganga, baadhi ya watu walifunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha kimakosa, hasa watu walioonekana kuipinga Serikali ya awamu ya tano.
Pia, mwanasiasa huyo amesema, sheria za nchi zinaelekeza DPP anaweza kuondolewa madarakani kama amepoteza uwezo wa kufanya kazi au kuwa ofisini kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuumwa.
Au kuwa na mwenendo usioendana na maadili ya maafisa wa sheria na mawakili wa serikali katika utumishi wa umma, kwa mujibu wa Sheria ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya mwaka 2005 pamoja na sheria nyingine zinazosimamia maadili ya watumishi wa umma.
Lissu ambaye kitaaluma ni mwanasheria, amesema Rais anaweza kumuondoa DPP baada ya kushauriana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), baada ya hapo aanzishe kamati ya watu watatu, mwenyekiti na wajumbe wawili kwa kushauriana na AG, ambao watachunguza mapendekezo ya Rais kama ni sahihi DPP aondolewe au abaki madarakani.
Mh. Rais umekosea & umevunja sheria: DPP Biswalo Mganga alitesa watu wasio & hatia kwa mashtaka ya uongo ya uhujumu uchumi & utakatishaji fedha. Wengi wanaozea magerezani kwa sababu yake. Alistahili kufukuzwa kazi chini ya Sheria hii; sio kupewa hadhi ya Jaji wa Mahakama Kuu yetu pic.twitter.com/MjpCNTJl5N
— Tundu Antiphas Lissu (@TunduALissu) May 11, 2021
Lissu amesema baada ya kamati hiyo kutoa mapendekezo yake, Rais atachukua hatua kulingana na mapendekezo hayo.
“Rais umekosea na umevunja sheria, DPP Biswalo Mganga alitesa watu wasio na hatia kwa mashtaka ya uongo ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha. Wengi wanaozea magerezani kwa sababu yake. Alistahili kufukuzwa kazi chini ya sheria hii; sio kupewa hadhi ya Jaji wa Mahakama Kuu yetu,” ameandika Lissu.
Asante ndugu lissu lakini uwelewe kuwa wakati umekupita ukiwa unatembea yaliyobaki kwako ni maneno matupu unachokifanya hakionekan