PENALTI ya dakika 26, kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Ujerumani ‘Bundesliga’ dhidi ya SC Freiburg uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2, ilitosha kwa Robert Lewandowski kuifikia rekodi ya mkongwe, Gerd Muller ya kupachika mabao 40 katika msimu mmoja. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).
Rekodi ya Gerd Muller ya kupachika mabao 40 ndani ya msimu mmoja kwenye Ligi Kuu ya Ujerumani, ilidumu kwa miaka 49, mara baada ya kufanya hivyo kwenye msimu wa 1971/1972.
Baada ya kufunga bao hilo, Lewandowski alifunua jezi na kuonesha fulana yake ya ndani iliyokuwa na picha ya mkongwe huyo na kuonesha heshima yake kwake kutokana na sasa kusumbuliwa na maradhi ambayo yamemuweka kitandani.

Mkongwe huyo aliweka rekodi hiyo ya mabao 40 kwenye msimu wa mwaka 1972 akiwa na kikosi cha klabu ya Bayern Munichen ambayo alifanikiwa kushinda nayo mataji matatu ya Bundesliga.
Kwa sasa Muller ana umri wa miaka 76, ambapo katika kipindi cha miaka sita sasa yupo kitandani akisumbuliwa na maradhi.
Lewandowski amefikia rekodi hiyo akiwa na umri wa miaka 32, huku akiwa na nafasi ya kuweka rekodi yake mpya kutokana kusalia na michezo mitano ya ligi hiyo.
Leave a comment