January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kuziona Twiga, She-Polopolo Tsh 2,000

Wachezaji wa Twiga Stars wakishangilia

Spread the love

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu nchini TFF limetangaza viingilio vya mchezo kati ya timu ya Taifa ya Tanzania ya Wanawake (Twiga Stars) dhidi ya timu ya Taifa ya Zambia (She-Polopolo) kiingilio cha juu sh.5,000 kwa VIP na sh. 2,000 kwa majukwaa yaliobakia, mechi hiyo itachezwa ijumaa jioni saa 10 kwenye dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Twiga Stars chini ya kocha mkuu Rogasian Kaijage imeendelea kujifua katika hosteli za TFF zilizopo Karume, kuhakikisha inaibuka na ushindi katika mchezo huo wa kuwnaia kufuzu kwa Michezo ya Afrika nchini Congo- Brazzavile mwezi Septemba mwaka huu.

Katika mchezo wa awali uliofanyika wiki tatu zilizopita jijini Lusaka nchini Zambia, Twiga Stars iliibuka na ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya wenyeji Zambia, hivyo katika mchezo wa ijumaa kuhitaji ushindi wa aina yoyote tu ili kuweza kufuzu kwa fainali hizo.

TFF inawaomba wapenzi, wadau na washabiki wa mpira wa miguu nchini, kujitokeza kwa wingi siku ya ijumaa jioni uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kuja kuwapa sapoti Twiga Stars watakapokuwa wanapeperusha bendera ya Taifa.

Wakati huo huo, timu ya Taifa ya Wanawake ya Zambia (She-Polopolo) inatarajiwa kuwasili usiku wa saa 7.25 kuamkia alhmisi kwa shirika la Ndege la Ethiopia wakiwa na msafara wa wachezaji 18 na viongozi saba na watafikia katika hoteli ya Tansoma iliyopo eneo la Gerezani Kariakoo.

Msafara wa Zambia (She-Polopolo) unaongozwa na mkuu wa msafara Lenny Khuwa, kocha mkuu Albert Kachinga, kocha msaidizi Kape Saili, kocha wa magolikipa Yona Phiri, daktari wa timu James Nyimbili, mchua misuli Conerlia Chazura, na meneja wa timu ni Besa Chibwe.

Wachezaji wanaotarajiwa kuwasili ni Rachel Nachula, Annie Kibanji, Chiko Nkhoma, Osala Kaleo, Joana Benai, Meya Banda (Nahodha), Misozi CR Chisamu, Jane Nshika Chalwe, Milika Limwanya, Mary Wilombe, Grace Chanda, Barbra Banda, Memory Mwaseba, Hazel Natasha Nali, Martha Tembo, Mary Mwakapila na Ireen Lungu.

Kesho jioni She-Polopolo wanatarajiwa kufanya mazoezi katika uwanja wa Taifa, uwanja ambao ndio utakaotumika kw amchezo huo.

Waamuzi wa mchezo huo kutoka nchini Uganda wanatarajiwa kuwasili leo mchana ambao ni  Ms Anna Akoyi , Ms Nakkito Nkumbi , Ms Jane  Mutonyi, na Ms Nabikko Ssemambo, Kamishina wa mchezo  Ms Nomsa Jacobeth Mhalangu kutoka nchini Afrika Kusini anatarajiwa kuwasili leo jioni.

Wakati huo huo, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF Jamal Malinzi, amempongeza Bw Leodgar Tenga kwa kuchaguliwa kuendelea kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF).

Aidha Rais Malinzi ametuma salamu za pongezi kwa wajumbe  waliochaguliwa kuwa wajumbe wapya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu baranai Afrika (CAF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani FIFA.

Katika salamu hizo na nakala zake kutumwa kwa Rais wa CAF Bw. Issa Haytou na Rais wa FIFA Bw. Blatter, Malinzi amewatakia kila la kheri katika majukumu hayo mapya,na  kwa ajili ya maendeleo ya mpira wa miguu duniani.

Tenga amechaguliwa nafasi hiyo baada ya kuwa mgombea pekee kutoka kanda ya Afrika Mashariki aliyejitokeza kuwania nafasi hiyo na kuungwa mkono na nchi zote wanachama wa CECAFA.

error: Content is protected !!