February 27, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Laana ya Makonda yagonga mwamba, makontena yauzwa

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango (kulia), picha ndogo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alipokuwa anapokea makontena aliyoagiza

Spread the love

BAADHI ya samani zilizokuwemo kwenye makontena yaliyoingizwa nchini na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na kukwama bandarini kutokana na kudaiwa kodi ya Sh. 1.2 bilioni, zimeanza kupata wateja. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Makontena hayo yameanza kupata wateja leo tarehe 1 Septemba 2018 huku mengine yakiendelea kusubiri wateja katika manta utakaotangazwa siku zijazo.

Baada ya mnada wa kwanza kufanyika Jumamosi iliyopita, Makonda alinukuliwa kulalamikia hatua ya kupigwa bei makontena hayo na kusema kuwa, atakayeyanunua atapata laana.

Kauli hiyo ilijibiwa vikali na Dk. Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwamba, hakuna laana yoyote kwa atakayenunua makontena hayo.

Kwenye mnada huo Scholastika Kevela, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart&Co. Ltd iliyopewa jukumu la kuuza makontena 20 ya Makonda na TRA ameeleza kuwa, tayari baadhi ya wafanyabiashara ‘wamefika bei’ kwenye mnada huo.

Kevela ameeleza kuwa, aina 10 za samani zilizokuwemo katika makontena hayo, zimefanikiwa kuuzwa leo katika mnada uliofanyika bandarini jijini Dar es Salaam na kwamba nyingine zitaingizwa kwenye mnada siku zijazo.

Hata hivyo, Kevela hakueleza idadi ya makontena yaliyopata wateja na bei iliyonunuliwa na kuahidi kwamba, akimaliza kufanya majumuisho ya makontena yaliyonunuliwa ataja idadi ya makontena hayo yaliyonunuliwa.

“Mengi yamefunguliwa, wako walio nunua na mengine tunaendelea kuuza, huu mnada si wa mwisho tutaendelea Jumamosi ijayo ili hadi yaishe. Kutokufikia bei haimaanishi kwamba ndio mwisho wa mnada, tutaendelea kuuza hadi kufikia bei iliyopangwa na TRA,” amesema na kuongeza.

“Hakuna mtu aliyepangwa kuja kuharibu mnada. Wateja ni wengi na waliohitaji ni wengi, baadaye nitafanya majumuisho,” amesema.”

Mnada huo ulihusisha vifaa vya kilimo magari pamoja na baadhi ya makontena ya Makonda.

error: Content is protected !!