JOTO la miamba ya soka nchini Tanzania maarufu Kariakoo Derby limeanza kushika kasi kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutangaza viingilio ambavyo kiwango cha chini kitakuwa Sh.10,000. Anaripoti Damas Ndelema na Wiston Josia, TUDARCo … (endelea).
Mtanange huo wa Simba na Yanga wa Ngao ya Jamii, utapigwa kuanzia saa 11:00 jioni ya Jumamosi hii, tarehe 25 Septemba 2021, katika dimba la Benjamin Mkapa, mkoani Dar es Salaam.
Ni mchezo unaoashiria ufunguzi wa msimu wa mashindano wa mwaka 2021/22.
Leo Jumanne, tarehe 21 Septemba 2021, TFF imefanya mkutano na waandishi wa habari ukiwahusisha timu husika Simba na Yanga makao makuu ya shirikisho hilo, Karime jijini Dar es Salaam.
Cliford Mario Ndimbo,Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF amesema, maandalizi ya mchezo huo yanakwenda vizuri ikiwemo viwango vitakavyotumika siku hiyo.
Ndimbo amesema, viingilio “havitahusisha VIP A ambayo haitakuwa na tiketi ni kwa mwaliko maalum. Kama kuna watu wanadhani wanaweza kualikwa wawasiliane na TFF.”

Amesema, VIP B itakuwa Sh. 30,000, VIP C na viti vya rangi ya machungwa Sh.20,000 na viti vya rangi ya blue na kijani Sh.10,000.
Timu hizo zinakwenda kukutana kila mmoja akiwa ametoka kufungwa michezo yao waliyocheza juzi Jumapili, tarehe 19 Septemba 2021.
Mabingwa watetezi wa ligi kuu 2020/21, Simba ilifungwa 1-0 na TP Mazembe, kwenye kilele cha tamasha la Simba Day, Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Ezekiel Kamwaga, Kaimu Ofisa Habari wa Simba amesema, baada ya tamasha hilo, wachezaji walipewa mapumziko ya siku mbili na leo Jumanne, wameingia kambini.
“Simba iko tayari. Mara baada ya tamasha la Jumapili, tulipumzika siku mbili na leo timu imeingia kambini na iko salama. Haina majeruhi yoyote. Tumepata mechi za vipimo vya kutosha na hatuna presha kwenye hiyo mechi,” amesema Kamwaga
Watani zao Yanga walikubali kipigo cha 1-0 kutoka kwa Rivers United nchini Nigeria, kwenye mchezo wa marudiano wa Klabu Bingwa Afrika. Kilikuwa kipicho cha pili kutoka kwa timu hiyo, kikitanguliwa na cha 1-0, Uwanja wa Mkapa na kuwatoa kwenye michuano hiyo.
Hassan Bumbuli, Ofisa Habari wa Yanga amesema, tayari kikosi cha timu hiyo kimerejea salama na kinaendelea na maandalizi “kwani ratiba ya huu mchezo tulikuwa tunaijua na wala hatuna presha.”
“Tunaingia katika mchezo huu dhidi ya Simba tukiwa na kikosi imara, kinaendelea kuimarika siku hadi siku na wale ambao mlikuwa mnawasikia sikia, nao watakuwepo. Sisi tupo imara sana,” amesema Bumbuli.
Bumbuli na Kamwaga wamewaomba mashabiki zao kujitokeza kwa wingi siku hiyo kushuhudia kandanda safi huku kila mmoja akijinasibu kuibuka mshindi katika mchezo huo.
Leave a comment