Wednesday , 24 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Lipumba chali, Maalim Seif aanza kumpekua
Habari za Siasa

Lipumba chali, Maalim Seif aanza kumpekua

Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa CUF. Picha ndogo Prof. Ibrahim Lipumba
Spread the love

PROFESA Ibrahimu Lupumba, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ameangukia pua. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Katika kesi ya kupinga uteuzi wa Bodi ya Udhamini ya CUF uliyofanywa na Prof. Lipumba, Mahakama Kuu imeeleza kuwa, uteuzi huo si halali.

Pia Mahakama Kuu imetupilia mbali majina yaliyowasilishwa na Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa chama hicho ya wajumbe wa Bodi ya CUF kwamba, nayo hayakufuata taratibu na kwamba, si Lipumba wala Maalim Seif aliyefuata Katiba ya CUF katika uteuzi wa wajumbe wa CUF.

Kwa hukumu hiyo, wajumbe wa Bodi ya CUF Kambi ya Prof. Lipumba waliokuwa wamesajiliwa Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (Rita) wameng’olewa rasmi na kwamba, wajumbe wa Bodi ya CUF sasa ni wale waliokuwepo kabla ya tarehe 22 Juni 2017 ambao wanamaliza muda wao mwaka huu.

Akitoa uamuzi kwenye Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kuhusu wajumbe halali wa Bodi ya Udhamini ya CUF leo tarehe 18 Februari 2019, Jaji Benhajj Masoud amefuta bodi iliyoteuliwa na Prof. Lipumba na kwamba, ilikiuka Katiba ya chama hicho.

Uamuzi huo umetolewa kufuatia Ally Saleh, Mbunge wa Malindi na mfuasi wa Kambi ya Maalim Seif kufungua kesi namba 13 ya mwaka 2017 kupinga bodi iliyoundwa na Prof. Lipumba.

Ally aliiomba mahakama itamke kuwa, ni ipi bodi kilali (iliyoundwa na Prof. Lipumba na ile ya awali) kwa mujibu wa sheria za nchi na Katiba ya CUF 1992 toleo la mwaka 2014.

Ally kwenye kesi hiyo aliwakilishwa na Fatuma Karume, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) akisaidiana na Wakili Mpale Mpoki.

Mbunge huyo aliishitaki Rita kwa kukubali kusajili bodi mpya ya Prof. Lipumba ambapo alidai kwamba, baadhi ya majina yaliyowasilishwa Rita kusajiliwa hayakuwa halali.

Bodi iliyovunjwa na Mahakama Kuu leo ni yenye majina haya; Mussa Kombo, Asha Suleima, Hajira Silia, Amina Mshamu, Salha Mohamed, Peter Malebo, Azizi Dangesh na Abdul Magomba.

Saa chache baada ya Mahakama Kuu kutengua ‘Bodi ya Lipumba’, Maalim Seif amemwomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kufanya ukaguzi maalum wa fedha za ruzuku za chama hicho.

Maalim Seif ametaka ukaguzi huo ufanywe kwa kuwa, baada ya kutokea mgogoro, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliendelea kumuhudumia Prof. Lipumba.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Maalim Seif amesema, kwa kuwa Mahakama Kuu imetengeua uteuzi wa wajumbe hao, CAG anatakiwa kufanya ukaguzi maalum wa matumizi ya fedha hizo zilizotolewa.

“CUF tunamuomba CAG kufanya ukaguzi maalum wa fedha za ruzuku zilizotolewa na Jaji Mutungi kwa Lipumba na genge lake kupitia bodi feki ya wadhamini ambapo kwa kipindi chote waliipa uhalali bodi hiyo,” amesema Maalim Seif na kuongeza;

“Mahakama imeeleza kwamba RITA haikuzingatia matakwa ya kifungu cha 17 cha sheria ya muunganisho wa wadhamini, imekata mzizi wa fitina kuhusiana na madai yetu tuliyokuwa tunasema tangu awali kwamba, RITA haikuwa sahihi kuwasajili watu waliopitishwa na kikundi kilichojiita Baraza Kuu la Uongozi la Taifa bila kujiridhisha kama kweli kikundi hicho kilikuwa halali.”

Amesema, Mahakama Kuu imetamka wazi mbali ya kwamba ni masharti ya kifungu cha 17 cha sheria ya muunganisho ya wadhamini, Rita inapaswa isimamaie kikao cha kupitisha wadhamini wa taasisi yoyote.

“Lakini kwa mazingira ya CUF ambapo kuna kambi mbili zinazokinzana, walipaswa kujiridhisha zaidi kwa chombo kilichopitisha wadhamini,” amesema.

Aidha, Maalim Seif amewataka viongozi na wanachama wa CUF kuwa wataulivu wakisubiri uamuzi wa mashauri mengine yaliyobakia ikiwemo shauri Na. 23/2016 linalotarajiwa kutolewa maamuzi Ijumaa ya terehe 22 Februari 2019 katika Mahakama Kuu.

Chama hicho cha upinzani cha tatu kwa ukubwa Tanzania Bara na cha pili kwa Tanzania Visiwani, kilitumbukia kwenye mgogoro mkubwa mwaka juzi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

Habari za Siasa

Serikali kuanzisha mradi wa Gridi ya maji ya Taifa

Spread the loveWaziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema katika mwaka wa fedha...

Habari za SiasaTangulizi

Shibuda amlima waraka mzito Bulembo

Spread the loveMKONGWE wa siasa nchini, John Shibuda amemshukia kada maarufu wa...

error: Content is protected !!