August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Lipumba awaponza Jaji Mtungi, Masaju

Wakili Hashimu Mziray akizungumza na waandishi wa habari

Spread the love

BODI ya Baraza la Wadhamini la Chama cha Wananchi (CUF), imefungua kesi dhidi ya Jaji Francis Mutungi, George Masaju, Profesa Ibrahimu Lipumba na wafuasi 12 waliotimuliwa na chama hicho katika Mahakama Kuu ya Tanzania, anaandika Shabani Matutu.

Jaji Mutungi ni Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Masaju ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Prof. Lipumba ni Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.

Bodi hiyo imefungua kesi hiyo ikiwa ni wiki chache baada ya mahakama hiyo kutoa kibali cha kufungua kesi dhidi yao.

Kibali hicho kilitolewa mbele ya Jaji Ama Isario Munisi ambapo alisema, mahakama ilijiridhisha kwamba, maombi ya bodi hiyo yaliyokuwa na hati ya kiapo cha Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad zipo sahihi, hivyo wanapaswa kufungua kesi hiyo ndani ya siku 14.

Hatua ya bodi kukimbilia mahakamani inatokana na kuibuka kwa mgogoro ndani ya chama hicho baada ya Prof. Lipumba kutangaza kujiuzulu nafasi ya Uenyekiti Agosti 6, mwaka jana na Juni mwaka huu, kutangaza kutengua barua yake na kisha kurejea kwenye wadhifa wake.

Bodi hiyo inayowakilishwa na mawakili zaidi ya 10 akiwemo Juma Nassoro, Hashimu Mziray na Twaha Taslima leo wamefanikiwa kufungua kesi iliyopokelewa na kupatiwa namba 23 ya mwaka 2016 chini ya hati ya dharura.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufungua kesi hiyo, Wakili Mziray amesema msingi wa kesi yao umejengwa katika hoja kubwa tatu ambazo;

Bodi imeiomba Mahakama Kuu kutengua barua ya Jaji Mutungi ya Septemba 23, mwaka huu iliyotengua uamuzi halali wa CUF, kumfuta uanachama Prof. Lipumba.

Pia bodi inaiomba mahakama hiyo kumzuia Jaji Mutungi kuendelea kufuatilia suala la CUF baada ya kupitishwa kwa uamuzi wa kumfuta uanachama Prof. Lipumba kwa kuwa, suala lake limefanyika kihalali.

Aidha katika hoja ya tatu, wanaiomba mahakama kumzuia rasmi Jaji Mutungi kutoingilia masuala yanayoihusu CUF, badala yake afanye kazi zinazomuhusu kisheria.

Badaa ya kueleza hayo, Wakili Mziray amesema sababu ya kufungua kesi hiyo chini ya hati ya dharura inatokana na hatari iliyopo ndani ya chama hicho.

“Licha ya kuwa kuna mambo yaliyotokea ndani ya chama, lakini kuna sababu ya kufungua kesi chini ya hati ya dharura kutokana na Ofisi Kuu ya chama pale Buguruni imekaliwa na watu ambao sio wanachama,”anasema na kuongeza;

“Lengo la chama ni kudhibiti ofisi zake zote katika hali ya usalama ikiwemo Makao Makuu, kwani Kaimu Katibu Mkuu anahitaji kusimamia kazi na shughuli za chama akiwa huru.”

Mbarara Maharagande, aliyeteuliwa kushika nafasi ya Unaibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano wa CUF amesema kuwa, chama hicho kinasikitishwa na utendaji kazi wa Jeshi la Polisi kwa kuwalinda na kuwaachia wahalifu wanaoivuruga CUF, badala yake inawakamata wasiohusika.

“Tunashangaa kuona polisi wanaharakisha kuwafikisha mahakamani wafuasi 23 waliokuja kuongeza nguvu ya kukilinda chama wakitokea Zanzibar, huku wakishindwa kuwachukuliwa hatua waliofanya tukio la utekaji ambalo ndio la kwanza kutokea,” anasema.

Maharagande anasema kutokana na hatua hiyo, asubuhi ya leo viongozi wa chama hicho wamekwenda Ofisi za Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswaro Mganga kuulizia hatma ya wafuasi waliohusika na tukio la utekaji iwapo wamechukuliwa hatua.

“Licha ya kufika ofisi hapo tumeshangazwa kuona hata kwenye orodha ya jalada la kesi za leo hakuna majina ya washtakiwa hao, licha ya kuwa wamekamatwa muda mrefu lakini wameshindwa kuchukuliwa hatua,” anasema na kuongeza; “hatua hiyo inayoonekana kuwepo kwa ubabaishaji wa kesi katika ofisi ya DPP na Jeshi la Polisi kushindwa kuwadhibiti wahalifu wanaoivuruga CUF.”

error: Content is protected !!