KWAYA ya Mtakatifu Kizito, Parokia ya Mwenyeheri Anuarite Makuburi, Jimbo kuu Katoliki la Dar es Salaam, inatarajia kufanya ziara ya kitume nchini Kenya kuanzia tarehe 31 Mei hadi 6 June mwaka huu. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Katika ziara hiyo pamoja na mambo mengine, kwaya itashiriki kwenye misa maalum iliyoandaliwa na Jimbo Kuu la Nairobi, kuomba amani wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo, utakaofanyika mwezi wa 8 mwaka huu.
Mbali na misa hiyo itakayoadhimishwa tarehe 4 June, Kwaya ya Mt Kizito itakuwa na tamasha kubwa siku inayofuata ya tarehe 5 June, tamasha litakalofanyika katika parokia ya Queen of Apostles Ruaraka, linalojulikana kama Kmk Gala.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kwaya ya Mt Kizito. Nicetas Lyamuya kwaya hiyo inakwenda kuhubiri amani.
“Tunakwenda kuhubiri amani, amani ya Wakenya ni amani ya Watanzania, na mbali ya kusali nao, Wakenya wawe tayari kupata burudani safi toka kwetu” alisema.
Akizungumzia ziara hiyo, Mkurugenzi wa Liturjia wa Jimbo Kuu la Nairobi, Padre Bernard Kabiu alisema “Tunawaomba wanakwaya, mapadre, walei na wote wenye mapenzi mema wafike katika matukio yote watakayofanya wanakwaya hawa ili wajifunze mambo mengi mazuri toka kwaya hii maarufu na bora kabisa katika ukanda huu wa AMECEA na kwingineko”.
Misa ya kuomba amani itakayoanza saa tatu asubuhi, itaadhimishwa katika Kanisa la St Mathias Mulumba, na inatarajiwa kuongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Nairobi, Mhashamu Phillip Anyolo.
Pamoja na kushiriki matukio hayo makubwa mawili, pia kwaya ya Mtakatifu Kizito itafanya ziara katika parokia mbalimbali za Jimbo la Nairobi, Ngong na Machakos.
Kwaya ya Mtakatifu Kizito Makuburi, iliyoanza utume wake mwaka 1988, inaundwa na wanakwaya 120. Inatarajia kurudi nchini June 6 mwaka huu.
Leave a comment