July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

LHRC yataja tamu, chungu mapendekezo bajeti 2022/23

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga

Spread the love

 

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimeipongeza Serikali kwa kuja na bajeti inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja, huku ikiiomba ifanye marekebisho katika masuala kadhaa, ambayo yana changamoto. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Pongezi na ushauri huo umetolewa leo Ijumaa, tarehe 17 Juni 2022, jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga, akitoa uchambuzi wa kituo hicho kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2022 iliyowasilishwa hivi karibuni bungeni jijini Dodoma, na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. MwiguluNchemba.

Henga amesema, bajeti hiyo imebeba masuala ya wananchi ikiwemo katika sekta ya kilimo kwa kuongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo hadi kufikia Sh. 954 bilioni, kutoka Sh. 294 bilioni, iliyotengwa 2021/22.

“Kilimo cha Tanzania kimekuwa kikifanyika katika mazingira duni yenye matokeo yasiyo tabirika. Suala la wakulima walio wengi kutegemea mvua kwa ajili ya uzalishaji ni suala ambalo sio endelevu na linalokatisha tamaa. Lakini Serikali imepanga kuongeza idadi ya kilimo cha umwagiliaji hii itafanyika kwa kuongeza eneo kufikia Hekta 8,500,000 ambazo zinategema kupunguza tatizo la umasiki kwa vijana na wanawake,” amesema Henga.

Suala lingine ambalo lililotajwa na Henga kuwa litaleta nafuu kwa wananchi, ni bajeti kuondoa kodi ya ongezeko la thamani kwenye mafuta ya kula yanayozalishwa nchini, pamoja na kuongeza uwekezaji katika mazao ghafi ya mafuta ya kula hususan michikichi na alizeti.

“Hatua hizi za kibajeti zinatarajiwa kuleta matokeo chanya katika maeneo mawili, kwanza ongezeo la bajeti litapelekea kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao hayo na pili upatikanaji uliowezeshwa kwa pembejeo utapelekea kuongezeka kwa uzalishaji.

Mkurugenzi huyo wa LHRC, amesema bajeti hiyo imetoa nafuu kwa wananchi katika suala la elimu, kwa kuondoa ada kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita, kutenga Sh. 8 bilioni kwa ajili ya kuanzisha dirisha maalum kwa ajili ya kusaidia watoto wanaotoka katika familia duni ikiwemo kwa kujenga mabweni.

Henga amesema, bajeti hiyo imeongeza kiwango cha malipo ya mafao ya mkupuo kutoka asilimia 25 iliyoamuliwa 2018, hadi asilimia 33, kushusha kiwango cha tozo za miamala ya simu, kutoka Sh. 7000 hadi 4000, pamoja na kuongeza kima cha chini cha mshahara kwa asilimia 23.3.

Kuhusu mapungufu ya bajeti hiyo, Henga amesema haijajibu kilio cha Watanzania kuhusu bima ya afya kwa wote huku akiiomba Serikali kuzingatia hitaji la kutenga bajeti kwa ajili ya suala hilo.

“Kwa watetezi wa haki za binadamu na usawa wa kijinsia, bajeti ya 2022/23 imekuwa na mapungufu kadhaa ya kijinsia, kwa mfano LHRC imekuwa na mshangao kuwa bajeti inapendekeza kushushwa kwa asilimia mikopo ya wanawake kupitia halmashauri kutoka asilimia nne hadi mbili,” amesema Henga.

Mapungufu mengine yaliyotajwa na Henga kuhusu bajeti hiyo, ni ada mpya za ving’amuzi, akiiomba Serikali kuiondoa kwa kuwa itaongeza gharama za vifurushi na kuongeza mzigo kwa wananchi kisha kuminya haki ya kupata taarifa.

error: Content is protected !!