August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lipumba azidi kusulubiwa Dar

Prof. Ibrahim Lipumba

Spread the love

WENYEVITI wa Serikali za mitaa wa Chama cha Wananchi (CUF) mkoa wa Dar es Salaam, wamemuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad na kumpuuza Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa vyama vya siasa nchini, Profesa Ibrahimu Lipumba juu ya wito wake wa kutaka kuwahoji kwa kile walichoeleza hana sifa za kufanya hivyo, anaandika Mwandishi Wetu.

Pia wameunga mkono tamko la Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Pwani Saed Kubenea ya kushirikiana katika operesheni yao inayojulikana kwa jina la ‘Ondoa Msaliti Buguruni’(OMB) iliyotangazwa kuanza hivi karibuni.

Akizungumza kwa niaba ya  wenyeviti hao, Bakari Kasubi wa mtaa wa Mtambani, amesema Lipumba hana sifa ya kuwaita kwa kuwa kwa mujibu wa Katiba alishafukuzwa chamani, hivyo atafute shughuli nyingine ya kufanya.

“Tunasikia eti wanaojiita viongozi wa chama walipora mamlaka isiyo yao wanaandaa utaratibu wa kuwaita baadhi ya wawakilishi wa chama, madiwani, wabunge na viongozi wa serikali za mitaa, kwa kile kinachoitwa kwenda kuhojiwa na kamati ‘feki’ ya maadili ya chama, hatuwezi kuhojiwa na watu hao,’’ amesema Kasubi.

Amesema wao wenyeviti wanaunga mkono juhudi na muelekeo uliochukuliwa na chama chao kutokana na maamuzi ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa  na msimamo wa chama uliotolewa na Katibu Mkuu wao.

Amesema wenyeviti wanaungana kupinga maamuzi ya RITA mbele ya Mamakama Kuu kwa kufungua kesi ambayo kwa mujibu wa kifungu cha 26 kwa kukiuka taratibu za sheria ya wadhamini na kesi nyingine zinazohusiana na hujuma ambazo walitaja kuwa ni fedha za ruzuku.

“Tunapingana kwa nguvu zote njama na mipango ya Msajili wa vyama vya siasa nchini Jaji Fransic Mutungi kwa kushindwa kuheshimu hadhi na nafasi yake mbele ya jamii na kujiingiza katika vitendo vya hovyo vyenye muelekeo wa kutaka kuiharibia mustakabali wa CUF  na kuwaathiri wadau mbalimbali walioshiriki katika kuasisi na kuijenga kwa takribani miongo miwili na nusu sasa,’’ amesema Kasubi.

Aidha amesema wanampinga Lipumba kwa kukubali kutumiwa na chama cha Mapinduzi (CCM) kwa maslahi yao binafsi  na kushindwa kuthamini mchango wa CUF katika kujenga demokrasia nchini.

“Lipumba leo amekuwa mtu wa kuweweseka ameshindwa kutumia taaluma yake kwa maslahi ya taifa,kila kukicha anatafuta msaada kwa vyombo vya dola  ili kufanikisha dhamira yake, ameshindwa kukemea vitendo viovu vinavyoendelea kufanywa na wafuasi wake wanapohudhuria mahakamani, kushambulia waandishi wa habari kauli za kashfa na kejeli dhidi ya viongozi,’’ amesema.

Ameongeza kuwa wito wao kwa wanachama na viongozi wa CUF kujiandaa vyema kukabilaiana na mfumo kandamizi wa demokrasia nchini na kuwashughulikia wale waliowaita vibaraka wanaotumika katika kuharibu demokarsia na kukivuruga chama hicho.

Juzi  CUF Unaoongozwa na Lipumba walitoa wito wa kuwaita baadhi ya wawakilishi wa chama, madiwani, wabunge na viongozi wa serikali za mitaa kwa ajili ya kuwahoji kwenye kamati ya nidhamu.

error: Content is protected !!