Monday , 27 May 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Kweli Mwl. Nyerere hafananishwi na yeyote
Makala & Uchambuzi

Kweli Mwl. Nyerere hafananishwi na yeyote

Spread the love

NI kweli kuwa, taifa si mtu mmoja kwa maana kwamba, akiondoka wengine watashika nafsi na siku zitasonga mbele. Anaandika Mchambuzi Wetu … (endelea).

Lakini hata hivyo, matukio na misimamo ya baadhi ya viongozi wetu yanakita fikra zetu na hata kuamini kwamba, mpaka sasa hakuna kama Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Mbali na Mwl. Nyerere kuwa mmoja wa wapigania uhuru wa nchi yetu ya Tanganyika,  na kisha kuwa rais wa kwanza wa nchi yetu, Tanganyika huru na baadaye rais wa kwanza wa Muungano wa Tanzania, yapo mambo mengi ya ziada tunayoyakumbuka na mengine kuyaona kwa macho yetu aliyowazidi warithi wake waliomfuatia.

Mambo hayo hayana kingine cha kumuongezea Nyerere zaidi ya kumfanya aonekane ni Baba wa Taifa kwa maana halisi.

Hebu nikumbushe kidogo, muda mfupi baada ya Tanganyika kuwa huru, mwaka 1963, aliyekuwa rais wa Marekani wakati huo, Jonh Fitzgerald Kennedy maarufu kama JFK alimwalika Mwalimu Marekani na kumpa mapokezi makubwa ya kitaifa.

Hata Rais Barack Obama, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 2 ya kuzaliwa, aliiongelea ziara hiyo ya Mwl. Nyerere alipoitembelea Tanzania.

Siyo kwamba hakuna marais wengine wa Tanzania waliokwenda Marekani, wapo na wengine wameitembelea mara nyingi kuliko Mwl. Nyerere ila kauli ya Obama kuhusu ziara hiyo, ilionesha kwamba Mwl. Nyerere ndiyo pekee imewekwa kwenye kumbukumbu ya taifa hilo.

Katika picha za video za ziara hiyo ya Mwl. Nyerere ya mwaka 1963, Nyerere anaonekana akitoa hotuba katika viwanja vya White House, Ikulu ya Marekani.

Ni  baada ya kukagua gwaride la heshima pamoja na kupigiwa mizinga. Hiyo ni heshima ambayo Wamarekani hawaitoi kwa kila mgeni wao.

Katika hotuba hiyo Mwl. Nyerere alisema kwamba, Tanganyika ni nchi inayoundwa na jamii ya watu wa aina mbili, wenyeji na wahamiaji, akasisitiza kwamba watu hao wote wana haki sawa.

Hiyo maana yake ni kwamba, Mwl. Nyerere hakuwahi kuwa na fikra za kuwatimua watu nchini kisa eti wanatoka nchi nyingine.

Sababu zake za kufanya hivyo zilikuwa wazi, ni kwamba yeye alikuwa msitari wa mbele katika kupinga vitendo vyote vya kibaguzi vilivyokuwa vikifanyika kuanzia Marekani mpaka Afrika Kusini vikiwa vimejikita kwenye tofauti za rangi na asili ya mtu.

Mpaka Mwl. Nyerere anaaga dunia, msimamo wake ulikuwa kwamba, watu wanaojiita wazawa wa nchi hii wakiwabagua wengine kuwa ni wahamiaji ni makaburu tu. Akawa anasisitiza kwamba ukaburu sio rangi bali ni tabia ya mtu.

Jambo la kujivunia zaidi kwa Mwl. Nyerere mbali na hilo la kutuondolea kubaguana kwa rangi na asili, alitupatia heshima kubwa katika jumuiya ya kimataifa.

Inakumbukwa kwamba, baada ya ziara yake ya Marekani mwaka 1963, miaka 14 baadaye, mwaka 1977, alifanya ziara nyingine nchini humo akiwa amealikwa na Rais wa Marekani wa wakati huo, Jimmy Carter.

Hata ziara hiyo ya pili rasmi ya Mwl. Nyerere nchini Marekani ililifanya taifa hilo kubwa kuzizima likionesha kwamba kuna mtu mzito kalitembelea.

Hiyo ilikuwa ni sifa na heshima ya pekee kwa nchi yetu. Tusimuenzi Mwl. Nyerere kwa hilo, tufanye kitu gani kingine?

Katika hotuba ya kumkaribisha Mwl. Nyerere, Agosti 4, 1977, Rais Carter alisema maneno yafuatayo, “Miaka 14 iliyopita kiongozi kijana wa taifa letu, John Kennedy alimkaribisha kiongozi kijana wa taifa jipya, Julius Nyerere, kwenye nchi yetu.

“Ilikuwa ni heshima kwa nchi yetu kutembelewa na kiongozi huyo mpya wakati nchi yake ina umri wa miaka miwili tu.”

Kwahiyo tunaweza kuona ni uzito kiasi gani aliokuwa akitupatia Mwl. Nyerere na tukitaka tunaweza kuulinganisha na uzito waliotupatia wengine ili kuona kama tunachokifanya kwa sasa, kumuenzi Mwl. Nyerere, kinasababishwa na msukumo wa hisia tu au ukweli usio na ubishi wowote.

Kitu kingine ni kwamba, Mwl. Nyerere alikuwa ndugu kwa wananchi wote. Kila Mtanzania alikuwa ndugu yake wa kweli. Hakuwahi kuonesha tofauti yoyote kati ya ndugu wa tumbo moja na ndugu wengine wa kitaifa.

Kama ni shule watoto wake walisoma shule za kawaida sawa na walizosoma watoto wa wananchi wa kawaida, vivyo hivyo kwa vyuo.

Mwaka 1985, wakati Mwl. Nyerere anakaribia kustaafu, mmoja wa watoto wake alifanya vurugu katika sehemu moja ya starehe na kufikishwa katika kituo kimoja cha polisi.

Askari kuona hivyo walichokifanya ni kupiga simu nyumbani kwa Mwl. Nyerere Msasani, bahati mbaya simu hiyo akaipokea mwenyewe.

Mwl. Nyerere aliwauliza askari hao kwamba, ina maana kila mtu anayefanya vurugu na kufikishwa kituoni hapo askari hao wanampigia simu baba yake?

Hiyo ni heshima nyingine ambayo Mwl. Nyerere ameijengea hata familia yake mbali na aliyolipatia taifa.

Inaonekana kwamba katika Afrika, watoto wengi wa marais wastaafu wanaishi maisha ya tabu, wengi wanaonekana wananyanyaswa achilia wale wanaotumikia vifungo vya muda mrefu na wengine kuuawa.

Hiyo ni kutokana na watoto hao kuutumia vibaya muda ambao wazazi wao walikuwa vinara wa nchi zao.

Watoto wengi wa marais wa Kiafrika waliotumia vibaya muda wa wazazi wao kuwa Ikulu, kwa kufanya mambo yasiyokubalika kijamii, wamejikuta katika matatizo makubwa baada ya wazazi wao kuondoka Ikulu.

 Ipo mifano ya Marehemu Wezi Kaunda  mtoto wa Mzee Keneth Kaunda wa Zambia, Atupele Muluzi mtoto Bakili Muluzi  wa Malawi ambaye yuko kifungoni, mtoto wa Abdoulaye Wade, rais mstaafu wa Senegal, Karim Wade  ambaye naye yuko kifungoni.

Lakini mpaka sasa watoto wa Mwl. Nyerere bado wanaishi kwa raha mustarehe kutokana na baba yao kutowaachia nafasi ya kufanya mambo yasiyokubalika kijamii. Kwa hakika Mwl. Nyerere hafananishwi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Rais Samia muonee huruma Dk. Phissoo

Spread the loveRAIS wangu mama Samia, wiki iliyopita baada ya kuwa nimekuandikia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

GGML inavyookoa walemavu dhidi ya dhana potofu

Spread the loveMKOA wa Geita ni mmoja wa mikoa ya Kanda ya...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Miaka 63 ya Uhuru bila katiba ya wananchi

Spread the loveWAFUASI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wanaharakati...

AfyaMakala & Uchambuzi

Uongo, uzushi, tiba ya matende, ngiri maji

Spread the loveKUNA uongo na uzushi katika jamii kuhusu wanaume, wanawake na...

error: Content is protected !!