Wednesday , 21 February 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Lazaro Nyalandu hakamatiki
Makala & Uchambuzi

Lazaro Nyalandu hakamatiki

Spread the love

KILICHOITWA na watawala, “Operesheni Tokomeza” iliyoishia kujiuzulu kwa waziri mmoja na kufutwa kazi mawaziri watatu wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete, yaweza kuwa funguo ya ukomeshaji wa vitendo vya mauwaji, utekaji na utesaji nchini, anaandika Saed Kubenea.

Ni kwa sababu, operesheni hii itakuwa imemfungulia milango mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu dhidi ya binadamu (ICC), kutinga nchini kusaka wanaoruhusu au kusimamia vitendo hivyo. Operesheni tokomeza, yaweza kuwa mahala sahihi pakuanzia.

Kifungu Na. 8(a) (i-viii) cha mkataba wa ICC kimeoredhesha makosa ya kuuwa raia kwa makusudi, kutesa au kudhalilisha binadamu; kumpa maumivu makubwa hadi kuharibu afya au viungo vyake vya mwili; na uharibifu mkubwa usio wa lazima kwa mali na miundominu.

Makosa mengine, ni pamoja na mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya ubinadamu, utekaji na utesaji.

Yaliyotendeka kwenye “Operesheni tokomeza,” yanaangukia moja kwa moja kwenye mkondo wa makosa yanayoweza kushughulikiwa na ICC.

Haitoshi kusema tayari Emmanuel Nchimbi, aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani, Shamsi Vuai Nahodha (ulinzi na jeshi la kujenga taifa), David Mathayo (mifungo na uvuvi), wamefutwa kazi; na au Balozi Khamis Kagasheki (maliasili na utalii), amejiuzulu.

Mawaziri hawa wamesulubiwa ili kulinda serikali. Wameondolewa kwenye nyazifa zao ili kulinda rais na waziri mkuu. Wameng’atuka baada ya wabunge kumkoromea Mizengo Pinda, wakimtaka achukue hatua dhidi ya mawaziri husika; vinginevyo ang’atuke yeye.

Ndiyo maana baadhi yao, ukimuondoa Balozi Kagasheki, aliyeonyesha ujasiri wa kipekee – kusimama bungeni na kutamka neno “najiuzulu” – hakuna aliyethubutu kusimama na kujisemea.

Ndani ya Bunge, wabunge walimwambia Pinda, waziri mkuu wa Jamhuri, “Fukuza mawaziri wanne, au ondoka mwenyewe.” Hiyo ndiyo amri aliyokuwa ametwisha. Ndiyo agizo alilopewa.

Kwa mujibu wa taratibu za mahakama ya ICC, ili raia akamatwe sharti mwendesha mashitaka mkuu atoe hati ya kukamatwa; hati hizo hutolewa kwa misingi ifuatayo:

Ni kama mwendesha mashitaka mkuu ataombwa na nchi mwanachama, au baraza la usalama la umoja wa mataifa, au na ICC yenyewe baada ya kupata taarifa kutoka vyanzo mbalimbali na kisha kufanya uchunguzi wa awali.

Tayari mahakama ya ICC kupitia mkondo wa aina hiyo, imeburuza mahakamani watuhumiwa 27 kutoka Afrika. Miongoni mwao, ni aliyekuwa rais wa Liberia, Charles Taylor.

Awali mwaka 2000, alishitakiwa katika Mahakama Maalum iliyoundwa kwa makubaliano kati ya serikali ya Sierra Leone na Umoja wa Mataifa. Baadaye mwaka 2006, kesi yake ilihamishiwa ICC, na tayari amehukumiwa kifungo cha miaka 50 gerezani.

Ripoti ya uchunguzi kuhusu “operesheni tokomeza” iliyowasilishwa bungeni na mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, imesheheni madai ambayo yanaruhusu moja kwa moja mwendesha mashitaka wa ICC (Fatou Bensouda) kutinga nchini.

Operesheni tokomeza imedhalilisha binadamu; imetesa na imesababisha watu kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria.

Waliokabidhiwa jukumu la kuendesha operesheni ya kusaka majangili, wameishia kubaka raia na kuwatendea binadamu vitendo vya kinyama.

Ripoti “operesheni tokomeza” imeibua tuhuma lukuki dhidi ya serikali; baadhi ya viongozi wakuu wa vyombo vya dola – jeshi la wananchi (JWTZ), usalama wa taifa (TISS) na jeshi la polisi.

Miongoni mwa tuhuma hizo, ni ukatili dhidi ya binadamu, mateso, vitisho na mauaji. Wapo waliodhalilishwa – wanawake kwa waume – baadhi yao walipewa adhabu wakiwa uchi. Wengine walishikwa sehemu zao za siri. Wakabinywa.

Wengine tayari wamethibitika kupoteza uwezo wa kufanya tendo la ndoa. Huu ni ukatili usiostahili kuvumilika na ambako mwendesha mashtaka wa ICC aweza kuchunguza.

Mahakama ya ICC yaweza kuchunguza juu ya tuhuma za kubariki; au kunyamazia vitendo vya ukatili vilivyofanywa na vyombo vya dola dhidi ya raia; kuchunguza nani hasa aliyetoa agizo la kutendwa vitendo hivyo. Huyo ndiye atakayekuwa mtuhumiwa mkuu wa kilichotendeka.

Ripoti haikutaja uhusika wa moja kwa moja wa viongozi wakuu wa vyombo vya dola. Hata hivyo, kwa jinsi “operesheni tokomeza,” ilivyoendeshwa na kugeuka haraka kutoka operesheni pambana na majangili, hadi kuwa uhalifu dhidi ya binadamu, wengi wanaweza kushitakiwa. Sababu ni tatu.

Kwanza, “operesheni tokomeza” iliyozinduliwa tarehe 4 Oktoba 2013, ilikuwa ya kijeshi. Iliekelezwa na kuendeshwa kwa amri ya jeshi Namba 0001/13 ya tarehe 28 Septemba 2013.

Tangazo la operesheni lilisainiwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi.
Hakuna mashaka hatua ya serikali kuingiza jeshi la kivita kwenye operesheni tokomeza, ni kinyume na katiba na kinyume na matakwa ya sheria za kimataifa.

Ili kuingiza jeshi kwenye shughuli za kiraia, sharti kuwapo tangazo la “hali ya hatari.” Tangazo hilo ni lazima lisainiwe na Rais wa Jamhuri; katika kipindi cha ndani ya wiki mbili, suala hilo lifikishwe bungeni.

Aidha, kuamuru jeshi kuingia kwenye operesheni ya aina hii, hufanyika pale nchi inapokuwa vitani au inaelekea kuvamiwa na nchi nyingine.

Hata katika mazingira hayo, masharti ya kupatikana kibali cha bunge, yanabaki palepale.
Sasa swali la kujiuliza: Nani aliyeamuru kuingizwa jeshi kupambana na raia wasiokuwa na silaha? Nani aliyetoa amri hiyo?

Bunge linasema, kulikuwa na tangazo Namba 0001/13 ya tarehe 28 Septemba 2013; lilisainiwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi. Je, alipata wapi mamlaka hayo? Alitumwa na nani? Mahakama ya ICC yaweza kumhoji na kujua ukweli.

Yapo madai kuwa mmoja wa mawaziri (jina tunalo) aliingilia utekelezaji wa operesheni kwa kuagiza wahusika wasiwaguse viongozi wa kisiasa wa ngazi zote katika kutekeleza kazi hiyo. Huko ni ukiukwaji wa sheria, upendeleo na nia mbaya dhidi ya wengine.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Lowassa: Mwanasiasa aliyetikisa CCM, Chadema

Spread the loveWAZIRI Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Edward Lowassa (70) amefariki Dunia...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Uongozi wa Samia kuendelea hadi 2030

Spread the loveKWETU sisi tuliowahi kusoma sekondari, iwe O levo au A...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Bado askari wastaafu wanaonewa

Spread the loveRAIS wangu Samia Suluhu Hassan tunaendelea kumshukuru Mungu kwamba wote...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Tunastawisha ufisadi na kuchukia matunda yake

Spread the loveBUNGE la Jamhuri linaloendelea mjini Dodoma, kwa wiki nzima limetawaliwa...

error: Content is protected !!