January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lishe duni huchangia kuzorota kwa elimu

Watoto wa shule wakinywa maji

Spread the love

LISHE duni ni moja kati ya sababu zinazochangia kuzorota kwa elimu nchini kutokana na matatizo ya udumavu wa ubongo na akili yanayowakabili asilimia 42 ya watoto nchini wenye udumavu wa ubongo na akili.

Tatizo hili huathiri uwezo wao wa kufundishika wanapokua darasani pamoja na kiwango cha ufaulu mashuleni.

Kutokana na utamaduni wa kutozingatia lishe bora na vyakula vyenye virutubisho muhimu kwa ukuaji wa mwili na akili, matatizo ya udumavu, utapiamlo na ukondefu yamekua yakiwapata watoto wengi.

Dokta Joyceline Kaganda ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Chakula na Lishe nchini  amesema kuwa, watoto wenye udumavu wa akili na ubongo wanapata shida katika kujifunza wanapokua mashuleni na hata kushindwa kufanya vizuri katika masomo yao.

Tatizo kubwa ni uelewa wa watu juu ya mahusiano kati ya lishe na maendeleo ya mtoto kitaaluma, kipimo kikubwa tunachokitumia kupima haliya udumavu ni watoto wenye umri kati  ya miaka 0 mpaka 5, (0-5). Katika umri huu mtoto asipopata lishe na virutubisho muhimu anaweza kupata udumavu.

Matatizo haya pia yanaanzia kwa kina mama pindi wanapokua wajawazito wanahitaji kupata lishe bora ili mtoto alioko tumboni aweze kukua

vizuri kimwili,kiakili na kuwa na afya bora kwa ujumla.

Wako watoto wanaokua na udumavu huu wa akili na kuwa watu wazima kiwango chao cha utendaji kazi na ufanisi pamoja na uwezo wa akili

unakua  mdogo kiini cha tatizo kinaanzia tangu mama anapokua mjamzito anamzaa mtoto na kumlea katika utoto wake.

Tunawasihi kina mama kupenda kujielimisha juu ya masuala ya lishe kupata lishe muhimu zitakazowasaidia kuwa na afya bora wao na watoto wao.

Mfano vyakula vya mboga mboga na matunda, vyakula vya vitamini kama samaki, maharagwe pamoja na vyakula vya wanga wali, ugali unaotokana na nafaka halisi za mahindi, mtama usikobolewa .

Suala la lishe likitiliwa mkazo litasaidia sana kukua kwa elimu nchini pamoja na kuchochea maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Profesa Joyce Kinabo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine Morogoro kitevu cha Kilimo na Lishe anaeleza kuwa nchi haiwezi kuwa na maendeleo iwapo wananchi wake wana tatizo la lishe duni kwani maendeleo katika sekta zote yanategemea lishe bora.

Mtu mwenye Lishe bora anaweza kufanya shughuli za uzalishaji kwa ubora na ufanisi wa hali ya juu hivyo kujiletea maendeleo yeye na jamii yake pamoja na taifa kwa ujumla.

Joyce anashauri serikali na mashirika bionafsi kutilia mkazo suala la lishe bora kwa ajili ya ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla.

Elimu ya masuala ya lishe itolewe kuanzia mashuleni,vyuoni watu wawe na uelewa mkubwa juu ya masuala ya lishe na kuondokana na tatizo la

lishe duni kwasababu watanzania wengi hawana uelewa juu ya masuala ya lishe.

Prof. Joyce anasema kuwa, hali ya lishe nchini hairidhishi. Matatizo ya udumavu, utapiamlo na kwashakoo bado ni makubwa hivyo elimu zaidi

juu ya lishe inahitajika.

“Miaka ya nyuma elimu juu ya masuala ya lishe ilitolewa mashuleni lakini baada ya hapo ikasitishwa sijui umuhimu wa somo hilo

haukuonekana lakini sasa ni wakati wa muafaka wa kulirudisha somo hili,” anasema Prof. Joyce.

Kuna uhusiano mkubwa kati ya lishe na maendeleo kama hatutaweka kipaumbele katika masuala ya lishe tukayaacha nyuma maendeleo nayo yatabaki nyuma ni muhimu kuhamasisha lishe bora na virutubisho kila mahali kuanzia kwenye familia,jamii na taifa.

“Serikali na watunga sera wanapaswa kutambua uhusiano ulioko kati ya lishe bora na maendeleo ya taifa,elimu ya lishe na virutubisho itolewe

kuanzia ngazi ya familia,jamii hadi kitaifa na pia mashuleni somo la lishe lirudishwe ili kuchochea ustawi bora wa jamii na taifa” Anasema Prof.

Joyce.

Amesema kuwa, jamii ya wafugaji hususan wamasai wanakabiliwa na tatizo la udumavu, ukondefu na upungufu wa damu mwilini kwa kukosa kutumia mboga mboga na matunda na vyakula vingine  kwani jamii hiyo hupendelea

maziwa na nyama.

“Asilimia 16 wana kimo kisicholingana na umri wao yote haya yanasababishwa na lishe duni kwa baadhi ya watu,” anasema Prof. Joyce.

Profesa Tola Atinmo wa Chuo Kikuu cha Ibadan nchini Nigeria, Kitengo cha Virutubisho vya Binadamu amesema kuwa, haki ya kupata lishe na

virutubisho ni haki ya msingi ya kila binadamu kama ilivyoainishwa kwenye mkataba wa haki za binadamu wa kimataifa wa mwaka 1948.

Mdau wa Masuala ya Lishe, George Kajubi anashauri serikali kutilia mkazo suala la lishe na kutengea bajeti muhimu kila sekta lishe ili

kuwa na taifa lenye watu wenye afya bora watakaojenga taifa bora.

“Suala la lishe linahitaji utayari wa Wanasiasa na viongozi mwenye mamlaka nchini wanapaswa kuwa na sera zenye mikakati madhubuti ya

kuhimiza na kuhakikisha lishe inapewa msisitizo mkubwa kitaifa,” anasema Kajubi.

Lishe bora ni kichocheo cha ustawi bora wa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na siasa juhudi za kuinua kiwango cha lishe kuanzia ngazi ya familia, jamii na taifa zinahitajika.

Mwandishi wa makala hii ni Ferdinand Shayo anapatikana kwa namba, 0765938008 na email ni ferdinandshayo@gmail.com

error: Content is protected !!