January 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lembeli aanika yaliyofichwa Operesheni Tokomeza

Spread the love

MGOMBEA ubunge wa jimbo la Kahama, James Lembeli kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ameishambulia serikali ya CCM na kueleza kwamba serikali hiyo haiwezi kuwapatia wananchi maendeleo kutokana na kuwa na mfumo mbovu wa kiutawala. Anaandika Dany Tibason, Bukombe … (endelea).

Mbali na hilo Lembeli alisema serikali ya CCM ndiyo serikali pekee yenye mfumo kandamizi, viongozi wake ni walaghai wakubwa na imekuwa na mfumo mchafu wa kulindana mafisadi kwa mafisadi huku wananchi wa kawaida wakiendelea kutaabika.

Lembeli ambaye awali alikuwa mbunge wa CCM jimbo la Kahama na baadaye kutimkia Chadema, alitoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa kampeni za Chadema zilizofanyika katika viwanja vya Freeman Mbowe ambapo uwanja huo ulijengwa na mbunge anayemaliza muda wake na kutetea jimbo hilo Prof Kulikoyela Kahigi.

Kiongozi huyo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni hizo alitonesha vidonda vya wafugaji wa jimbo hilo kwa kueleza kwamba serikali imekalia ripoti ya uchunguzi wa Tume iliyoundwa na bunge kwa ajili ya Operesheni tokomeza.

Alisema sababu kubwa ya serikali kushindwa kuweka hadharani taarifa hiyo ambayo Lembeli alikuwa mwenyekiti ni kutokana na vitendo vingi vilivyofanywa vilikuwa vikihusisha vigogo wa serikali na ndiyo maana kuna hali ya kulindana licha ya kuwa wapo watu ambao wamepata vilema na wengine kupoteza maisha.

Alisema katika taarifa hiyo kuna mambo mengi ya kutisha ambayo yalifanywa na watumishi wa serikali ikiwa ni pamoja na kudhalilisha utu wa mtu, mauaji pamoja na uharibifu wa mali za wananchi hususan wafugaji.

“Ndugu zangu wana Bukombe kuna msemo usemao siri ya mtungi aijuaye kata, sasa mtungi ni CCM na kata ni mimi (Lembeli) mimi nimetoka CCM baada ya kuona kwamba hakuna chama dharimu, kandamizaji, kinachotumia migogo ya wanyonge masikini kujinufaisha.

“Sijaona chama chenye viongozi ambao wanalinda ufisadi wa kutisha, wizi wa kutisha pamoja na watu ambao hata upeo wa kufikiri umekwisha bali wamekuwa watu wa kupokea vitisho vya hali ya juu na hatima yake wanatugeuza kuwa wapumbavu na malofa,” amesema Lembeli.

Akizungumzia ahadi za mgombea urais kupitia CCM, Dk. John Magufuli, Lembeli amesema kwamba mgombea huyo kwa sasa amekuwa akiwalaghai wasukuma kwa madai kwamba atawapatia maendeleo pale tu atakapochaguliwa.

Amesema kauli hiyo ni ya uongo na unafiki kamwe Dk. Magufuli awezi hata kuwatetea wasukuma wenzake.

“Nawapa mifano miwili tu wakati Dk. Magufuli akiwa waziri wa mafugo aliwasaidia nini wafugaji wakati mifugo ikiteketea na kukosekana kwa soko.

“Mbali na hilo alipochaguliwa kuwa waziri wa mifugo na uvuvi ni nani ambaye alikuwa akichoma kokolo za wavuvi kwa madai hazifahi, alikuwa wapi kushika nyavu hizo zikiwa madukani na kuzipiga marufuku wakati huo huo aliendelea kuchoma nyavu hizo, hapo kweli ana nia ya kuwakomboa watanzania hususani wakulima na wafugaji,” alihoji Lembeli.

error: Content is protected !!