June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kwa Nyalandu, tembo watatoroka nchi

Tembo wakiwa katika Hifadhi

Spread the love

LAZARO Nyalandu, Waziri wa Maliasili na Utalii, anakwepa kupambana na majangili mwituni. Badala yake, kutwa kucha kiguu na njia kwenye vyombo vya habari kupiga porojo na ‘kuuza sura’. Anaandika Yusuph Katimba … (endelea).

Huko anajigamba ‘Tutawasaka, tutawakamata popote walipo.’ Mwisho wa siku anarejea mikono mitupu. Tembo wanazidi kuteketezwa huku akitumia rasilimali za nchi kuzurura. 

Wiki tatu zilizopita, ameandamana na viongozi wa dini na wasanii kuzindua jijini Dar es Salaam, kilichoitwa “kampeni ya kupambana na ujangili.”

Hivi karibuni Nyalandu katika safari yake isiyo na matumaini kawaingiza Asasi ya Kimataifa ya WildAid na African Wildlife Foundation kwa nia ya kuelimisha jamii kuhusu ujangili.

Nyalandu anazindua kampeni hii wakati akiwa na majina ya majangili mkononi, ambayo aliahidi kuyaweka hadharani. Zaidi ya mwaka sasa, kimya.

Kimya chake hicho yawezekana kimemvurua Rais Jakaya Kikwete, ambaye mara kadhaa hubanwa na asasi na mataifa aeleze jitihada za serikali yake kulinda tembo. Ilitokea alipoalikwa na familia ya kifalme ya Uingereza 2014.

Hivi ni kweli waziri huyu hajui sababu ya kushamiri kwa ujangili nchini? Kama kweli hajui, anatambaje nchini na akizunguka dunia kuwa Tanzania iko makini katika kudhibiti ujangili?

Kwa uzito wa tatizo, akachukua viongozi wa dini na wasanii akiwatumia kushawishi washiriki wa ujangili waache ukatili wao kwa wanyamapori hazina ya nchi? Anasema, wasanii na viongozi wa dini waelimishe jamii madhara ya ujangili, ni kweli kazi hiyo inawafaa? Amewapa nyenzo?

Harakati za kusaidia Wizara ya Maliasili na Utalii zimesaidiwa na wadau wengi ndani na nje ya nchi. Juhudi zote hizo matokeo yake yamekuwa sifuri.

Mifano ni Mei 2014, Nyalandu alipokea magari matatu aina ya Land Cruiser yenye thamani ya Sh. 350 milioni kutoka Mwenyekiti wa Taasisi ya Uhifadhi Wanyamapori Tanzania, Eric Pasanis kwenye Hoteli ya Hyatt Kilimanjaro, jijini Dar es Salaam.

Machi mwaka huu, alikabidhiwa ndege aina ya Micro Light Nyinja 5h-hel iliyonunuliwa na kampuni ya Tanganyika Wildlife Safari.

Mwaka jana, Wizara ilipokea Dola 15 milioni za Marekani (sawa na Sh. 300 bilioni) kutoka Uingereza baada ya kusaini makubaliano ya kusaidia kukomesha ujangili. Fedha alikabidhi Balozi wa Uingereza nchini, Diana Melrose.

Mkurugenzi wa Frankfurt Zoological Society (FZS) Kanda ya Afrika, Robert Muir ameikabidhi Wizara magari 11 ya kusaidia kampeni hiyo ya kukomesha ujangili. Msaada ulipokewa na Rais Jakaya Kikwete.

Utafiti uliofanywa wiki mbili zilizopita na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) umebaini kuwa Tanzania inaongoza kwa tatizo la ujangili kwa wanyamapori wake. 

Wakati wataalamu wa wanyamapori wakishauri, askari wa kikosi cha kudhibiti ujangili (KDU) wakipaza sauti zao kutokana na mazingira mabaya ya utendaji wa kazi – mishahara isiyotosha, upungufu wa sare – waziri Nyalandu anayepaswa kuongoza vita, anarandaranda hata kutajwa na Katibu Mkuu wa CCM, Kanali Abdulrahman Kinana kuwa mzururaji hadi nje ya nchi.

Kwa bahati mbaya, mirando na uzururaji wake unatiliwa nguvu na vyombo vya habari vinavyomripoti hata akikohoa tu. Kuwalinda tembo, simba na chui si kazi ya lelemama huku wapambanaji wakijipaka uturi. 

Hivi Nyalandu ni nani? Jeuri, ujasiri na roho ngumu aliyonayo vinatoka wapi? Kama ni Mungu wake, basi kapendelewa. Kama ni kamzizi basi namvulia kofia mganga wake!

Wakati waziri huyu anauza sura kwenye vyombo vya habari, huko mwituni, wanyama wanaendelea kupaza sauti zao zilizokosa msaada kutokana na kushambuliwa na kuuawa siku hadi siku.

Kama binadamu angekuwa anazawadiwa udaktari wa heshima (PhD) kwa kuwa na roho ngumu, basi Nyalandu angestahili kwa kuwa, wanyama wanateketea msituni, yeye anadunda mtaani.

Mbaya zaidi, mpiganaji wa vita vya ujangili naye anatuhumiwa ujangili. Iliandikwa hii kwamba unampa mbwa mwitu kundi la mbuzi awalinde. Ripoti za tuhuma hizi zimo mikononi mwa serikali maana zimeandaliwa na makachero. 

Katika mapambano ya ujangili, anavyo vipaumbele vya ajabu. Wakati watendaji wa wizara na mashirika yake, tena wenye taaluma zao, wanashindwa kutekeleza majukumu yao kutokana na bajeti duni, yeye anatumia kwa mamilioni kusafiri. 

Badala ya kushiriki vizuri na askari wake porini walau kupunguza kama si kumaliza tatizo la ujangili, yeye anakwepa na mwaka jana akathubutu kufukuza maprofesa Alexander Songorwa na Japhari Kideghesho waliokuwa wanashinda hifadhini kushiriki kampeni pamoja na askari.

Katika safari zake za kustarehe badala ya kuwa makini katika kudhibiti ujangili, waziri Nyalandu aliagiza wizara imgharamie Aunt Ezekiel nchini Marekani alikotetea ilikuwa safari ya kupambana na majangili wanaoua wanyama nchini Tanzania. 

Ninashikwa na kwikwi ninapokumbuka kashfa za wizara hii, ile ya waziri Nyalandu kushinikiza Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) ilipie Sh. 560 milioni kugharamia mashindano ya mrembo wa Afrika Mashariki (Miss East Africa).

Hivi karibuni alikutana na kigingi alipobanwa buingeni kueleza kwanini ameshindwa kuanzisha rasmi kiwango cha tozo kwa mahoteli yanayopokea watalii hivyo kuipotezea serikali zaidi ya Sh. 70 bilioni kwa mwaka. 

Oktoba 2 mwaka jana, Rais Kikwete alifungua Maonesho ya Kimataifa ya Utalii (Swahili International Tourism Expo -SITE), Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam. Maonesho haya ya aina yake yalishirikisha watu wa mataifa barani Afrika na kwingineko. Waziri Nyalandu hakuwepo ukumbini. 

Kutokuwepo kwake kulisababisha usumbufu kwa wadau mbalimbali waliohudhuria; walitaka kufanya majadiliano na waziri mhusika kuhusu wanavyoweza kutoa msaada katika matatizo yanayokabili sekta ya utalii. Walijibiwa “Waziri hayupo.”

Yeye ndiye aliyetakiwa kuwa mwenyeji wa mkutano na Rais aoneshe bashasha kuwa anae waziri makini. Masikini wee, Rais Kikwete alitelekezwa na waziri wake. 

Pamoja na kutumia muda mwingi nchini Marekani ambako aliwahi kuishi kwa hadhi ya “mhamiaji mahsusi”, wakati tukio hili likifanyika waziri alikuwepo ndani ya nchi. Je, kwenye mazingira haya kweli anaweza kuwa askari makini wa kuwashughulikia majangili? 

Kioja ni pale unapokuta waziri aliyejijengea umaarufu kwa kufunga safari za ughaibuni wakati akihitajika kuongoza kampeni ya kulinda tembo na wanyamapori wengine wanaoitilia nchi mabilioni ya shilingi kila mwaka kwa kuvutia watalii, ameingia katika orodha ya wasaka urais kupitia chama chao – CCM. 

Duu, itakuaje akipitishwa? Naona hata kabla ya kuingia Oktoba 25, tembo wakishapata taarifa, watatoroka wakahamie Kenya.

Mawasiliano: yusqup@yahoo.com, 0713 517011 / 0767 517012

error: Content is protected !!