November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

LEAD Foundation waibuka kinara ustawishaji miti Afrika

Spread the love

 

SHIRIKA la LEAD Foundation linalojihusisha na utunzaji wa mazingira mkoani Dodoma limetangazwa miongoni mwa mashirika 20, yanayoongoza katika miradi ya ustawishaji miti barani Afrika. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Mashirika hayo yalitangazwa rasmi katika mkutano wa mwaka huu wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) uliofanyika hivi karibuni Jijini Glasgow.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo tarehe 21 Novemba, 2021 na Shirika hilo kwa vyombo vya habari imesema zaidi ya mashirika 3,200 ya Afrika kutoka katika nchi 31 yalituma maombi kupata fedha kwa ajili ya kuendesha miradi mbalimbali ya kutunza mazingira.

Katika awamu ya kwanza mashirika 20 ya Afrika yaliyofanya vizuri zaidi katika miradi ya kustawisha miti yamechaguliwa.

Kwa Tanzania shirika pekee lililochaguliwa katika awamu hii ni LEAD Foundation.

“Kuanzia mwaka 2011, LEAD Foundation imefanya kazi kwa karibu na zaidi ya wakulima 120,000 kukomboa ardhi katika maeneo kame ya Tanzania” ilisema sehemu ya taarifa hiyo

Ilisema kwa pamoja wameweza kustawisha zaidi ya miti milioni tisa ya asili na kukomboa zaidi ya hekta 124,000 za ardhi kwa kutumia njia mbalimbali ikiwemo njia ya Kilimo Msitu ya Kisiki Hai (FMNR) pamoja na njia Uvunaji wa Maji ya Mvua (RWH).

Kwa msaada wa fedha hizo, LEAD Foundation inategemea kuendeleza jitihada zake za kukomboa mazingira katika maeneo kame ambayo yalikuwa bado hayajafikiwa katika mkoa wa Dodoma.

Jiji la Dodoma

Aidha, shirika hilo litawasaidia wakulima na wafugaji kustawisha miti ili kuondokana na athari za ukame, mmomonyoko wa udongo pamoja na kurutubisha ardhi ya mashamba na malisho ya mifugo.

Taarifa hiyo ilibainisha kuwa miaka sita iliyopita, viongozi wa Afrika walitambua kuwa uharibifu mkubwa wa takriban asilimia 65 ya ardhi ya kilimo katika bara hilo ni tishio kwa uchumi na maisha ya mamilioni ya wakulima.

Ilisema waligundua hivyo kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi yanayosababisha uzalishaji mdogo wa mazao, mvua zisizotabirika na vipindi virefu vya ukame vinavyofanya maisha ya mamilioni ya wakulima kuwa magumu na hivyo kusababisha ongezeko kubwa la watu wanaoacha shughuli za kilimo na kukimbilia mijini kutafuta riziki.

“Hii ndio sababu mwaka 2015 nchi za Afrika ziliahidi kukomboa hekta milioni 100 za mazingira na ardhi iliyochakaa kufikia mwaka 2030 kupitia Mpango wa AFR100” ilibainisha taarifa hiyo

Kutokana na hali hiyo maelfu ya mashirika madogo ya kiafrika yameibua miradi na njia mbalimbali za kibunifu za kukomboa mazingira ili kuleta matokeo chanya kwa faida ya Afrika ya kesho.

“Inakadiriwa kuwa wakulima barani Afrika wanamiliki karibu asilimia 70 ya ardhi yote ya Afrika” ilieleza taarifa hiyo.

error: Content is protected !!