Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Lipumba amchambua Rais Samia, ampa 75%
Habari za SiasaTangulizi

Lipumba amchambua Rais Samia, ampa 75%

Spread the love

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amechambua uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassana ambapo amesema kwa kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake tathmini yake anampa asilimia 75 ya utekelezaji. Anaripoti Mwandishi Wetu… (endelea).

Prof. Lipumba ametoa uchambuzi huo dhidi ya Rais Samia kwa saa 1.04  leo tarehe 17 Julai,2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi Kuu za chama hicho zilizopo Buguruni Ilala jijini Dar es Salaam.

Amesema wakati Rais Samia anaapishwa Machi 19,2021 alipokea nchi ambayo misingi ya kidemokrasia, haki, usawa na utawala bora haizingatiwi ila kwa kipindi cha mwaka mmoja na miezi michache ameweza kuwafanya Watanzania wapumue.

“Taasisi inayofuatilia maendeleo ya demokrasia na uhuru duniani Freedom House kila mwaka inatoa Taarifa ya hali ya uhuru na demokrasia duniani. Freedom House inatathmini hali ilivyo juu ya haki za uhuru wa kisiasa na kijamii katika kila nchi na kutoa alama stahiki. Kwa kadri nchi inavyokaribia alama 100 ndivyo inavyoaminika kuwa na haki na uhuru mkubwa zaidi wa kisiasa na kijamii,” amesema.

Lipumba amesema katika taarifa yake ya mwaka 2021 Tanzania imepata alama 34 kati ya 100; ukilinganisha na 45 mwaka 2019, 52 mwaka 2018, 58 mwaka 2017, 60 mwaka 2016, 63 mwaka 2015, 64 mwaka 2014 na 66 mwaka 2013.

“Utafiti huu unaonesha hali ya uhuru na demokrasia nchini imekuwa ikipungua mfululizo katika kipindi cha Serikali ya awamu ya tano. Ukweli ni kwamba katika awamu ya tano demokrasia iliporomoka na uvunjifu wa haki za binadamu uliongezeka, ila Rais Samia ameanza vuzuri, hili lazima tukubali,” amesema.

Amesema wakati Taifa likielekea kuazimisha miaka 30 ya uwepo wa vyama vingi mwaka 2020 lilishuhudia uchaguzi ambao haukuzingatia vigezo vya klidemokrasia.

“Uchaguzi wa mwaka 2020 ulikuwa mbovu kuliko chaguzi zote za Tanzania au Tanganyika kupata Uhuru na Novemba 2 mwaka jana CUF tulieleza  uchaguzi uligubikwa na ubakwaji mkubwa wa demokrasia,” amesema.

Amesema uchaguzi huo uliondoka mazuri yaliyofanyika kuanzia mwaka 1995, hadi 2015 na kushuhudia mwaka 2020 upinzani ukipata asilimia 3 viti vyote.

Amesema katika uchaguzi huo mgombea Ubunge  jimbo la Temeke Zaynab Mndolwa, alipata kura sufuri kwenye kituo alichopigia kura yeye mwenyewe na wana familia yake ya watu saba.

MATUMAINI MAPYA

Mwenyekiti huyo amesema kuapishwa Rais Samia kulileta matumaini mapya nchini akifananisha na nuru ilichomoza katika mazingira ya hali ya kisiasa ambapo amebainisha kuwa kiongozi huyo anatoa kauli madhubuti lakini hazina vitisho.

Amesema baada ya Samia kuapishwa CUF kilimpongeza na kumshauri ajiwekee lengo binafsi la kushinda Tuzo ya Mo Ibrahim baada ya kumaliza kipindi cha uongozi wake, ikiwa ni kusimamia misngi ya kidemokrasia.

Lipumba amesema walimtaka ajenga misingi imara ya utawala bora na kupambana na ufisadi, kukuza demokrasia, kulinda haki za binadamu, kutekeleza sera zinazokuza uchumi, kuongeza ajira na kutokomeza umaskini jambo ambalo kwa asilimia fulani linatekelezwa.

Amesema pia walimshauri Rais Samia Serikali ifute kesi zote zinazotokana na purukushani za uchaguzi na atumie uzoefu wake kama Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba kukamilisha mchakato wa kupata Katiba Mpya itokanayo na maoni ya wananchi.

“Tumefarijika na msimamo wa Kamati Kuu ya CCM ulioelezwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka wa kuitaka Serikali kuangalia namna bora ya kufufua na kukwamua mchakato wa Katiba mpya kwa maslahi mapana ya Taifa.

Mtazamo huu wa CCM utasaidia sana kuwepo na mazingira ya kuleta mabadiliko chanya ya mfumo wa siasa nchini. Lakini ni kweli kuwa yote hayo yanatokana na utashi wa Rais Samia,” alisema.

Kuhusu Tume Huru ya Uchaguzi alisema anapongeza Rais Samia kuliona hilo na kuunda Kikosi Kazi, pamoja na ukweli kuwa Rasimu ya Katiba ya Jaji  Joseph Warioba na Katiba Pendekezwa vimeanesha namna ya upatikaji wa tume hiyo.

“Ni vyema Sheria ya Uchaguzi ikabadilishwa mapema kwa kuzingatia mwongozo uliopo ndani ya rasimu ya Katiba ili pawe na muda wa kutosha wa kuandaa uchaguzi ulio huru na wa haki miaka ijayo,” alisisitiza.

Eneo lingine ambalo CUF imedai kumuomba Rais Samia na kulitekeleza kwa asilimia 100 ni kuhusu maradhi ya Uviko-19, ambapo walimuomba aweke kando msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano na kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Jumuiya ya Kimataifa kwenye suala hili.

Lipumba alisema walishauri Tanzania itumie fursa ya kupata mkopo usiokuwa na riba kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kushughulikia chanjo, tiba na athari za Uviko-19 ambapo Serikali likuwa na fursa ya kukopa hadi dola milioni 569 bila riba yeyote.

“Tunashukuru mambo mengi tulioshauri Aprili mosi 2021 yamefanyiwa kazi. Serikal imejiunga na Jumuiya ya Kimataifa katika kushughulikia kadhia ya Uviko-19. Tanzania imepata mkopo wa masharti nafuu usio na riba wa Sh. trilioni 1.3,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema wakati akizungumza bungeni alisisitiza umuhimu sera nzuri za kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ili sekta binafsi iweze kushiriki kikamilifu kukuza uchumi na ajira jambo ambalo linatekelezwa kwa sasa.

Alisema dhamira ya kisiasa ya Rais Samia ya kuleta mabadiliko chanya katika mfumo wetu wa kisiasa ulijidhihirisha katika hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Maendeleo ya Demokrasia ulioandaliwa na Baraza la Vyama vya Siasa kwa kushirikiana na Msajili wa Vyama vya Siasa jijini Dodoma Desemba 15-17.

“Katika hotuba hiyo kauli iliyovutia sana ni pale alipoeleza kuwa “hii ni nchi yetu sote hakuna mwenye hati miliki ya nchi hii.” Alisisitiza Vyama vya Siasa vifanye siasa za kistaarabu za kujenga hoja na kueleza sera mbadala na siyo “siasa za chuki, uhasama, na zinazokwamisha maendeleo ya wananchi.”

Rais Samia alionyesha utashi wa kisiasa wa kufikia maridhiano na kujenga Tanzania mpya aliposema “yupo tayari kusikiliza viongozi wenzake, washawishiane kusameheana, kwa kuwa anajua kuna mengi ya kusikiliza, madukuduku, hasira, malalamiko, nongwa, yanayotokana na uchanga wa demokrasia.”

Lipumba alisema hotuba ya Rais Samia ililipa imani Kongamano kujadili hoja za ujenzi wa demokrasia kwa uwazi bila woga na kusababisha zaidi ya hoja 80 kulijitokeza katika mijadala.

Prof. Lipumba alisema andiko la Rais Samia siku ya kadhimisha miaka 30 ya Mfumo wa Vyama vingi limeongeza matumaini ya ujenzi wa demokrasia nchini Tanzania.

Ameandika kuwa “kwenye uongozi wangu anaamini katika kile kinachojulikana kama 4R ikiwa ni ufupisho wa maneno manne ya lugha ya Kiingereza; Reconciliation (Maridhiano), Resiliency (Ustahamilivu), Reforms (Mabadiliko) na Rebuilding (Kujenga Upya). Kwa kiswahili hizo 4R nitazipa jina la MUMKU,” alisema.

Rais ameeleza “Kwenye kujenga Tanzania bora anatamani kujenga jamii yenye maridhiano na maelewano. Ninatamani kujenga umoja pasipo kujali tofauti zetu za kisiasa, kidini, kikabila na nyingine zote.

Hili litawezekana kwa kujenga jamii inayopata haki sawa mbele ya sheria, isiyobaguana na inayotoa fursa sawa za kiuchumi kwa wote. Ninaamini maridhiano hayawezi kupatikana penye ubaguzi na pale ambapo kuna wanaokosa fursa na haki zao za kiuchumi na kiraia.” Hapa naona kama Rais amefafanua falsafa yetu ya Haki Sawa kwa Wote,” alisema Lipumba.

Lipumba alisema kuhusu Ustahimilivu Rais ameeleza “Huko tuendako tutatikiswa na kuyumbishwa. Iwe kiuchumi, kimazingira, kijamii na kisiasa lakini ni lazima tujenge ustahamilivu. Hii ni kwa sababu hatuna nchi nyingine zaidi ya hii na hapa ndiyo kwetu.”

Katika suala la Mabadiliko Rais kaandika “Amedhamiria kwamba kwenye kuenzi miaka yetu ya demokrasia ya vyama vingi, Serikali yake itajitahidi kufanya mabadiliko katika mifumo ya kisiasa, kiuchumi na katika sheria zetu za uchaguzi.

Mabadiliko katika sheria zetu za uchaguzi yataleta ushindani wa haki na kuwapa watu fursa ya kuwachagua wawatakao kuwaongoza. Kwenye uchumi, mabadiliko yatakuwa na lengo la kutoa fursa zaidi kwa watu wengi zaidi kunufaika kiuchumi badala ya wachache.”

Rais Samia ana lengo la Kujenga Upya kwa sababu “Ninafahamu kwamba wananchi hawali maridhiano, ustahamilivu wala mabadiliko. Mwisho wa siku lengo kuu linatakiwa kuwa ukuaji wa uchumi wetu. Uchumi utakaoongeza ajira kwa vijana wetu na utakaofungua fursa kwa makundi yote ya kijamii yaliyo nchini”

Maelezo ya Malengo ya Rais Samia ni mazuri. Anastahiki kupongezwa na kuungwa mkono. Hata hivyo maneno mazuri hayatoshi. Kunahitajika utekelezaji.

Lipumba alisema MUMKU au 4R inatakiwa kuwekewa mpango wa utekelezaji unaoenda kwa wakati ikiwemo kutunga au kurekebisha sheria na bajeti ya kutekeleza mipango ya uchumi.

Alisema wanatoa wito kwa Kikosi Kazi kukamilisha majukumu yake na serikali kuandaa Mpango wa Utekelezaji wa Tume Huru ya Uchaguzi itakayoendesha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.

Pia ametaka mchakato wa kupata Katiba mpya inayotokana na maoni ya wananchi ufanyike, kurekebisha na kulijenga upya Jeshi la Polisi liheshimu haki za binadamu na liwe na weledi

Mwenyekiti alisema jambo lingine ni kurekebisha Sheria ya Vyama vya Siasa ya 2019, kuandaa dira ya Taifa shirikishi, kuboresha mazingira ya kufanyabiashara na uwekezaji, upambana na ufisadi na kujenga utawala bora na kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Lipumba aliwaambia wanachama wa CUF kuwa wanwajibika kutambua na kuyaenzi mabadiliko ya mazingira ya kisiasa na waondokane na uduwanzi na kukatishwa tamaa kuliko kithiri katika uongozi wa awamu ya tano.

“Ninatoa wito maalum kwa watanzania na hasa vijana wa kike na wa kiume kutumia fursa mpya ya kisiasa kujiunga na chama cha CUF kilichojikita katika lengo muhimu la kudai haki sawa kwa wote ikiwa ni pamoja na haki za kisiasa,  kiuchumi, kijamii, mazingira na utamaduni.

1 Comment

  • Prof una maana gani Aprili 2021 “alipokea nchi”? Yeye alikuwemo sana ndani ya serikali aliyoipokea. Katika mbio ya relay race huwezi kusema aliyeshinda ni yule tu aliyepokea kijiti na akamaliza mbio. Ni team work. Sikubali kuwa JPM angeweza kufanya alichofanya angelikuwa peke yake bila ya kusaidiwa na makamo wa rais na waziri mkuu na kadhalika.
    Katika kesi ya Nurenberg trial wale wasaidizi wa Hitler walisema wao walikuwa wakifuata amri tu wala hawakukubaliana naye. Hata hivyo mahakama iliwakuta wana hatia. Katika sheria hii inaitwa aiding and abeting. Prof na wengine wanapaswa wajue hii
    TUSIWE WANAFIKI

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!