Friday , 1 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Lissu aanika matobo miswada sheria za uchaguzi
Habari za SiasaTangulizi

Lissu aanika matobo miswada sheria za uchaguzi

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema
Spread the love

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amekosoa miswada ya mabadiliko ya sheria za uchaguzi, akidai mapendekezo yake hayalengi kutatua changamoto za kisheria zilizopo kwenye mfumo wa uchaguzi nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Mwanasiasa huyo aliyekuwa mgombea urais wa Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa 2020, ametoa kauli hiyo leo tarehe 2 Desemba 2023, akizungumzia Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa 2023, kwa njia ya mtandao.

Lissu ametoa maoni yake akisema kuwa, mapendekezo ya muswada huo hayalengi kutatua changamoto za kisheria zilizopo katika mfumo wa uchaguzi.

Mwanasiasa huyo amedai muswada huo mapendekezo yake hayajibu changamoto ya wasimamizi wa uchaguzi kufanya upendeleo kwa kuwa ni watumishi wa umma.

“Wasimamizi wa uchaguzi wa kimataifa ambao wameangalia chaguzi  miaka yote hii wamesema kwamba tatizo la usimamizi wa uchaguzi Tanzania ni kwamba hawako huru ni watumishi wa serikali wanakuwa chini ya mamlaka ya Rais wa CCM,” amesema Lissu.

Lissu amesema “muswada huu unasema katika kipengele cha sita kinawataja wasimamizi hao wa uchaguzi endapo sheria hii itapitishwa, watakuwa wakurugenzi walewale wa miaka yote. Maana yake ni kwamba hawa ambao wanatuengua miaka yote ndio watakaosimamia chaguzi zijazo, hakuna mabadiliko yoyote.”

Makamu huyo mwenyekiti wa Chadema, amedai  muswada huo haujalenga kutatua changamoto ya wapiga kura wenye sifa kuachwa kuandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura, kwa kuwa hakuna pendekezo linalolenga zoezi hilo kufanyika kila mwaka.

“Mfumo wetu wa wapiga kura unaacha wapiga kura wengi wenye sifa nje, sababu unandikishaji wapiga kura unafanyika mara mbili katika miaka mitano ya mzunguko wa uchaguzi. Mfumo sahihi wa uandikishaji wapiga kura inatakiwa hilo daftari liwe wazi muda wote watu waweze kuandikishwa,”

“Inahitajika wafanyakazi wa kudumu wa tume kuandikisha wapiga kura, ndio maana ya pendekezo la kuwa na tume huru ya uchaguzi ni pamoja na kuwa na watumishi wa tume wa kudumu waweze andikisha muda wote. Hakuna pendekezo lolote jipya kwa hiyo system ya uandikishaji itakuwa ileile,” amesema Lissu.

Dosari nyingine aliyotaja Lissu katika muswada huo, ni muswada huo kutotatua changamoto ya zuio la wagombea binafsi.

“Tatizo lililopo sasa katika mfumo wetu wa uchaguzi ambalo ni kubwa sana ni ubaguzi wa wazanzibar na watanganyika. Mfumo wetu wa sasa unasema Tume ya Taifa ya Uchaguzi ina mamlaka kuandikisha wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, upande wa Zanzibar mtu ili aandikishwe inatakiwa akidhi amsharti ya ukaazi,” amesema Lissu.

Lissu amesema “mtu anaweza atoke Zanzibar leo akaja Tanganyika kesho kubwa anaandikishwa daftari la kudumu la wapiga kura, lakini sheria ya Zanzibar inasema ili uje uandikishwe kuwa mpiga kura lazima uthibitishe umekuwa mkazi wa eneo husika si chini ya miaka mitatu, kama hujafikisha uandikishwi.”

Aidha, Lissu amesema kuwa, mapendekezo ya muswada huo, yanalenga kufanya mabadiliko katika Sheria ya Sheria ya Uchaguzi wa Taifa unaohusu nafasi ya Urais na Wabunge iliyotungwa 1985 na Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa iliyotungwa 1979, kwa kuziunganisha na kuwa sheria moja.

“Kwa maoni yangu kitu ambacho ni kikubwa zaidi ambacho hakina maana yoyote katika muswada huo ni kuunganisha sheria hizi na kuwa sheria moja. Nani ameshindwa kufanya chochote kwenye uchaguzi kwa sababu ya kuwepo sheria mbili tofauti?”

“Kuunganisha sheria hizi kuwa moja haziboreshi sheria yenyewe, kama sheria zilikuwa mbovu haziwi bora kwa kuunganisha ni kwamba unaunganisha ubovu uliopo katika sheria mbili unaunganisha katika sheria moja,” amesema Lissu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Mwili wa Hayati Mwinyi kuagwa leo saa 8 Uwanja wa Uhuru

Spread the loveMWILI wa Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi unatarajiwa kuagwa kuanza...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Mwinyi kuzikwa Machi 2 visiwani Unguja

Spread the loveMWILI wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili wa Tanzania,...

Habari za SiasaTangulizi

Rais mstaafu Mwinyi afariki dunia

Spread the loveRais Mstaafu wa awamu ya pili wa Tanzania, Ally Hassan...

Habari za Siasa

Waziri mkuu Ethiopia atua Tanzania

Spread the loveWaziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia,...

error: Content is protected !!