SERIKALI ya Tanzania, imesema mpaka kufika Juni 2021, jumla ya laini za simu milioni 53 zimesajiliwa, watu wanaotumia mtandao wa intaneti milion 29 na miamala ya simu milioni 32 hufanywa kila mwezi. Anaripoti Yusuf Katimba, Dodoma…(endelea).
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano, tarehe 16 Juni 2021, na Dk. Faustine Ndugulile, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (Tehama), kwenye simina ya wizara hiyo na wahariri.
“Kasi ya maendeleo ya teknolojia ni kubwa, serikali imejipanga kwenda sambamba na mabadiliko hayo,” amesema.
Amesema, wizara hiyo ni mpya na ina miezi sita tangu ianzishwe tarehe 5 Desemba 2020.
Dk. Ndugulile amesema, serikali imeanzisha wizara hiyo kutokana na kasi ya mapinduzi ya nne ya viwanda ambapo, teknolojia ndio msingi mkuu wa dunia.
“Sasa hivi ni mapinduzi ya nne ya viwanda, mashine zitakuwa zikifanya kila kitu, binadamu tutakuwa hatuna kazi.”

“Sisi kama serikali, lazima tujiandae kwenda sambamba na hilo, ndio maana wizara hii ikaanzishwa,” amesema Dk. Ndugulile.
Amesisitiza, dunia imewekeza kwenye teknolojia na kwamba, katika mlipuko wa ugonjwa wa corona, kampuni zilizotumia teknolojia ndio zimepata faida kubwa.
Amewaambia wanahabari kuwa, kasi ya teknolojia imesukuma vijana kuingiza biashara kutoka nje kutumia twitter, instagram, Facebook na mitandao mingine kufanya biashara.
Amesema, wizara hiyo ndio inayosimamia mawasiliano ya serikali kwenye taasisi zote na matumizi ya mawasiliano ya wananchi kila siku.
“Tunataka serikali iende kiganjani mwa mwananchi. Tunataka mtu akipiga X-Ray Kyela anaipeleka Dar es Salaam inasafishwa na kisha inarejeshwa Kyela ndani ya nusu saa.
“Lakini unapotumia simu, televisheni, benki, mawasiliano ya ndege na mawasiliano yote, wizara hii inahusika,” ameeleza Dk. Ndugulile.
Akizungumzia mkongo wa taifa, amesema mpaka sasa serikali imetandika kilometa za mraba 8,319 lengo likiwa ni kufikisha kilometa za mraba 15,000 mpaka kufika mwaka 2025 ambapo bilioni 677 zimetumika.
“Tunataka Tanzania kuwa kituo kikubwa cha mawasiliano, kazi inaendelea kuunganisha Tanzania na Msumbiji, Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
“Asilimia 94 ya mawasiliano (2G) yamefika nchi nzima (kitochi), asilimia 66 ya ardhi ya Tanzania wanatapa internet, ” amesema.
Waziri huyo amesema, serikali inaandaa Sheria ya Kulinda Data kutokana na kuingiliwa kwa mawasiliano na data kwa watu wasiohusika.
Pia, amesema, serikali imefanya mapitio ya ada za usajili lakini pia tozo za adhabu.
Leave a comment