Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Lipo doa, NEC itazamwe vizuri
Makala & Uchambuzi

Lipo doa, NEC itazamwe vizuri

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage
Spread the love

MFUMO wa uendeshaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini (NEC) unalalamikiwa – kwa muda mrefu sasa kutokana na madai ya kushindwa kubeba uhuru na uwazi katika shughuli zake. Anaandika Yusuph Katimba … (endelea).

Wanaolalamika ni wengi; kuanzia viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani na wagombea wa nafasi mbalimbali za kuchaguliwa kupitia sanduku la kura.

Pia wamo wanaharakati na wafuatiliaji wa masuala ya uchaguzi katika ngazi mbalimbali, wasomi na hata wananchi wa kawaida.

Malalamiko yamekuwa yakitolewa tangu kuanza kwa mchakato wa kuandikisha wapigakura, uwasilishaji na uhakiki wa taarifa zao, matangazo na hata wakati mwingine ratiba za zoezi la kupiga kura.

Mbali na hayo, pia wanaolalamika wamekuwa wakilaani uendeshaji na usimamizi wa kupiga kura na hatua za kutangaza washindi.

Mifano ya malalamiko hayo ipo mingi na wengi wanaolalamika wanajenga msingi wao wakisema kuwa “wanaonewa” kwa kuwa hawako ndani ya chama tawala- Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ieleweke kuwa sheria za Tanzania zinampa madaraka mgombea mmoja miongoni mwa wagombea wa nafasi ya urais, kuwa mteuzi wa viongozi wa juu wa NEC. Tume ambayo inasimamia uchaguzi, naye akiwa anatafuta nafasi ya kutangazwa na anaowateua.

Hawa ni pamoja na mwenyekiti wa NEC na wajumbe wote na pia mkurugenzi wa tume ambaye ndiye mtendaji mkuu wa kazi za tume hiyo ya uchaguzi.

Mbali na viongozi hao, pia mwenyekiti wa chama tawala- ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndiye mteuzi wa wasimamizi wakuu wa mchakato wa uchaguzi kwa ngazi chini; wasimamizi hawa ni wakurugenzi wa halmashauri.

Wakurugenzi husimamia shughuli zote za uchaguzi kwa niaba ya tume na wao ndiyo hutangaza matokeo ya madiwani na wabunge.

Kimsingi, wateule hawa wa mgombea mmoja wa kinyang’anyiro cha urais, ndiyo wamekuwa wakilalamikiwa kila mara.

Mazingira ya kawaida, kwa mtu mwenye akili timamu, akili inakataa kuamini kuwa mteule wa mmoja wa wagombea au wale wanaomuunga mkono wanaweza kutanganzwa wamshinda, wakati mtangazaji na msimamizi wa uchaguzi ni mteuliwa kutoka timu yao?

Hoja hii ya wateule hawa kupewa nafasi na mmoja wa wagombea kusimamia uchaguzi anaoshiriki, imekuwa ikiibua malalamiko kila siku; kabla, wakati na baada ya kila uchaguzi.

Lakini majibu wanayopewa na wakubwa wa tume hiyo na hata serikali ni kwamba, hakuna tatizo lolote ikiwa misingi ya sheria inasimamiwa ipasavyo.

Majibu haya na mengine yanayofanana na haya yamekuwa wakiwaumiza vichwa wanaolalamikia utendaji wa tume hiyo ya taifa ya uchaguzi.

Ni katika kuumiza kichwa, Mbunge wa Ubungo (Chadema) Saed Kubenea akaamua kuandaa na baadaye kuwasilisha hoja binafsi bungeni ili wawakilishi hao wa wananchi; wakiwa wanaongoza mhimili mwingine wa dola, watoe msimamo.

Hatua hii ya Kubenea ni mwangi wa mtazamo wa wengine wengi kwamba “haki” wanayoipigania inaonekana kutopatikana kutoka kwa walalamikiwa.

Katika barua yake aliyoiwasilisha bungeni Dodoma, Kubenea anaeleza kuona hatari inayoweza kutokea siku za usoni ikiwa wananchi wengi wataona haki ya sanduku la kura haifuatwi katika kuwapata viongozi wanaowapenda.

Katika barua hiyo anaeleza kuwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi haiko huru kusimamia uchaguzi wa haki na matakwa ya wananchi. Barua hiyo aliiwasilisha Alhamisi Machi 8, 2018 katika ofisi ya Katibu wa Bunge mjini Dodoma.

“Tusipokuwa makini na kurekebisha hali ya sasa ya tume ya uchaguzi, Tanzania inaweza kutumbukia katika machafuko ambayo yataharibu kabisa sifa za Tanzania na watu wake,” aliandika Kubenea.

Anasema, wananchi wenye nia njema na Tanzania kamwe hawawezi kuiacha hali hii iendelee, ndiyo maana akaamua kupeleka bungeni hoja binafsi ili, ikiwezekana, utolewe msimamo wa kuzuia kutokea kwa machafuko yanayosababisha na mchakato wa uchaguzi.

“Tangu nchi iingie katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, uchaguzi mkuu umekuwa ukifanyika kwa kusimamiwa na tume isiyokuwa huru na ndiyo maana kumekuwa na malalamiko mengi mno, tunahitaji kubadilika,” anaeleza.

Hata hivyo, kama ilivyotarajiwa, hoja ya Kubenea, ilikutana na kigingi kutoka kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye alieleza umma kuwa hoja hiyo “hakuielewa.”

Spika Ndugai alisema, Kubenea anapaswa kujipanga upya, kama anapenda kuwasilisha tena hoja yake ili iweze kujadiliwa na bunge.

Alisema; “naikataa taarifa ya mheshimiwa Kubenea, akajipange upya kama bado anaona anataka kuileta bungeni.

“Kama bado una nia uje katika utaratibu unaotakiwa kama hatukukuelewa, tutatafuta muda ili tueleweshane zaidi ila sisi tumeelewa hivyo.

“Mheshimiwa Saed Kubenea ameleta kusudio la kuwasilisha hoja binafsi bungeni akitaka Bunge lifanye marekebisho ya masuala yanayohusiana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

“Ili ikidhi matakwa ya mfumo wa vyama vingi hapa nchini sasa kwa kuwa Tume hiyo ya Taifa ya Uchaguzi imeanzishwa na Katiba katika ibara ya 74 marekebisho yote juu ya tume hiyo yanatakiwa kuletwa kwa kupitia muswada wa marekebisho ya Katiba na siyo hoja binafsi ya mbunge,” aliongeza Ndugai.

Pamoja na kuwepo kwa kile kinachoweza kuelezwa kuwa ni upungufu katika kuwasilisha, ni vyema ikaeleweka kuwa njia zote hizo zote haziondoi uzito wa kile kinachowasilishwa, hivyo ni vyema Kubenea akaona namna nzuri ya kuwasilisha hoja yake.

Hoja ya Kubenea inabeba mashiko ambayo ni kilio cha wengi na inaweza kuleta mwanga ikiwa itapata nafasi ya kupokelewa na kujadiliwa na wabunge.

Kinachopiganiwa na Kubenea kimekuwa kilio cha wengi na mbunge huyo anabeba malalamiko ya wengi ambayo yamekosa majibu muhimu ili kuleta haki katika mchakato mzima wa uchaguzi.

Katika mazingira ya sasa ya vyama vingi, upungufu katika utendaji wa NEC unaonekana hasa kwa watendaji wake kuwa wateuliwa wa mmoja wa wagombea wa nafasi kubwa ya kuongoza nchi yetu. Hii ni njia rahisi mno ya kuonekana kwamba haki haiwezi kutendeka.

Ni vyema basi, Kubenea akafanya linaloonekana kuwa sahihi, ili kuwasilisha hoja yake upya, ipokelewe na wabunge wapate mwanya wa kuijadili ili hatimaye upatikane uamuzi utakaokuwa mwanga wa haki katika uchaguzi kwa kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi Tanzania.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaMakala & Uchambuzi

Kanda ya Ziwa yaonyesha NMB inavyosaidia afya ya mama na mtoto

Spread the loveMafanikio inayozidi kupata Tanzania katika kupunguza vifo vya mama na...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

‘Mwanapekee’ wa Rais Samia: Atabadili nini Arusha?

Spread the loveMAPEMA wiki hii, baadhi ya viongozi walioapishwa na Rais Samia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kipunguni waihoji serikali, ziko wapi fedha za fidia?

Spread the loveWATU wanaodai kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu,...

Habari za SiasaMakala & UchambuziTangulizi

Askofu Bagonza: Tusichonganishwe; tusichokozane na tusikufuru

Spread the loveJOTO la chaguzi linapanda kila siku hapa nchini. Upo umuhimu...

error: Content is protected !!