June 19, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Lipumba kaajiriwa na nani kuivuruga CUF?

Spread the love

VITUKO, mapenzi na mahaba ya ghafla ya vyombo vya dola na hasa Jeshi la Polisi kwa mtu anayedaiwa kuwa Mwenyekiti Halali wa Chama cha Wananchi au kwa kimombo Civic United Front (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, yamenikumbusha mbali sana tena sana, anaandika Mwandishi wetu.

Mahaba ya Vikosi vya Operesheni vya Polisi chini ya Kamishna wa polisi Nsato Marijani, kwa Profesa Lipumba na wafuasi wake yamenikumbusha zama zile za miaka ya mwanzo ya 80 nilipokuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mvuha wilayani Morogoro Vijijini mkoani Morogoro.

Mapenzi ya ghafla ya Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam chini ya Kamishna wa Polisi Simon Sirro, yaliyowezesha kuvumilia maandamano ya Lipumba na wafuasi wake kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa hadi Buguruni Sokoni, zilipo ofisi za CUF yamenikumbusha enzi zangu za uhuni nilipokuwa kijana.

Nikiwa kijana mdogo wa miaka 25 tu, lakini wakati huo nikiwa miongoni mwa vijana wachache walimu tuliokuwa wahitimu wa kidato cha nne, niliteuliwa kuwa Mwalimu Mkuu na kuhamishwa kutoka Shule ya Msingi Kongwa kwenda Shule ya Msingi jirani ya Mvuha kuwa Mwalimu Mkuu.

Wenyeji wa Mvuha ni Wakutu na Waluguru wachache na wote ni wapenzi sana wa mpira wa miguu. Ikatokea siku moja tukapata mwaliko kwenda kucheza mpira na Shule ya Msingi Duthumi katika tarafa ya Bwakira huko huko Ukutu, Morogoro.

Kwa kushirikiana na walimu wenzangu wa kiume, diwani Vavatu, viongozi wa timu za Mvuha akina Jaka na Ali Mchemia, tulikula njama za kuwajumlisha wachezaji wa timu za Nyota na Faru za kijijini Mvuha kwenye timu ya shule ya Msingi ya Mvuha.

Katika njama hizo tulipanga pia namna ya kuwaaminisha wenyeji wa Duthumi, walimu na wanafunzi wao, kuwa watakaochezea timu ya Mvuha ni wanafunzi kweli hakuna mamluki. Tukakubaliana kukodi trekta la kubeba timu na kwamba tukifika Duthumi wachezaji wachelewe kidogo kwa makusudi.

Pia tukapanga kwamba watakapokuwa wamechelewa, mimi Mwalimu Mkuu niwaite kwa hasira na kufoka na kuwapa adhabu ya kuruka kichura ikiishia na viboko viwili viwili watu waamini kuwa anayekubali kuchapwa na Mwalimu lazima atakuwa mwanafunzi wa kweli.

Wote wakakubali ila kulikua na ombi moja kwamba: “lakini mwalimu usituumize, viboko visiwe vya nguvu sana vya kuchubua mtu tako.” Na kweli siku ya siku ikafika nami kwa ushambenga, nikajichanganya na walimu wa Duthumi na wakati ulipowadia timu ya shule yangu, Mvuha haionekani, eti wanacheza mtoni!

Basi, nikatuma kiranja kuwaita maana wanachelewesha mechi, vijana wakaja wanatembea goigoi kwa makusudi, nikawafuata kwa hasira, nikawaamuru kuruka kichura, huku nawacharaza bakora ya mti uitwao mkole, kule kwetu Mara tunauita ‘umokoma’ na balaa lake halielezeki kwa kelele, mateke na viboko juu.

Kila mtu kijijini Duthumi aliamini wanaochapwa na kuburuzwa ni wanafunzi. Na kwa bahati Waluguru, Wakwere, Wakutu, Wakami na Wazaramo wote ni wafupi, mrefu kati yao ana futi nne tu kasoro Jakaya Kikwete, yeye kapanda juu kidogo, hivyo vijana wale wa timu za Faru na Nyota walionekana watoto kumbe wana miaka  20 na ushei.

Duthumi kutia mguu uwanjani walifungwa nne kwa bila, tukarudi Mvuha kwa furaha tunashangilia kuanzia viongozi wa kijiji mpaka viongozi wa serikali. Siri ilikuwa moja. Duthumi walifungwa na kombaini ya Nyota na Faru wakidhani wamefungwa na Shule ya Msingi Mvuha! Siri hiyo! Siri sirini! Enzi zangu za uhuni hizo.

Hebu linganisha mfano huo na kitendo cha Jeshi la Polisi kumsindikiza Lipumba na wafuasi wake hadi Buguruni. Jamani Polisi hawahawa ambao wakisikia kuna mpango wa kuandamana wanaanza kutia jaramba mitaani kwa mazoezi ya kung fu, leo wanaona maandamano na hawafanyi chochote kuyazuia?

Jamani serikali yetu hiihii iliyorusha ndege na kufanya mazoezi ya kujihami na ukuta, leo inashindwa kuzuia watu 50 wanaoandamana barabarani, tena wanasindikizana na Polisi hadi ofisi za CUF, na kupanda ukuta, wanavunja mlango, makufuli na kumnyang’anya mlinzi bunduki!

Hivi kweli hakukuwapo makubaliano ya awali baina ya wafuasi wa Lipumba na Kamanda wa Operesheni Kamishna Nsato kwamba “andamaneni tu msitie shaka, sisi hatutachukua hatua? Kama hakukuwa na makubaliano hayo, wale waliojiamini na kupanda ukuta walipata wapi ujasiri ule mbele ya Polisi?

Kweli na ukali wote huu wa serikali ya John Pombe Magufuli mtu unajiamini kupanda ukuta bila hofu ya kupigwa risasi? Yaani askari wa Nsato wakashindwa hata kupiga risasi moja juu ya kutishia tu? Hapana, kuna namna hapa.

Mahaba haya ya Mkuu wa Operesheni wa Jeshi la Polisi, Kamanda …. Nsato kwa Lipumba kwanza yanafurahisha kwa wapuuzi na pili yanatia kinyaa kwa werevu hasa tukikumbuka kwamba Lipumba alikuwa mwanasiasa wa kwanza na wa pekee wa upinzani aliyekutana na Rais Magufuli mara tu alipoapishwa baada ya Uchaguzi Mkuu Novemba 2015.

Tungeelezwa wakati ule kama Lipumba alipoitwa au kukarbishwa kwa Mkuu wa Nchi kwa majadiliano, kama majadiliano yale yalihusu nini, tungeelewa. Tunaona hatukuambiwa yote yaliyojiri ndani ya Ofisi ya Raisi.

Sisi hatukuwepo lakini tunadhani siku ile Mheshimiwa Raisi alimwambia Profesa Lipumba hivi: “asante sana mwanakwetu kwa kuwasambaratisha Ukawa, sasa kajifanye unarudi CUF ili kuwachanganya zaidi na kuwagawa CUF, yaani fanya kama ile ya Mrema na Marando iliyoiua NCCR Mageuzi hadi leo.”

Kama si hivyo kumbe ni vipi? Kwa nini Lipumba awe mwanasiasa pekee kukutana na Magufuli baada ya ushindi? Why? Na baada ya hapo Lipumba asipate hata ubunge wa kuteuliwa, wala ubalozi, wala ukuu wa mkoa, wala ukatibu Tawala, wala ushauri wa uchumi wa raisi, wala unanihiii, wala unoni, kifupi haielezeki hii.

Nasema iko namna baina ya Profesa na Mkemia Mkuu wa Nchi, si bure. Halafu yanatokea haya yanayotokea Buguruni kwenye ofisi za CUF na Polisi wasichukue hatua yoyote nao wapo landrova nane? Hii haitofautiana na yetu ile ya Mwalimu Mkuu Nyaronyo kuchapa wanakijiji wanaojifanya ni wanafunzi ili kuwaaminisha watu kuwa timu inayocheza ni ya shule na hakuna mamluki.

Ukiangalia picha ya wale wanaompiga mlinzi wa CUF (uk 4 Mwananchi ya Jumamosi) hawaonekani kuwa wanachama wa CUF, wapo wanaosema ni wanausalama, wapo wanaosema ni polisi wa CID wanaovaa kiraia na wapo wanaodai eti ni magreen guard wa CCM waliojitolea kumsaidia Profesa kuua upinzani nchini.

Mimi sina uhakika, na picha zile naziona tu, na wahusika sijawahi kuwaona kwenye vikao vya ukawa, labda ni wana-CUF kweli, lakini vitendo vyao vinaonyesha ni wanaccm au mashushushu au mamluki.

Swali moja ambalo sina jibu lake, ni kwamba ni nani hasa kamwajiri Profesa wetu kuivuruga CUF? Na jee Profesa wetu analipwa shilingi ngapi hadi anakubali aibu anayoipata mbele za watu? Mimi na viongozi wa serikali ya kijiji cha Mvuha tulipata sifa ya kuifunga Shule ya Msingi Duthumi, Profesa Lipumba yeye anapata nini?

Makala hii imechapishwa pia katika gazeti la MwanaHALISI la tarehe 3 Oktoba, 2016.

error: Content is protected !!