January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

LAPF yatoa msaada wa 2.8 mil Makole

Spread the love

UONGOZI wa kituo cha afya Makole, mjini Dodoma umepokea msaada wa vifaa vikiwemo vya usafi vyenye thamani ya Sh. 2.8 milioni kwa ajili kuhudumia wagonjwa hospitalini hapo pamoja na kutunza mazingira. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Vifaa hivyo vimetolewa jana na Mfuko wa Pensheni wa LAPF ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 54 ya Uhuru ambapo walianza kwa kufanya usafi katika maeneo yanayozunguka hospitali hiyo pamoja na wodini pamoja na maeneo ya ofisini zao.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa LAPF, Eliud Sanga amesema msaada huo umelenga kuboresha huduma kwa wagonjwa waliolazwa kituoni hapo, wengi wao wakiwa wajawazito na watoto, na kwamba inaunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha huduma za afya nchini.

Baadhi ya vifaa vilivyotolewa katika maadhimisho hayo ni pamoja na mashuka 50, vyandarua 50, vifaa vya kuwekea uchafu, katoni za madawa ya usafi pamoja na vifaa mbalimbali vya kufanyia usafi yakiwemo majembe, reki na makwanja ambayo yalitumika pia kufanyia usafi.

“Tunaunga mkono agizo la Rais Dk. John Pombe Magufuli la kufanya usafi katika kuadhimisha miaka 54 ya Uhuru hivyo watumishi wa LAPF tumeshiriki kufanya usafi katika maeneo yote ya ndani na njeya kituo cha Afya cha Makole,” amesema.

Amesema LAPF inaaamini kuwa misaada hiyo itasaidia wanachama wake pamoja na watanzania kwa ujumla ambao wamekuwa wakikitumia kituo hicho cha afya kupata huduma.

Akipokea msaada huo, Mkuu wa wilaya ya Dodoma, Jasmine Tiisekwa amesema maadhimisho ya miaka 54 ya Uhuru yataingia kwenye kumbukumbu za watanzania na kuwa historia kutokana na aina ya uadhimishaji uliofanyika kwa watu kushiriki kufanya usafi bila kujali vyeo vyao.

Amesema Rais Magufuli ametufungulia njia na kutukumbusha kuwa usafi ni wajibu katika kuepukana na magonjwa ya milipuko na ndio maana kila mtu amekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza agizo hilo.

“Tumuunge mkono Rais wetu kwa kufanya usafi wakati wote kwani tumeshuhudia katika kipindi cha siku tatu mfululizo hadi leo hakuna mgonjwa kipindupindu aliyepokelewa, matokeo ni mazuri na usafi ni endelevu,” amesema Mkuu wa wilaya.

Katika hatua nyingine, Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Dodoma, Clemense Mkusa alikiri kuwepo kwa changamoto ya vifaa vya uzoaji taka katika maeneo mbalimbali yaliyofanyika usafi.

Amesema halmashauri imejipanga kupitia vikundi vyake vya usafi vilivyopo katika kata vimekuwa vikisomba taka hizo na kupelekea katika maeneo ambayo taka hizo zitaondolewa na magari ya manispaa na kupelekwa dampo.

Mbali na usafi uliofanyika katika kituo cha afya cha makole, pia wananchi pamoja na taasisi walijitokeza na kufanya usafi katika maeneo mbalimbali likiwemo soko la Chang’ombe.

error: Content is protected !!