Tuesday , 16 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa La Prof. Kabudi, Zanzibar na mtego wa Komba
Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

La Prof. Kabudi, Zanzibar na mtego wa Komba

Spread the love

KOMBA amepewa sifa nyingi za ujanja. Kwa wanaomjua wanampa sifa nyengine, nayo ni ya ujasiri. Anaandika Othman Masoud Othman … (endelea).

Anapotafuta anachokitaka, hachelei kuingia katika nyumba ya mtu na hata chumbani.

Pamoja na udogo wake, lakini komba anapokabiliwa na tishio kutoka kwa binadamu, atachukua miguu yake ya mbele na kuiweka kichwani, kisha atatembea kwa miguu miwili ya nyuma akiwa wima; na hapo, kwa asiye mweledi wa kumjua komba anaweza kukimbia akidhani amekutana na jinni au kiumbe wa ajabu.

Naam, baba wa miraba minne anaweza kukimbizwa na komba huku akipiga kelele, pengine na suruali ikiwa ameshaiharibu.

Pamoja na ujanja, mbinu na ujasiri lakini kitu kimoja kimemsaliti. Uchu wake wa kupenda ndizi mbivu. Komba kwa ndizi mbivu ndio maafa na mauti yake.  Binadamu baada ya kujua udhaifu huu wa komba hawapati shida.

Ndizi mbivu huwekwa katika mtego wa komba na baadaye huachiwa yeye mwenyewe popote alipo aufuate na kujiangamiza mwenyewe. Mtego wa komba ni kipakacha chembamba sana kinachotengenezwa kwa kuti la mnazi.

Chembamba kiasi kwamba hata yeye komba huingia kwa shida. Ndizi mbivu huwekwa mwisho kabisa wa kipakacha.

Mlango wa kuingilia wa kipakacha huzungushwa kitanzi cha uzi madhubuti usiokatika na baadaye uzi huo hutumika kuifunga ndizi iliyoingizwa ndani ya mtego wa komba.

Nadhani kwa tabia yake, komba anapofika katika mtego, roho humtua akajua binadamu, kama kawaida yake mweledi wa kuficha, kaficha ndizi yake akijua komba haipati.

Basi hapo, komba huyu hupenyeza kichwa taratibu akivuta kidogo ndizi akaanza kula.

Kila ikipungua, anaivuta zaidi na zaidi na zaidi mpaka tumbo limejaa, mlo wa siku umetimia. Shida inaanza anapotaka kutoka katika kipakacha kile kwenda na safari zake. Anajikuta amekwama. Kuna kitu kimemnasa shingoni.

Mwanzo anadhani ni nyuzi tu za kipakacha, lakini baadaye anaanza kutanabahi kuwa ni kitu kibaya zaidi; ni kitanzi na kimeshakaa shingoni kinaanza kumbana.

Kinachomponza komba ni ukosefu wa nadhari. Badala ya kutulia angalau akabaki hai, anaanza kujinasua kwa pupa. Kila akijivuta, kila akitumia nguvu na kitanzi kinabana. Tahamaki roho imetoka.

Asubuhi, wale waliomtega wanapoenda kuangalia, hujisifu: “Aaah wa jana bwana…komba na ujanja wake, bwana ukimtaka, ndizi mbivu tu umemshika!”

Hawajali kama iliyotoka ni roho, tena wameitoa kwa sababu ya ndizi moja tu. Wanafurahi, wanasherehekea na wanajiandaa kutega komba mwengine.

Bila ya shaka, maafa ya Zanzibar hayafanani kwa asilimia mia moja na komba na mtego wa ndizi moja.

Lakini kwa fikra zangu, ipo elimu kubwa katika hili la mtego wa komba kwa Zanzibar, kwa Wazanzibari na hata kwa watawala wa Zanzibar wa sasa hivi, Tanganyika alias Tanzania.

Mjadala na Wasifu wa Profesa Kabudi

Nimefuatilia mjadala juu ya kauli ya Mwalimu wangu, Profesa Palamagamba Kabudi, aliyoitoa Bungeni akiwa Waziri wa Sheria wa Serikali ya Tanzania.

Miongoni mwa yanayolalamikiwa sana ni kauli yake juu ya hadhi ya Rais wa Zanzibar, hadhi ya Katiba ya Zanzibar na pia hadhi na mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Yamesemwa mengi, yamesemwa na wengi, si madhumuni yangu kuanza kuyarejea.

Wakati nasikiliza zile vidio za maelezo ya baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar pamoja na baadhi ya mawaziri walizozitoa katika Baraza la Wawakilishi kumjibu na hata kumlaani Profesa Kabudi, adhana ya laasir ikasomwa. Adhana ilinitanabahisha mambo mawili.

Kwanza, kwamba wakati wa sala umefika. Lakini la pili ni ile busara iliyomo ndani ya adhana.

Pamoja na kwamba sala ni amri ya Allah kwa waumini wa Kiislamu, lakini pia ni nguzo ya dini ya Kiislamu. Hata hivyo, waumini wanakumbushwa kila inapofika wakati wa sala. Falsafa ya kukumbusha ndiyo iliyonipelekea kuandika makala hii fupi.

Kwanza, napenda kutanabahisha wasifu wa Profesa Kabudi. Kwa kadri ninavyomuelewa ni mtu anayeufahamu vya kutosha mfumo wa sheria na katiba wa Zanzibar, historia yake na maendeleo yake. Anajua vionjo na viroja vya siasa za Zanzibar. Anajua hisia na mtazamo wa umma wa Zanzibar.

Lakini anajua pia udhaifu wa waliopo katika nyadhifa mbalimbali Zanzibar kama anavyoujua umakini na umahiri wa baadhi ya watu wa Zanzibar.

Ana faida ya kuijua Zanzibar tokea kwa babu zake. Hata jina lake la Palamagamba amelipata Pemba ambako babu yake aliwahi kufanya kazi ya fundi uashi.

Wengi wasiomjua Profesa Kabudi, wanadhani ni mwalimu tu wa Sheria wa Chuo Kikuu ambaye hatimaye ameteuliwa kuwa Waziri.

Wanaomjua wanakumbuka kwamba wakati wa vita vya Kagera alikuwa Mwandishi Msaidizi wa Mwalimu Julius Nyerere, kazi yake ikiwa ni kushughulikia utaalamu wa kuandika taarifa za vita.

Ni katika waliomshauri Mwalimu Nyerere kuwa taarifa zote za vita ziandikwe katika gazeti la Kiswahili la Serikali na waliobaki wanukuu kutoka katika gazeti hilo.

Weledi wa propaganda za vita na diplomasia wanajua kwamba hiyo sio mbinu ya kitoto bali ni ya weledi wa hali ya juu na inaonesha upeo wa waliotoa uamuzi huo.

Jengine ambalo binafsi nalifahamu kwa Profesa Kabudi ni kwamba msimamo wake binafsi ni kuwa Zanzibar inastahiki kukaliwa na Tanganyika [occupied] kwa maslahi mapana anayoyaita ya kimkakati.

Bila ya shaka hiyo ni kasumba ya wengi wasioungalia Muungano kiuchumi na mwenendo wa sasa wa kidunia. Huo ni mtazamo sio wake peke yake, bali wa makada wengi waliopita katika darsa ya MWALIMU yule aliyekuwa akitumia mtaala wa miaka ya 60.

Mbali ya sifa za kitaaluma na kiutumishi, lakini hata kwa upande wa dini amepata fursa ya kulitumikia Kanisa la Anglikana katika nafasi nyeti ya Katibu akiwa na jukumu moja muhimu nalo ni la kuchunga taratibu za kiutawala na uongozi.  Kwa ufupi amekuwa mchungaji wa Katiba, sheria na taratibu za Kanisa hilo.

Uzoefu katika nafasi zote hizo ukichanganya na sifa yake kubwa nyengine ya kuwa mtu mwenye kumbukumbu ya kusifika [photographic memory] haziendani na kile kinachodhaniwa kuwa amesahau alichokisema miaka mitatu tu iliyopita.

Kwa wenye tafakuri na wakawa wanamjua vyema Profesa Kabudi watatanabahi tu kwamba yupo katika mchezo wa kuaminisha lile liliomo katika ajenda ya Tanganyika ambayo baadhi ya viongozi walioiingiza Zanzibar katika mtego wa komba wanajifanya hawaijui.  Wanaotaka tuamini kwamba siasa za Muungano ni siasa za itikadi za vyama na sio siasa za kimkakati wa mtawala na mtawaliwa.

Ni rahisi kuchakata kauli za Profesa Kabudi kuonesha kwamba uwaziri umemfanya kuwa mnafiki na mwenye kigeugeu.  Nadhani ni busara kuangalia kwamba huyu ni mtu ambaye amekuwa katika “establishment” katika takriban uhai wake wote wa kikazi na kitaaluma.

Kubwa zaidi ni kuangalia hatima ya ugeugeu wake au “unafiki” wake. Yote mawili yana faida kubwa kwa mwajiri wake na yanakoleza ajenda tuliyotangulia kuieleza ya mtawala na mtawaliwa.

Katika falsafa ya vita hakuna kigeugeu bali kuna kujipanga upya. Kama kugeuka kauli au mbinu yako ni njia ya kushinda vita itakuwaje kigeugeu hicho kiwe na ila??? Binafsi yangu sioni kama katika aliyoyasema Profesa Kabudi lipo jambo jipya ambalo viongozi wetu hawalifahamu kwamba hiyo ndio dhana ya Muungano waliyonayo wengi wa viongozi wa umma wa Tanganyika.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Samia arejesha mikopo ya 10%, bilioni 227.96 zatengwa

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amerejesha utaratibu wa utoaji mikopo...

Habari za Siasa

Rais Samia amfariji mjane wa Musa Abdulrahman

Spread the loveRais Samia Suluhu Hassan leo Jumanne amempa pole Mwanakheri Mussa...

Habari za Siasa

Nape: Wanasiasa, wanahabari, wafanyabiashara mteteeni Samia

Spread the loveWaziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano,...

Habari za Siasa

CAG: TAWA imegawa vibali vya uwindaji bila idhini ya waziri

Spread the loveRIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali...

error: Content is protected !!