LIGI kuu soka Tanzania Bara inaendelea tena leo kwa kupigwa jumla ya michezo minne katika viwanja tofauti mara baada ya mapumziko ya michezo ya kirafiki na kimashindano ya kalenda ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani ‘Fifa.’ Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).
Mchezo wa mapema leo utawakutanisha JKT Tanzania ambao watakuwa nyumbani dhidi ya Ruvu Shooting, mechi itakayochezwa majira ya saa 8 mchana kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.
Mechi nyingine tatu zitachezwa majira ya saa 10 kamili jioni, ambapo KMC watawakaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam na Biashara United atakuwa kwenye dimba la Karume mkoni Mara kuwaalika Ihefu FC kutoka Mbeya.

Baada ya kupoteza dhidi ya Azam FC, klabu ya Kagera Sugar itakuwa na wakati wa kujiuliza mbele ya Namungo FC kwenye mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Majaliwa, Luangwa mkoani Lindi.
Mpaka ligi hiyo inasimama Azam FC walikuwa juu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 15 huku nafasi ya pili ikishikwa na Simba yenye pointi 13 sawa na Yanga aliyeshika nafasi ya tatu.
Leave a comment