August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lipumba wa jana si bora kuliko Lowassa wa leo

Spread the love

WAKATI Profesa Ibrahim Lipumba akiendelea kutumia jina la Edward Lowassa kama kinga ya usaliti wake dhidi ya CUF na UKAWA, baadhi ya wasomaji wa safu hii wameniuliza maswali kadhaa juu ya Lowassa, anaandika Ansbert Ngurumo. 

Nitajibu swali moja kwa mifano. Msomaji mmoja amesema: “Tafadhali naomba ujibu swali hili. Mimi ni Mkristo, naamini kauli za viongozi wangu wa dini. Nikiwa mfuasi wa Chadema, nimekuwa mtii kwa kauli na maagizo ya viongozi wangu. Viongozi wangu wakisema jambo hili ni baya, naamini. Niliwaamini Chadema walipotuambia kwamba Lowassa ni fisadi. Sasa walitumia kigezo gani kumpokea na kumteua agombee urais?”

Swali hili lilinikumbusha kauli ya Profesa Lipumba, aliyejivua uenyekiti wa CUF Agosti 2015 “kupinga hatua ya Chadema kumteua Lowassa kuwa mgombea urais kwa mwavuli wa UKAWA.”

Ameirudia majuzi kuwa ataendelea kumkataa Lowassa kwa kuwa alishirikiana na wanaCCM kupinga katiba mpya Bungeni. Kwa kuwa muuliza swali amejiegemeza kwenye dini, nami nitamjibu kwa  mwelekeo wa kidini. Kwa kifupi, kigezo walichotumia kumpokea na kuteua Lowassa ni kigezo kile kile walichotumia mitume kumpokea Sauli.

Tusome Biblia katika kitabu cha Matendo ya Mitume. Katika sura ya saba (7:54-60) wapinga ukristo walimuua mtume Stefano kwa mawe. Miongoni mwa walioshiriki mauaji ya Mtume Stefano, ni kijana aitwaye Sauli.

Mwanzoni mwa sura ya nane (8:3) kuna maneno haya: “Sauli akaliharibu kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani.

Sura ya tisa (9:1-2) inasisitiza: “Lakini Sauli akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea kuhani mkuu, akataka ampe barua za kwenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa njia hii, waume kwa wake,awafunge na kuwaleta Yerusalemu.”

Matendo 9:3-9 inasema: “Hata alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafla ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni. Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, ‘Sauli, Sauli, mbona unaniudhi?’ Akasema, ‘U nani wewe Bwana? Naye akasema, ‘Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe. Lakini simama uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda.’

“Na wale watu waliosafiri pamoja naye wakasimama kimya, wakiisikia sauti, wasione mtu. Sauli akainuka katika nchi, na macho yake yalipofumbuka, hakuona kitu; wakamshika mkono wakamleta mpaka Dameski. Akawa siku tatu haoni; hali, wala hanywi.”

Mistari ya 10-18 inatuonesha Sauli akiwa katika nyumba ya Yuda, akitembelewa na Ananiasi na kuponywa macho kwa maneno haya: “Ndugu Sauli, Bwana amenituma, Yesu, yeye aliyekutokea katika njia uliyoijia, upate kuona tena, ukajazwe Roho Mtakatifu. Mara vikaanguka machoni vitu kama magamba, akapata kuona, akasimama, akabatizwa, akala chakula, na kupata nguvu.”

Matendo 9:19-25 inasema: “Akawa huko siku kadha wa kadha pamoja na wanafunzi walioko Dameski. Mara akamhubiri Yesu katika masinagogi, kwamba Yeye ni Mwana wa Mungu.  Na wote waliosikia wakashangaa, wakasema, ‘siye huyu aliyewaharibu walioliitia Jina hili huko Yerusalemu? Na hapa si alikuwa amekuja kwa kusudio hilo, awafunge na kuwapeleka kwa wakuu wa makuhani?’

“Sauli akazidi kuwa hodari, akawatia fadhaa Wayahudi waliokaa Dameski, akithibitisha ya kuwa huyu ndiye Kristo. Hata siku nyingi zilipopita, Wayahudi wakafanya shauri ili wamuue, lakini hila yao ikajulikana na Sauli. Wakamvizia malangoni mchana na usiku wapate kumuua. Wanafunzi wake wakamtwaa usiku wakamshusha ukutani, wakimtelemsha katika kapu.”

Hata hivyo, wakristo walikuwa bado na woga. “Sauli alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi. Lakini Barnaba akamtwaa, akampeleka kwa mitume, akawaeleza jinsi alivyomwona Bwana njiani… naye akawa nao katika Yerusalemu.”

Sauli huyu ndiye baadaye aliitwa Paulo, akawa mtume wa mataifa. Paulo aliyepinga ukristo ndiye ametumwa kuhubiri ukristo kwa nguvu kubwa. Ndiye aliandika nyaraka kwa Warumi, Wakorintho, Wakolosai, Waefeso, Wafilipi, Wagalatia, Wathesalonike, Timotheo, na Tito. Alikuwa tayari kuvumilia taabu za kazi, kutembea, kuchoka, njaa, na kiu kwa ajili ya imani aliyowahi kupinga.

Paulo hakuwahi kuishi na Yesu kama akina Yakobo na Yohane. Na wongofu wake haukuwa wa kukusudia. Mabadiliko makubwa yalimtokea akiwa njiani kwenda kuumiza wakristo. Ndiye huyu ambaye aliuawa na Warumi kwa ajili ya ukristo.

Yuda Iskarioti aliishi na Yesu, akiwa mtunza hazina wao. Aliona miujiza mikubwa iliyotendwa na Yesu. Aliona maji yakigeuzwa divai, Yesu anatembea juu ya maji, wagonjwa wanaponywa, wafu wanafufuliwa. Lakini alipata ujasiri wa kumsaliti Yesu. Na alishindwa kutubu, akajiua. Kwa hiyo, mema yake yote aliyotenda huko nyuma yalipotea kwa tendo moja la mwisho – usaliti.

Profesa Lipumba alishirikiana na CCM kupinga UKAWA, akajivua uenyekiti wa CUF. Kama Yuda, alipoteza mema aliyokuwa amefanya kupitia CUF. Kinyume chake, Lowassa, aliyewahi kuhujumu upinzani, akashirikiana na UKAWA kusaka katiba mpya. Alipata heshima kama aliyopata Paulo kwa kujiunga na wanafunzi wa Yesu.

Kama Paulo alivyowahi kupinga ukristo, Lowassa naye aliwahi kupinga mabadiliko akiwa mwanaCCM. Sauli alishiriki mauaji ya Mtume Stefano. Lowassa alishirikiana na wanaCCM kuhujumu katiba mpya. Sauli aliongoka ghafla. Lowassa alibadilika ghafla akasema, “CCM si mama yangu.”

Wanafunzi walimwogopa na kumtilia shaka Sauli. Wapo baadhi ya wanaUKAWA waliomtilia shaka Lowassa. Barnabas alimpeleka Sauli kwa mitume. Freeman Mbowe alimtambulisha Lowassa kwa Chadema na UKAWA.

Tulipomsema na kumkosoa Lowassa, hakubadilika. Lakini alipopigwa na dhoruba ya CCM, alibadilika. Sauli  naye aliongoka baada ya kupigwa na dhoruba, si kwa mahubiri ya mitume. Sauli aligeuka Paulo, mtume wa mataifa; Lowassa amekuwa chachu ya mabadiliko ya kweli.

Sauli alileta taharuki kwa Wayahudi, wakataka kumuua mara kadhaa. Ni yale yale kwa Lowassa na CCM. Kwa kauli zao na vitimbi wanavyomfanyia, wamethibitisha hilo, na mara kadhaa, amenusurika katika majaribio magumu.

Kama Paulo alivyofanya kazi kubwa kuliko hata baadhi ya mitume walioishi na Yesu, Lowassa naye anaweza kushangaza wengi kwa kutumikia na kujenga Chadema kuliko hata baadhi ya wanachama aliowakuta.

Kwa sasa, Lowassa ni mwana UKAWA, anatetea katiba mpya. Anafanya kile ambacho Prof. Lipumba alishiriki kukianzisha, akakisaliti. Lipumba wa jana hawezi kuwa bora kuliko Lowassa wa leo.

Uchambuzi huu umechapishwa pia katika gazeti la MwanaHALISI, kwenye safu ya Maswali Magumu, Oktoba 3, 2016.

 

 

error: Content is protected !!