January 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

LHRC wawakumbusha polisi kuachia vifaa vyao

Spread the love

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimezidi kulipigia kelele Jeshi la Polisi kwa kuendelea kuvishikiria vifaa vilivyokuwa vikitumiwa na wadau mbalimbali katika uchunguzi wa ndani kwenye uchaguzi mkuu uliopita. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Vifaa hivyo vinavyoshikiliwa na Jeshi la Polisi vilikamatwa 29 Octoba 2015 baada ya polisi kuvamia kituo cha kazi kilichopo Mbezi Beach, Jijini Dar es Salaam, licha ya ukweli kwamba kituo hicho kilipewa ruhusa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kushiriki katika uchaguzi.

Kituo hicho kilichokuwa kinatumiwa na wafanyakazi wa shirika la TACCEO, linalofanya kazi pamoja na LHRC, kinadaiwa kwamba kilivunja sheria ya mitandaoni ya mwaka 2015 kifungu cha 16 kwa kusambaza taarifa za uchaguzi zisizo rasmi mitandaoni.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mwenyekiti wa LHCR, Israel Ilunde, amesema kuwa licha ya vifaa hivyo kuendelea kushikiliwa hakuna taarifa yoyote ya kueleweka kutoka Polisi inayoonyesha uhusiano uliopo kati ya makosa wanayotuhumiwa kufanya na vifaa hivyo.

“Tulinyang’anywa simu za ofisi, simu binafsi , laptop na kompyuta za ofisi wakidai kuwa tumevunja taratibu. Tangu siku hiyo tunahudhuria polisi hakuna lolote linaloendelea. Wamekwishatuhoji wafanyakazi wote kwa nyakati tofauti lakini bado hawarudishi,” amesema Ilunde.

Ilunde amesema kuwa, kitu kinachofaywa na Jeshi la Polisi kuendelea kuvishikilia vifaa hivyo ni uvunjaji wa haki za binadamu kwani wananchi wana haki ya kujua kilichoendelea katika uchaguzi mkuu.

“Hadi sasa bado hatujatoa ripoti yetu tuliyoifanya katika uchunguzi wetu kwani taarifa nyingi zipo kule, tunaomba Polisi waturudishie vifaa vyetu ili tuendelee na utoaji ripoti” amesema Ilunde.

Mpaka sasa wamefanikiwa kutoa taarifa ya awali ya uchaguzi mkuu uliopita 29 Octoba 2015. TACCEO walifanya uchunguzi katika majimbo zaidi ya 200 katika nchi nzima.

Amesema kuwa, uchunguzi huo uliofanywa katika kipindi cha uchaguzi pia uliwahusisha wadau wengine 17 kutoka katika Taasisi za kirai zilizopo nchini. Taasisis hizo ni pamoja na Tanzania Gender Networking Program (TGNP), Tanzania Media Women Association (TAMWA), na Policy Forum Tanzania.

Amesema kuwa, kwa mujibu wa wachunguzi 2100 waliokuwa wamesambazwa katika majimbo 200 nchini walibaini kasoro nyingi zilizojitokeza katika uchaguzi mkuu uliomalizika.

Kasoro hizo ni pamoja na uchache wa vifaa vya BVR, kuchelewa kujisajili, uchache wa vituo vya kujisajili, umbali wa vituo ambapo ilipelekea baadhi ya watu kutojiandikisha, uangalizi wa walemavu na wenye mahitaji muhimu haukuzingatiwa.

Kasoro nyingine ni, wanafunzi wa vyuo wengi hawakujiandikisha, utoaji wa elimu ya mpiga kura haukuwa mzuri, ndani ya vyama kulijawa na rushwa, ucheleweshwaji wa vifaa vituoni, kuchelewa kwa kutangazwa kwa matokeo, unyanyasaji wa kijinsia pamoja na utumiaji mbaya wa mali ya umma.

“Hatuwezi kusema kwamba uchaguzi ulikuwa huru na wa haki. Bali sisi tuna haki ya kutoa taarifa ya kile tukichokiona. Hiyo ni taarifa fupi ya awali lakini taarifa nyingi zipo katika vifaa vilivyokamatwa na polisi,” amesema Ilunde.

error: Content is protected !!