August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Lema amemkosea nani?

Godbless Lema, Mbunge wa Arusha Mjini, akirudishwa rumande baada ya kukosa dhamana

Spread the love

GODBLESS Lema, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), bado anasota kwenye gereza kuu la Kisongo, mkoani Arusha, anaandika Yusuph Katimba.

Lema yuko gerezani kufuatia upande wa mashitaka kupinga kuachiwa kwa dhamana katika kesi ya uchochezi inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, mkoani Arusha.

Upande wa utetezi unaendelea kupigania haki ya Lema ya kuachiwa kwa dhamana katika Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha. Maombi ya rufaa yamepangwa kusilikilizwa Feburuari mwakani.

Kutokana na hali hiyo, wengi wametoa maoni tofauti juu ya kilichompata Lema. Tundu Lissu, wakili wa mahakama kuu, mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) na mwanasheria mkuu wa chama hicho, anasema ifuatavyo:

Kwenye kesi yangu ya dikteta uchwara One (ya kwanza), Hakimu Mkazi alitoa dhamana na mara mawakili wa Serikali wakatoa taarifa ya mdomo kwamba wanatarajia kukata rufaa.

Wakamuomba Hakimu kutoendelea na utaratibu wa kutoa dhamana kwa sababu ya nia yao hiyo. Hakimu Mkazi aliwakatalia kwa hoja kwamba asipotoa dhamana atakuwa ametengua uamuzi wake mwenyewe wa kutoa dhamana alioutoa awali.

Wanasheria wanaita functus officio (hali ya kutokuwa na mamlaka zaidi). Alishamaliza kazi yake kuhusu dhamana na asingeweza kuirudia tena.

Mazingira ya kesi ya Lema yalikuwa hayo hayo, lakini Hakimu Mkazi alitoa maamuzi tofauti kabisa. Tunapenda sana kusema mahakimu na majaji wetu wanaangalia sheria tu.

Ukweli ni kwamba kuna mambo mengi sana yanayoingia katika hukumu, hasa kesi za kisiasa kama hii, ni zaidi ya sheria. Mtazamo wa kisiasa na wa falsafa ya kisheria wa hakimu au Jaji husika ni kitu muhimu sana katika kuelewa maamuzi wanayoyatoa mahakamani.

Mashinikizo ya wanasiasa au nguvu ya rushwa au fedha inaingia katika maamuzi ya kimahakama. Kwenye kesi kubwa kama hii ni wazi mashinikizo haya yatakuwa yamechukua nafasi kubwa katika maamuzi ya leo ya Jaji.

Kwa mfano, ni Jaji ndiye aliyewaelekeza mawakili wa Lema kukata rufaa. Baada ya kufanya hivyo na kuwekewa pingamizi na mawakili wa serikali, ni Jaji huyo huyo aliyeikataa rufaa kwa hoja kwamba walitakiwa kutoa notisi kwanza.

Jaji mwingine asingekubaliana na pingamizi hilo kwa hoja kwamba ni yeye Jaji ndiye aliyetoa maelekezo rufaa ikatwe kwenye hatua ya awali.

Lakini ni Jaji gani aliyeamua rufaa ya leo? Mh. Fatuma Massengi? Angalieni nilichokisema bungeni juu ya majaji wetu mwaka 2013 na baadaye kwenye mkutano wa mwaka wa chama cha wanasheria Tanganyika (TLS), jijini Arusha.

Ni mmojawapo wa majaji walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete ambao, kwa maoni yangu, kwa wakati wote hawezi kutoa maamuzi kama Jaji.

Lakini Albert Msando ana mtazamo tofauti na ule wa Lissu. Anasema makosa yote aliyoshtakiwa Lema yanaweza kudhaminika na kwamba Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, ilitoa uamuzi kutupa hoja za upande wa mashtaka kwamba Lema asipewe dhamana kwa sababu ambazo walizitoa.

Lakini baada ya uamuzi huo, upande wa mashtaka ukatoa notisi (taarifa) kuwa hawajaridhika na uamuzi wa kutupilia mbali mapingamizi yao ya dhamana.

Hivyo basi, baada ya kutoa taarifa hiyo hakimu akatoa uamuzi kwamba hawezi kumpa dhamana Lema kwa sababu tayari kuna taarifa ya rufaa.

Baada ya uamuzi wa kutokumpa Lema dhamana kwa sababu kuna notisi ya rufaa upande wa mawakili wa Lema, kwanza waliomba marejeo ya uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mfawidhi kutompa dhamana kwa sababu kuna notisi ya rufaa. Walishindwa.

Pili, waliambiwa walitakiwa wakate rufaa na sio kuomba marejeo. Wakakata rufaa. Upande wa mashtaka ukaweka pingamizi kwamba hawakuwa wametoa notisi ya kukata rufaa kwa mujibu wa sheria! Hivyo rufaa ikatupwa.

Kwa hiyo wanachofanya upande wa mashtaka ni kucheza na makosa ya kiufundi (technicalities). Wanajua kabisa wanamkomoa Lema kwa kutumia mbinu za makosa ya kiufundi.

Wanajua kabisa kwamba Mahakama Kuu inaenda likizo mpaka mwakani. Na mahakama inaendeshwa na ratiba. Huwezi ukasikiliza kesi ya Lema pekee wakati washtakiwa wote wana haki sawa.

Hata hivyo, mahakama imejitahidi angalau kwenda kwa kasi ingawa mwishoni makosa ya kiufundi yametumika kugongesha mwamba.

Kwa upande wa Zitto Kabwe, mbunge wa Kigoma Mjini anasema:

Leo Ijumaa, tarehe 2 Desemba 2016 nimepata fursa ya kumsalimu Lema, katika gereza kuu la Arusha. Nimemtembelea kama mbunge mwenzangu na kumhakikishia solidarity (mshikamano) katika harakati za kutafuta na kulinda haki.

Lema ana ari kubwa ya mapambano. Anasikitishwa sana na ukiukwaji mkubwa wa haki na mahakama kuonekana kuendeshwa na serikali. Yeye ameona ni bora akae ndani mpaka hapo dola itakapopenda kumpa dhamana. Kosa lake lina dhamana na hakimu alimpa dhamana.

Ameomba tutazame mahabusu wengi wanaokaa ndani miaka mingi bila kesi zao kuendelea. Tuwatetee.
Amemshukuru Mungu kwa kumpa mke jasiri anayempa moyo na ndio ngome yake kwa sasa.

Nimemwomba Lema aone kuwa hii struggle (mapambano) sio yake peke yake, bali anawakilisha watu wengi wanaotaka haki kutendeka katika uendeshaji wa nchi. Siku zote haki hushinda.

Akisoma uamuzi mdogo wa Jaji Fatuma Masengi, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Angero Rumisha alisema, Mahakama imeifuta Rufaa hiyo, kutokana na wakata rufaa kuikata nje ya muda.

Rumisha amesema waomba rufaa walitakiwa kuonesha kusudio la kukata rufaa ndani ya siku kumi tangu uamuzi wa maombi ya marejeo kutupwa na Mahakama Kuu, yaliokuwa mbele ya Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Sekela Moshi 11 Novemba.

“Hivyo Mwomba rufaa hii Lema kupitia Mawakili wake alitakiwa kuonyesha kusudio au kutoa notisi kuonesha Mahakama sababu ya kukata rufaa na 21 Novemba walipaswa kukata rufaa lakini wao wamekata Novemba 22 nje ya muda wa kukata rufaa,” alisema.

Amesema kutokana na hali hiyo, Mahakama imekubaliana na upande wa pingamizi lililowekwa na upande wa serikali kupitia wakili Paul Kadushi akishirikiana na Martenus Marandu kuwa rufaa hiyo haikufuata misingi ya kisheria, kwa sababu hakuna kusudio la kuikata na kuomba Mahakama iitupilie mbali.

Rumisha alisema baada ya pingamizi hilo kutolewa na upande wa Lema kujibu kwa kuomba mahakama ilitupilie mbali pingamizi lililopo mbele yake, kwa kuwa rufaa yao ipo ndani ya muda na imewasilishwa kwa hati ya dharura, Mahakama imekubaliana na hoja kuwa rufaa hiyo imeletwa mahakamani nje ya muda unaotakiwa.

Aidha, Rumisha alisema mbali na nje ya muda, wakata rufaa hawakuzingatia sheria inavyotaka kuwa ukikata rufaa lazima uanze na kutoa taarifa ya kusudio la kukata rufaa.

Mke wa Lema Neema Lema anasema: “Nashukuru watu wote waliojitokeza katika kesi hii, licha ya usumbufu mwingi waliokutana nao. Nilipoongea na Lema, tumeona katika kesi hii kuna mtu anataka mahakama ifuate maagizo yake. Tumeona tuache maagizo ya mtu huyo yafuatwe.

error: Content is protected !!