Monday , 26 February 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Lipumba maji ya shingo
Habari za SiasaTangulizi

Lipumba maji ya shingo

Spread the love

GENGE linalojitambulisha kuwa linamwakilisha Profesa Ibrahim Lipumba katika kinachodhihirika kuwa na lengo la kukidhoofisha Chama cha Wananchi (CUF) likiwa limekwama kupata ruzuku, sasa limeamua kumtaka jaji ajitoe, anaandika Faki Sosi.

Hali hii imejionesha pale mawakili wa upande huo wakiongozwa na Mashaka Ngole, walipowasilisha mbele ya Mahakama Kuu, hoja ya kutaka Jaji Wilfred Dyansobera ajitoe katika usikilizaji wa kesi zilizofunguliwa wakati chama hicho kikikabiliwa na mgogoro mkubwa kiuongozi.

Wakili Ngole alitoa hoja kwamba Jaji Dyansobera asisikilize kesi hizo na badala yake jukumu hilo apewe Jaji Suleiman Kihiyo ambaye ndiye alianza kusikiliza kesi hizo katika hatua za mwanzo za ufungiliwaji wa kesi, kabla ya mawakili wa CUF kumtaka ajitoe.

Hoja hiyo ilikuja mahakamani tarehe 31 Oktoba 2017 (Jumanne wiki iliyopita), siku ambayo ilitarajiwa maamuzi mazito ya baadhi ya kesi hizo kutolewa baada ya usikilizaji wake kukamilika.

Jaji Dyansobera baada ya kusikia hoja hiyo, akitii muongozo wa Mahakama ya Rufaa Tanzania kwa suala kama hilo, alielekeza kwamba wenye nia hiyo wawasilishe hoja zao kesho yake – Jumatano.

Hata hivyo, wakili Ngole aliomba wapatiwe muda zaidi wa kujipanga na kuwasilisha malalamiko ya wateja wake. Na hatimaye, Jaji Dyansobera alipanga hoja za upande huo zisikilizwe Novemba 13.

Moja ya kesi hizo ni shauri Na. 51/2017 la Chama cha Wananchi ya kuomba kuwazuia Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini iliyosajiliwa kutokana na mapendekezo ya Profesa Lipumba wasifanye kazi ya Bodi hiyo mpaka pale shauri la msingi Na.13/2017 litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Mbele ya Jaji Dyansobera, mashauri yaliopo ni Na. 28/2017 linalohusu zuio la ruzuku, shauri Na. 68/2017 linalohusu kesi ya msingi ya kulalamikia kutolewa ruzuku isivyostahili, kesi ya msingi Na. 13/2017) inayohoji uhalali wa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya CUF iliyosajiliwa na Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (RITA) iliyofunguliwa na Ally Abdalla Saleh ambaye ni Mbunge wa Malindi.

Katika kesi hiyo ya kupinga bodi ya udhamini, walalamikiwa ni Profesa Lipumba na wenzake; Mwanasheria Mkuu wa Serikali na shauri la jinai Na. 50/2017 linalomhusu Prof. Lipumba pamoja na Emmy Hudson (Mkurugenzi Mwendeshaji wa RITA), Jaji Franscis Mutungi (Msajaili wa Vyama vya Siasa Tanzania) katika nafasi binafsi.

Hii inahusu tuhuma za kuwa walalamikiwa wameghushi nyaraka kwa nia ya kutaka kuingilia mwenendo wa mashauri yaliyopo mahakamani.

Katika hatua nyingine, usikilizaji wa mashauri hayo, uliingia mtihani mapema wiki hii, baada ya Wakili Ngole na mwenzake, Hosea Chamba, kujenga hoja za kutaka mahakama iondoe utaratibu wa usikilizaji kesi hizo kwa njia ya majibizano ya kimaandishi (Written Submissions).

Hoja yao ililenga kuzuia maelezo yaliyowasilishwa na Wakili Mpale Mpoki anayemwakilisha mbunge Ally Abdalla Saleh katika kesi iliyofunguliwa dhidi ya Prof. Lipumba na wenzake.

Suala linalorekebishika kwa mwasilishaji kuiomba mahakama chini ya kifungu cha 97 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai. Kufuatia hoja za wakili Ngole, mwanasheria Gabriel Malata anayemwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alitoa ufafanuzi wa kisheria ambao uliungwa mkono na mawakili Juma Nassor, Daimu Halfani, Hashim Mziray na Lovenes Denis wanaowakilisha CUF.

Shauri Na.  51/2017 lilishapangwa tangu awali kutajwa tarehe 7 Novemba 2017 wakati mashauri mengine yote yatatajwa tena tarehe 24 Novemba 2017 siku ambayo pia Jaji Dyansobera atafanya uamuzi kuhusu hoja za kumtaka ajitoe kwenye kesi hizo.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Hamahama Ngorongoro kutikisa maandamano ya Chadema Arusha

Spread the loveMAELFU ya wanachama na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na...

Habari za SiasaTangulizi

Waliofariki ajalini Arusha kuagwa siku ya maandamano Chadema

Spread the loveMIILI ya watu 25 waliofariki dunia katika ajali iliyohusisha lori...

Habari za SiasaTangulizi

Serikali kuiburuzwa mahakamani ajali iliyoua 25 Arusha

Spread the loveMTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), imeitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Samia atoa pole ajali iliyoua 25, kujeruhi 21 Arusha

Spread the loveRais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu...

error: Content is protected !!