January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lembeli, Nyerere, Wenje kubomoa ngome za CCM

Spread the love

KIKOSI kazi cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikiongozwa na James Lembeli anayegombea Jimbo la Kahama Mjini, Vicent Nyerere wa Jimbo la Musoma Mjini na Wenje wa Nyamagana wote kutoka Chadema kinatarajiwa kuanza kampeni katika majimbo ya mkoa wa Geita. Anaandika Moses Mseti, Mwanza … (endelea).

Wagombea hao wanafanya kampeni hizo katika majimbo yote ya mkoa wa Geita wakiwanadi wagombea wa Ubunge na Udiwani wanaoungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Katika kuhakikisha kikosi hicho kinafika katika majimbo yote kwa muda mfupi, watatumia Chopa ya chama hicho iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mabowe.

Akizungumza na Mwanahalisi Online kabla ya kuondoka kuelekea Geita, Wenje amesema wamekabidhiwa jukumu la kuisimamia helikopta hiyo sambamba na kuwanadi wagombea wote wa Kanda ya Ziwa, na sasa wanahamishia mashambulizi katika majimbo ya mkoa wa Geita.

Wenje amesema tangu helkopta hiyo ipokelewe mwishoni mwa wiki iliyopita, wamefanikiwa kufanya mikutano zaidi ya 20 katika majimbo ya Nyamagana na Misungwi na kuongeza kuwa ujio wa chopa hiyo imebadilisha upepo majimboni na kusababisha maelfu ya wananchi kuhudhuria tofauti na ilivyokuwa awali.

“Kabla ya chopa hii kuja Mwanza, ilianzia mkoani Mara ambapo tulifanya tuliitumia katika kufanya mikutano katika jimbo moja la Musoma Mjini, tukaruka hadi hapa kwetu na kufanya mikutano jimbo la Buchosa, Sengerema, Nyamagana na Misungwi, leo (jana) tunavamia mkoa wa Geita, baadaye tutaangalia mkoa mwingine,” amesema.

“Tunatarajia hadi kufikia Oktoba 24, mwaka huu, tutakuwa tumemaliza majimbo yote, lengo letu ni kuhakikisha wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) hawashindi ili Ukawa twende Ikulu kuwakomboa Watanzania baada ya kuteseka zaidi ya miaka 54 tangu uhuru,” amesema Wenje.

Hata hivyo Wenje akiwa katika mikutano mbalimbali jimboni Nyamagana, aliwaomba wananchi kuitosa CCM kwa kuwa imeshindwa kuwaletea maendeleo badala yake watu wachache wamejimilikisha nchi kwa kutumia rasilimali za taifa bila kujali watu wengine wanateseka.

Wenje amesema anashangazwa na kitendo cha wagombea wa CCM kuanzia ngazi ya urais hadi udiwani kutembea na wasanii zaidi ya 50 katika kampeni zao ambapo alidai kuwa tangu kampeni zianze wasanii hao wamepewa Sh. 5 bilioni.

Amesema fedha hizo ambazo ni kodi ya wananchi zilipaswa kutumika kumaliza tatizo la ukosefu wa madawati kitendo ambacho kinasababisha sekta ya elimu kudorora. “Hapa jiji la Mwanza kwa miaka mitatu tunapata hati chafu. Chanzo ni Meya, Stanslaus Mabula ambaye leo anajitokeza kugombea ubunge, haya ni maajabu.

“Kwa miaka mitano yangu nimejitahidi kuboresha sekta ya elimu, miundombinu, maji, umeme na mambo mengine, nawaomba ifikapo Oktoba 25, mwaka msikosee kunichagua tena, kwani Ukawa tuna uhakika kwa kwenda Ikulu,” amesema.

error: Content is protected !!