July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kwa sababu hizi, CCM wamekosa kura yangu

Wanachama wa CCM wakiwa katika mkutano wa hadhara

Spread the love

ZAIDI ya miaka 50 sasa, Tanzania imekua chini ya utawala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Tumekuwa katika mfumo wa chama kimoja hadi mwaka 1992, Watanzania waliporidhia demokrasia ya vyama vingi.

Tangu uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, nguvu ya CCM imekuwa ikipunguzwa taratibu kutokana na vyama vya upinzani kuimarika mijini na vijijini.

Kuna mambo mengi yaliyosababisha chama hiki kupoteza umaarufu na kura nyingi kwa kipindi kifupi mno; kubwa kati ya yote ni ufisadi mkubwa uliokithiri katika serikali.

Sasa imebakia miezi michache tu kabla ya Rais Jakaya Kikwete kuachia ngazi kutokana na muda wake wa kuongoza kuwa umefika ukingoni.

Mimi na Watanzania wengi wapenda maendeleo tuliochoka kunyanyaswa, tunaomba kwa nguvu zote siku ziende ili huyu jamaa (CCM) akapumzike na serikali yake iliyoshindwa.

Ninasema wakapumzike Oktoba kwa sababu wamechoka sana na ndio maana nchi wanaipeleka siko kabisa yaani ni kama mtumbwi katikati ya bahari uliokosa kasia.

Hivyo basi kwa yeyote atakayesimama kwa tiketi ya chama hiki kugombea nafasi yoyote, kura yangu ataikosa tu. Haijalishi ni diwani, mbunge au rais kwangu akitokea tu kwenye huu ukoo usio na huruma na moyo wa uzalendo basi ni “hapana” na ninazo sababu.

Utekelezaji mbovu wa ilani ya uchaguzi ya chama chao. Wakati wa kampeni mwaka 2010, wagombea wa CCM walizunguka nchi nzima kunadi ilani yao iliyosheheni ahadi lukuki ambazo hadi leo nyingi zimebaki bila utekelezaji.

Sera nzuri walizopewa wakulima, wafanyakazi, vijana, walimu, wazee, wanawake na makundi mengine, zimeshindwa kutekelezeka chini ya utawala wa CCM.

Sababu nyingine ni sera mbovu za serikali kuhusu maendeleo ya nchi yetu. Nchi yetu imekua na utajiri wa watunga sera ambao kila wakati huja na mipango mingi ambayo utekelezaji wake huwa ni sifuri.

Kila siku wanabadilisha sera zao kwa kuzipa majina mazuri na yenye mvuto kwa kuyasikiliza lakini hakuna mafanikio. Tumeanzisha sera ya kilimo kwanza kwa nguvu, lakini leo tunapojipapatua na matokeo makubwa sasa, wakulima wako hoi.

Watanzania wa sasa sio wale wa enzi zile; ukiziangalia sera hizi na malengo yake yana utofauti gani na sera kama kilimo cha kufa na kupona na kilimo ni siasa za hayati Mwalimu Nyerere?

Zote zililenga uzalishaji wenye tija katika kilimo na kwa kiasi fulani zilifanikiwa. Je, kuna haja gani kwa nchi kubadilisha sera za maendeleo kila siku bila hata kukaa chini na kuangalia sera zilizopita zimefanikiwa au kushindwaje.

 Viongozi wa CCM hawana muda wa kuyawaza haya na kila mtu akiamka anawaza lake na jinsi gani atainyonya Tanzania yetu. Je, CCM watapata vipi kura yangu?

Sababu nyingine ni matumizi  mabaya ya rasilimali za taifa na uchukuliwaji mbovu hatua kwa wahusika. Tanzania ni nchi pekee duniani inayosamehe wezi wa mabilioni ya fedha.

Yaani kiongozi mkuu anasimama na kuwaambia wezi warudishe fedha halafu wanasamehewa. Hivi kweli tuko makini na maendeleo ya taifa hili au watu wanataka kuwa viongozi ili wajinufaishe wao na jamaa zao.

Hillary Clinton aliyewahi kuwa waziri wa masuala ya nje wa Marekani alifikishwa mahakamani kwa kosa la kutumia mawasiliano binafsi ya mtandao (e-mail) kwa shughuli za kiofisi. Ingekuwa Tanzania ingekuwa jambo la kawaida.

Ukifuatilia Bunge letu kila siku ni fulani kala kiasi hiki, yule kafisadi kiasi hiki lakini cha ajabu hakuna hatua zinazochukuliwa.Watu wamechota mabilioni kwenye akaunti ya Tegeta Escrow lakini wakihojiwa wanatoa majibu mepesi -mepesi yanayoamsha hisia za walalahoi.

Sasa napata majibu kwanini CCM walitoa vipengele vya uadilifu, uzalendo na uwajibikaji katika katiba pendekezwa; wakachakachua rasimu ya Jaji Joseph Warioba.

Tembo wanauawa hakuna majibu ya kuridhisha zaidi ya kusikia watu wakisema bungeni kuwa wana majina ya wahusika lakini kwa kuwa wahusika ni wao wenyewe.

Sababu nyingine ni hali mbaya ya usalama wa nchi yetu, hivi karibuni kumekuwa na hali ya sintofahamu kwa wananchi wa maeneo mengi kutokana na kushamiri kwa vitendo vya kihalifu ndani ya nchi yetu.

Raia na askari wasio na hatia wamejeruhiwa na kupoteza maisha katika matukio hayo tofauti ya kihalifu, silaha zimeporwa ingawa polisi wanadai nyingi zimekamatwa na wahusika kutiwa hatiani. Hapa CCM wanapataje kura yangu.

Sababu nyingine ni kuongezeka kwa ugumu wa maisha kwa watanzania wengi hasa wa kipato cha kati kama wafanyakazi, wakulima na wafanyabiashara, ugumu huu unatokana na kushindwa kwa serikali yetu kuwawezesha au kuyajengea makundi haya mazingira mazuri ya kuendesha shughuli zao.

Katika sababu chache hizi hakika naisubiri CCM kwa hamu kubwa ifikapo Oktoba mwaka huu, niwapigie kura yao ya “hapana”.

Mwandhishi wa makala hii ni Charles Mlelwa ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mkwawa Iringa. Anapatikana kwa 0754 820453/ Charles.mlelwa@yahoo.com

error: Content is protected !!