August 12, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lipumba atibua, ngumi zatawala

Spread the love

NDANI na nje ya Ukumbi wa Mkutano unaotumiwa na Chama cha Wananchi (CUF) katika Hoteli ya Blue Pearl, Ubungo jijini Dar es Salaam kufanya uchaguzi wa viongozi wa chama hicho kuna patashika, anaandika Charles William.

Nje ya ukumbi, wafuasi wa Prof. Lipumba na wale wasiomtaka wananyukana makonde. Hali ni tete.

Wajumbe wa mkutano huo walio ndani, wanaendelea na upigaji kura, baadhi yao wametoka nje – wamesusa.

Ni Mkutano Mkuu wa CUF uliotanguliwa na Baraza Kuu la Uongozi (BKUT) la chama hicho, lililopitisha majina matatu ya kuwania nafasi ya uenyekiti iliyoachwa na Prof. Lipumba baada ya kujiuzulu Agosti mwaka jana.

Hata hivyo Juni mwaka huu, Prof. Lipumba aliomba kurejea kwenye nafasi yake ya uenyekiti bila mafanikio.

Prof. Lipumba na sehemu ya kundi lake bado wamo ndani ya ukumbi wa mkutano, zogo kubwa linaendelea huku uamuzi wa kujadiliwa kwa barua ya kiongozi huyo aliyoomba kujuzulu ukiendelea.

Julius Mtatiro, Mwenyekiti wa kikao cha uchaguzi huo ametangaza uamuzi wa kupiga kura ili kuamua kwamba, barua ya Lipumba kujiuzulu iridhiwe ama la.

Tangu kuwasili kwa Prof. Lipumba na kundi lake ukumbini hapo, hofu ndani ya ukumbi huo ilianza kutawala kwa kuwa, hakutegemewa kuwasili na hata alipowasili aliingia kwa nguvu huku akilindwa na walinzi binafsi (mabaunsa).

Prof. Lipumba, alivamia mkutano huo na kundi lake akidai, anasubiri mjadala wa maombi ya barua yake ya kujiuzulu uenyekiti aliyomuandikia Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa CUF.

Hatua ya Prof. Lipumba ya kuvamia mkutano huo imetibua taratibu zote zilizokuwepo ndani ya ukumbi huo, kwani ameingia na watu wasiokuwa wajumbe wa mkutano huo lakini hata yeye pia si mjumbe halali wa mkutano huo wala hakualikwa hivyo hakupaswa kuwemo ukumbini.

Patashika hii inatokea ikiwa ni baada ya kupitishwa kwa majina matatu ya wanachama wanaowania nafasi ya uenyekiti wa CUF taifa.

Waliopitishwa kuwania nafasi hiyo ni Twaha Issa Taslima, wakili wa Mahakama Kuu, Riziki Mngwali, Mbunge wa viti maalum wa chama hicho na mfanyabiashara Juma Nkumbi ambaye pia ni kiongozi wa chama hicho wilaya ya Kinondoni.

Majina hayo yamepitishwa na BKUT lililoketi jana kujadili majina ya waombaji tisa yaliyofikishwa mbele ya mkutano mkuu maalum wa leo.

Kwa muda mrefu, ndani ya CUF kumekuwepo na makundi makuu mawili, moja likimtaka Prof. Lipumba na lingine likitaka atoswe.

Hoja za wanaomtaka Prof. Lipumba zimekuwa zikigemea katika Katiba ya CUF ya mwaka 1992, Toleo mwaka 2013 Ibara ya 117(2) inayoeleza kuwa,

‘Kiongozi aliyeandika barua ya kujiuzulu kwa katibu wa mamlaka yake atathibitishwa kujiuzulu kwake na mamlaka iliyomchagua baada ya kujadiliwa kwa barua yake ya kujiuzulu, na hatimaye kufanyiwa maamuzi.’

Maombi ya Prof. Lipumba kujiuzulu yalimfikia katibu wa mamlaka (Maalim Seif) na kwamba, kwa mujibu wa ibara hiyo, alipaswa kupeleka maombi hao katika Mkutano Mkuu wa chama hicho kuijadili barua hiyo na baadaye kujibu barua hiyo jambo ambalo mpaka sasa halikuwa limefanyika.

Baadhi ya wanachama ambao ni kundi la Prof. Lipumba, wamekuwa wakipaza sauti wakidai ‘bado ni mwenyekiti halali’ wakitaja kifungu hicho cha Katiba ya chama hicho.

Kura za wajumbe wa Mkutano mkuu zinatarajiwa, kuamua aidha kuidhinisha kujiuzulu kwa Lipumba au kumtaka aendelee kuwa mwenyekiti wa chama hicho.

Tutakuletea matokeo ya uchaguzi huo……

…………………………………………………………………………………………………..

Soma gazeti la MwanaHALISI kila Jumatatu kwenye simu yako kupitia, (bonyeza)> Mpaper kwa wateja wa Vodacom pia (bonyeza)> Simgazeti kwa wateja wa Vodacom, Tigo na Airtel. Pia unaweza kupakua (download) app ya Mpaper au Simgazeti kutoka kwenye playstore.

error: Content is protected !!