August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Laana UDOM

Spread the love

LAANA zimeanza kumiminwa kwa uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDSM) hususan walisosababisha kusimamishwa masomo kwa wanafunzi 7802, anaandika Dany Tibason.

Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udomasa) imetoa tamko la kulaani kitendo cha cha wanafunzi hao wa programu maalumu ya ualimu wa msingi na sekondari, walio rudishwa nyumbani bila kupewa muda wa kutosha kujiandaa kwa kuzingatia umri wao na mazingira waliyokuwa wanaishi.

Tamko hilo limetolewa leo na Lameck Thomas, katibu wa jumuiya hiyo na kwamba, lawama zimekuwa zikitupwa kwa walimu kutokana na taarifa hizo kutolewa na upande mmoja ambao ni menejimenti ya chuo kwenda serikalini bila kuwepo na taarifa yoyote kutoka kwa walimu kupitia jumuiya yao.

“Kama jumuiya tumeona sio busara kukaa kimya bila kuelezea suala hili kwa usahihi wake kwani ni kuifanya jamii kuamini katika maelezo yaliyo wasilishwa serikalini na upande wa menejimenti ya chuo…, siyo kweli kuwa waalimu tuligoma kufundisha program hii kama inavyoelezwa sehemu mbalimbali,” amesema Thomasi.

Amesema kuwa, tatizo kubwa ni kutoelewana kati ya walimu na menejimenti ya chuo kutokana na mazingira mabovu ya uendeshaji wa program hiyo chuoni hapo.

“Matatizo haya yamelalamikiwa sana na walimu tangu kuanzishwa kwa program hii na kumekuwa hakuna dalili yoyote ya ufumbuzi huku wakiendelea kufundisha kwa uzalendo mkubwa” amesema.

Amesema kuwa, jumuiya ya wanataluma inapata hisia kuwa wizara imeamua kwa makusudi kushirikiana na uongozi wa UDOM kupotosha uhalisia wa jambo hilo kwani hakuna hata wakati mmoja ambapo wamefanya mawasilianao na walimu kupata taarifa kutoka upande wao.

“Katika kutafuta ufumbuzi wakati wa mgogoro, serikali kupitia Naibu Waziri wa Elimu ilifanya kikao na menejimenti ya chuo kwa kushirikiana na viongozi wa Udomasa Mei 19 chuoni hapo.

“Katika kikao hicho, wajumbe walikubaliana kwa pamoja kuundwa kwa kamati ndogo ya kufuatilia suala hili ikijumuisha wajumbe mchanganyiko toka menejimenti ya chuo na Udomasa ikiongozwa na mwenyekiti atakaye toka nje ya chuo ili kuifanya iwe huru zaidi,” amesema.

Ameongeza kuwa, chakushangaza zaidi kamati hiyo haikuwa huru kutokana na menejimenti ya UDOM kutupilia mbali mapendekezo ya jumuiya ya wanataaluma hasa katika majina ya wajumbe waliochaguliwa kuingia kwenye kamati hiyo.

Amesema kuwa, kamati hiyo ambayo haikushirikisha wajumbe walioteuliwa na wahadhiri ilitakiwa kumaliza muda wake tarehe 30 Mei na mpaka sasa jumuiya ya wanataaluma haina taarifa yoyote juu ya ufanyaji kazi wa kamati hiyo.

“Kama jumuiya pia tunasikitishwa na upotoshwaji makusudi wa taarifa unaofanywa na watu mbalimbali kwa kuwasukumia walimu lawama moja kwa moja bila kuwasiliana na walimu hata mara moja,” amesema.

Amesema kuwa, alichosema waziri tarehe 30 Mei ni taarifa ya upande mmoja ambayo haitasaidia katika utatuzi wa kudumu wa suala hilo kutokana na ukweli kuwa, walimu nao wana mambo mengi ya kuzungumza juu ya mgogoro huo ikiwemo madai yao.

Amesema kuwa, jumuiya hiyo haijawahi kuulizwa lolote juu ya uhaba wa walimu pamoja na kuwepo kwa taarifa za tatizo hilo katika chuo hicho.

“Mfano, mpaka sasa katika koleji ya Sayansi Asilia na Hesabu kuna upungufu wa walimu 128 waliokuwa wanahitajika kufundisha program hiyo kwa ufanisi

“…kwa muhula uliopita ni walimu 72 tu ndiyo walio beba mzingo wa upungufu huo na kwa muhula huu hali ilikuwa inaelekea kuwa mbaya sana,” amesema.

Amesema kuwa, wingi wa wanafunzi na uhaba wa walimu ulisababisha upangaji wa ratiba ya kufundisha kuwa ngumu kutokana na kozi kugawanya katika mikondo mingi ambayo walimu walilazimika kuifundisha huku wakiwa na majukumu ya kufundisha kozi za shahada na majukumu mengine.

“Changamoto hizi za ufundishaji imekuwa ngumu kwa  menejimenti kuzifahamu kutokana na ukweli kwamba, wengi wao hawafundishi hivyo ni vigumu kupata maumivu yanayotokana na majukumu haya makubwa,” amesema.

Hata hivyo amesema kuwa, wanawakaribisha viongozi na wananchi mbalimbali kutembelea chuo chetu ili kujionea mazingira ya ufundishaji yalivyo na kuhakikisha wanayo yaeleza.

error: Content is protected !!