September 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Lipumba: Magufuli ananyanyasa wafanyabiashara

Spread the love

PROFESA Ibrahim Lipumba, Mtaalam aliyebobea kwenye masuala ya Uchumi amesema Rais wa Tanzania John Magufuli anatumia cheo kuwanyanyasa wafanyabiashara, anaripoti Hamisi Mguta.

Lipumba ameyasema hayo katika mahojiano ya moja kwa moja na Kituo cha Runinga cha AzamTwo wakati akichambua sakata la ufichwaji wa sukari nchini.

Amesema kuwa endapo angekua anakaa na Rais Magufuli angehakikisha kunakuwepo na utaratibu wa uagizaji wa sukari kwa watu ambao ni waaminifu ambo hawatakwepa kodi zilizowekwa na kuagiza sukari ili pamoja na gharama na faida iweze kuuzwa kwa bei ya Tsh 1,800 ili viwanda vya ndani vinavyozalisha sukari viweze kulindwa.

“Tuepukane na kufanya mambo mazito ya sera kwenye majukwaa ya siasa na kuwatisha wafanyabiashara katika hali ambayo haiendani na halihalisi iliyopo,”amesema.

Aidha amesema wanasiasa wanapotengeneza sera na kufanya maamuzi kuijua hali halisi ilivyo.

Lipumba amesema hayo siku chache baada Rais John Magufuli kutangaza kutaifisha tani zote za sukari zitakazokamatwa zikiwa zimefichwa na wafanyabishara kwenye maghala na kisha kuzigawa kwa wananchi bure.

Hata hivyo Kwa siku za hivi karibuni kumekuwepo na malalamiko ya sukari kupanda bei kwa kuuzwa kwa Sh. 2,500 hadi 2,800 kutoka kikomo cha bei elekezi ya Sh. 1,800.

Rais Magufuli alipiga marufuku uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi bila ya kuwa na kibali cha serikali mapema mwaka huu ili kuondoa ushindani usio rafiki kwa viwanda vya ndani vya bidhaa hiyo.

Akilihutubia Bunge la 11, April Mwaka huu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema nchi inahitaji tani 420,000 za sukari kwa mwaka na kwamba uwezo wa viwanda vya ndani umekuwa ni tani 320,000 na hivyo kufanya kuwepo kwa nakisi ya tani 100,000.

Amesema pamoja na mpango huo wa kuagiza sukari kutoka nje, serikali itakuwa macho katika kuhakikisha kuwa sukari inayoruhusiwa kuingia ni ile inayotakiwa na si zaidi huku lengo la mkakati wa serikali ikiwa ni kuvifanya viwanda vya ndani kuendelea na uzalishaji hadi kuviwezesha kufikia uwezo wa juu wa kukidhi mahitaji ya nchi.

Amesema pamoja na upungufu uliopo, serikali inazo taarifa kwamba sukari iliyopo nchini hivi sasa inafikia tani 37,000, lakini baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakificha waliyonayo ili kusubiri kupanda kwa bei kutokana na upungufu uliopo.

error: Content is protected !!