September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

LHRC yataka Polisi iharakishe uchunguzi tukio la Mbowe 

Spread the love

TUKIO la kushambuliwa na watu wasiojulikana lililomkuta Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), usiku wa kuamkia Jumanne tarehe 9 Juni 2020, limekiibua Kituo cha Sheria na Haki za Bonadamu Tanzania (LHRC). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

LHRC kupitia Anna Henga, Mkurugenzi Mtendaji, jana Jumanne kilitoa tamko la kulaani tukio hilo, lililotokea nyumbani kwa Mbowe, maeneo ya Area D jijini Dodoma.

Kituo hicho cha kutetea haki za binadamu, kimelitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa haraka juu ya tukio hilo, ili kuhakikisha waliohusika wanafikishwa katika mikono ya sheria.

“LHRC inatoa wito kwa Jeshi la Polisi nchini kufanya uchunguzi wa haraka juu ya tukio hilo ili kuhakikisha wahalifu wanafikishwa kwenye mikono ya sheria, kwani tukio hilo linaleta taswira mbaya juu ya usalama wa wananchi,” amesema Henga.

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe akipandiswa kwenye Ambulance kwa ajili ya kuelekea Airport kwenda Dar Es Salaam kwa Matibabu Zaidi.

LHRC kimeungana na wito wa Spika Job Ndugai, wa kulitaka jeshi hilo kuharakisha uchunguzi wa awali, kisha kutoa taarifa juu ya tukio hilo, ili kuepusha uzushwaji wa maneno ya uongo kuhusu kushambuliwa kwa mwenyekiti huyo wa Chadema.

Spika wa Bunge, Job Ndugai jana wakati akizungumza bungeni jijini Dodoma, aliwaahidi wabunge kwamba, leo Jumatano tarehe 10 Juni 2020, majira ya jioni atakuwa na cha kusema juu ya tukio hilo.

Pia, Spika Ndugai alivitaka vyombo vya dola kutoa taarifa haraka ya tukio hilo ili ukweli uweze kujulikana.

Kwa sasa Mbowe anatibiwa katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam, baada ya kuhamishwa kutoka jijini Dodoma.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI ONLINE & MwanaHALISI TV kwa habari zaidi

error: Content is protected !!