December 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

LHRC: 43% ya wafanyakazi hawajui haki zao

Anna Henga, Mkurugenzi Mtendaji LHRC

Spread the love

MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga amesema, asilimia 43 ya wafanyakazi waliowahoji, hawajui haki zao. Anaandika Hamis Mguta…(endelea).

Henga ameeleza hayo leo tarehe 14 Novemba 2019, jijini Dar es Salaam wakati akizindua Ripoti ya Haki za Binadamu na Haki za Biashara ambayo hutolewa kila mwaka.

Amesema, ripoti hiyo imeibua mambo mengi ikiwemo suala la  ufahamu wa wafanyakazi mbalimbali juu ya haki zao, mikataba ya ajira na mapunziko.

Na kwamba, ripoti hiyo imeonesha asilimia kubwa ya wafanyakazi, hawana muda wa kupunzika kutokana na mikataba yao kuwa ya kulipwa kwa siku, hivyo ulazimika kwenda kazini kila siku ili alipwe.

“Tumegundua wengi hawajui haki zao kwasababu tulikuwa tunawauliza ulifanya nini ulipovunjiwa haki yako?asilimia 29 walisema, waliripoti kwa bosi.

“… lakini asilimia 43 walisema, hawakuripoti chochote hivyo hii inamaanisha hawajui utaratibu wa kufanya pindi anapovunjiwa haki zao,” amesema.

Fundikila Wazambi, mtafiti anayefanyabkazi kwenye kituo hicho amesema, kwa mwaka 2019, asilimia 84 ya wafanyakazi wameonekana kuwa na mikataba ya ajira, lakini uelewa wao bado changamoto pia hawajui sheria za kazi.

“Wafanyakazi waliofikiwa waliulizwa kama wanazijua sheria zinazohusiana na masuala ya kazi, na kama wanazijua wataje sheria tatu. Wengi walishindwa, ni asilimia 5 tu ndio waliweza kutaja,” amesema.

Ameeleza, wafanyakazi wengi wanashindwa kutofautisha kati ya haki na wajibu, huku wengine walipoulizwa kuwa haki zao ni zipi, walitaja kuwahi kazini badala ya wajibu.

“Tatizo hili limechangia kwa kiasi kikubwa ukiukwaji wa haki zao, kwasababu wenyewe hawazijui vizuri, mkoa kama Mtwara ulionekana kuwa na uelewa mdogo zaidi kuliko mikoa yote,” amesema.

Hata hivyo, ripoti hiyo imeeleza bado kuna changamoto kubwa kutokana na kiwango cha ajira kwa watoto kuendelea kuwepo hasa kwenye maeneo ya uwekezaji wa kampuni za biashara.

Na kwamba, Geita na Shinyanga ndio mikoa inayoongoza kwa ajira za watoto kwenye maeneo ya migodi. Katika maeneo mengine, wanawaajiriwa kwa ajili ya kuchunga mifugo.

error: Content is protected !!