August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lipumba, Sakaya nje, CUF kuwaka moto

Spread the love

NDANI ya Chama cha Wananchi (CUF) kwafukuta baada ya kutolewa taarifa za kusimamishwa uanachama wa Prof. Ibrahim Lipumba pia kufukuzwa kwa Magdalena Sakaya na Maftaha Nachuma, anaandika Faki Sosi.

Prof. Lipumba alikuwa mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Sakaya -Mbunge wa Kaliua, Tabora pia Naibu Katibu Mkuu Bara na Nachuma-Mbunge wa Mtwara Mjini.

Viongozi wengine waliotimuliwa ni Abdul Kambaya, aliyekuwa Naibu Mkuugenzi wa Habari, Shashu Lugeye na Ashura Mustafa ambao ni wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi.

Uamuzi huo umefikiwa na Baraza Kuu la Uongozi wa chama hicho lilikokutana jana visiwani Zanzibar kujadili na kutathimini kuvunjika kwa Mkutano Mkuu wa wiki iliyopita baada ya kutokea kwa vurugu.

Kuvuliwa uanachama wa CUF kwa mujibu wa sheria kumewapotezea ubunge Sakaya na Nachuma.

“Tunasuburu taarifa yao, hapa ndio utajua kuwa CUF ya Bara haitaburuzwa na ile ya Zanzibar.

“Kila kitu lazima kifanyike kwa mujibu wa Katiba yetu, unawezaje kusema Haki Sawa kwa Wote halafu unafanya upuuzi wa namna ile. Tumejipanga na tutatekeleza,” amesema mjumbe mmoja wa Mkutano Mkuu kutka Ofisi Kuu ya CUF, Dar es Salaam aliyeomba kuhifadhiwa jina kwa sasa.

Kusimamishwa uanachama wa Prof. Lipumba kunatajwa kusababishwa na kuwa ‘chanzo’ cha vurugu zilizotokea wakati wa Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika wiki moja iliyopita katika Hoteli ya Blue Pearl na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh. 500 Mil.

Inaelezwa kuwa, wajumbe wengine waliofukuzwa wanadaiwa kuwa wafuasi wa Prof. Lipumba ndani ya chama hicho huku Sakaya akionekana waziwazi kuonesha upinzani dhidi ya hatua yoyote iliyotaka kuchukuliwa dhidi ya Lipumba.

Prf. Lipumba alijiuzulu Agosti mwaka jana kwa madai ya kutoridhishwa na hatua ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumkaribisha Edward Lowassa kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwa mgombea urais anayeungwa mkono na umoja huo.

Ukawa unajumuisha jumla ya vyama vinne ambayo ni CUF yenyewe, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha NCCR-Mageuzi na NLD.

error: Content is protected !!