Saturday , 22 June 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Lema achafua Bunge, wapinzani watoka nje 
Habari za SiasaTangulizi

Lema achafua Bunge, wapinzani watoka nje 

Spread the love

BAADHI ya wabunge wa upinzani, wametoka nje ya Bunge, kupinga hatua ya Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, kumshitaki kwenye Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge, mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema (Chadema). Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Dk. Tulia ameagiza Lema kuitwa na kuhojiwa na kamati hiyo, mara moja kufuatia kauli yake kuwa, Bunge ni dhaifu.

Naibu Spika amesema, “kauli ya Lema, imelenga kulidhalilisha Bunge.”

Lema alitoa kauli hiyo wakati akichangia taarifa ya Kamati ya Maadili, iliyokuwa ikisikiliza shauri lililowasilishwa kwake na Spika wa Bunge, Job Ndugai dhidi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Asaad na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema).

Akichangia ripoti hiyo, leo tarehe 2 Aprili 2019, bungeni mjini Dodoma, Lema alisema, “…mnamjadili Mheshimiwa Mdee kwa kusema Bunge ni dhaifu. Mimi kama mbunge, naweza kuthibitisha pasipo na shaka, kuwa Bunge, ni dhaifu.”

Ripoti ya Kamati ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge, iliwasilishwa bungeni na mwenyekiti wake, Emmanuel Mwakasaka.

Ripoti ya Kamati ya Mwakasaka, ilileta ndani ya Bunge mapendekezo ya adhabu dhidi ya CAG na Mdee.

Spika Ndugai aliagiza CAG ahojiwe kwa madai ya kulidhalilisha Bunge. Kilichomponza mtendaji huyo, ni kauli yake aliyoitoa  katika mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya Redio ya Umoja wa Mataifa nchini Marekani mwaka jana. nchini Marekani ambako alisema, “Bunge ni dhaifu.”

Mara baada ya kauli ya Lemay a kuita, “Bunge dhaifu,”  na huku akiwa bado anaendelea kuchangia, Dk. Tulia, haraka aliingia na  kusema, “kwa mameno hayo uliyosema, na wewe naagiza upelekwe kwenye Kamati ya Madili.”

Aliongeza, “naomba ukae na hamna kuchangia tena. Haiwezekani kabisa, tumekaa hapa tunajadili adhabu kuhusu maneno hayo (ya CAG), nawe unasema, utaweza kuthibitisha kuwa Bunge ni dhaifu.

“… na wewe utaelekea kwenye kamati hiyo ukathibitishe vizuri kule, kwa hiyo kamati na huyu naye analetwa kwenu kwa utaratibu wa kawaida.”

Ndani ya Bunge, Lema alitetea kauli ya Mdee kuwa Bunge linaloongozwa na Ndugai na Tulia, ni dhaifu.

Kufuatia uamuzi huo wa Dk. Tulia, wabunge wote wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na baadhi ya wabunge kutoka Chama cha Wananchi (CUF), waliamua kutoka nje ili kuonesha jisi wasivyofurahishwa na kitendo hicho.

Bunge lilipitisha kwa wingi wa kura, mapendekezo ya Kamati ya Maadili yaliyotaka Mdee asimamishwe kuhudhuria mikutano miwili ya Bunge – mkutano huu wa 15 na mkutano ujao wa Septemba.

Wakati Bunge linabariki “kifungo kwa Mdee,” mwanasiasa huyo alikuwa ndani ya Bunge na alipata nafasi ya kujieleza.

Mara baada ya Mdee kujieleza, Dk. Tulia alilihoji Bunge juu ya mapendekezo ya Kamati ya Maadili yaliyotaka mbunge huyo asimamishwe mikutano miwili ya Bunge, ambapo  wabunge wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliridhia adhabu hiyo.

“Kwa mipaka iliyoweka na ibara ya 30, ni dhahiri kuwa Mdee alitumia uhuru wake kwa namna ambayo imeathiri haki na heshima ya bunge. Hivyo kuathiri masilahi ya umma, kwa mantiki hiyo alikiuka masharti ya kikatiba kwa kuingilia mhimili wa bunge,” alieleza Dk. Tulia, mara baada ya Bunge kupitisha azimio hilo.

Hii ni mara ya tatu kwa Mdee kusimamishwa kuhudhuria mikutano wa Bunge. Aprili mwaka 2017, mbunge huyo alisimamishwa kuhudhuria mikutano mitatu ya Bunge.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

Padre anayetuhumiwa mauaji ya Asimwe, asimamishwa

Spread the loveKanisa Katoliki Jimbo la Bukoba limemsimamisha kutoa huduma za kichungaji...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Serikali yaahidi kushirikiana na Prof. Ndakidemi kuhamasisha zao la kahawa

Spread the loveSerikali imeahidi kuungana na Mbunge wa Moshi Vijijini, Profesa Patrick...

BiasharaHabari MchanganyikoHabari za Siasa

IMF yaimwagia Tanzania trilioni 2.4 kukabili mabadiliko ya hali ya hewa

Spread the loveShirika la Kimataifa la Fedha (IMF) jana Alhamisi limesema bodi...

Habari za SiasaKimataifa

Mmoja afariki, 30 wajeruhiwa maandamano Kenya

Spread the loveMtu mmoja ameripotiwa kuuawa na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa...

error: Content is protected !!