SIMULIZI za Merry Mgowe, mkazi wa Kisiwa cha Ukara zinaumiza ngoma za masikio hasa baada ya kubaini kuwa, sasa yeye ndiyo mlezi kamili wa wajukuu zake watatu mmoja kati yao akiwa ananyonya. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Akiwa ufukweni mwa Ziwa Victoria katika Kisiwa cha Ukara huku akitazama maji ya ziwa hilo, anayo matumaini ya kumpata mtoto wake akiwa hai ama amekufa.
“Nimeacha wajukuu zangu watatu nyumbani, mama yao alikuwa kwenye meli hiyo na sijamwona mpaka sasa. Nipo hapa tangu juzi, kila anayetolewa kwenye maji nakwenda kumwangalia walau naweza kubahatika kumwona mwanangu lakini bado sijaona sura yake mpaka sasa,” anasema Bi. Merry.
Anasema kuwa, ni siku ya tatu sasa yupo ufukweni akitazama huku na kule kama anaweza kumwona mwanaye lakini mpaka sasa hajapata taarifa yoyote kuhusu mtoto wake.
Akibubujikwa machozi Bi. Merry anasema, alirejea mara moja nyumbani kwake kuwaangalia wajukuu zake na kurudi ufukweni hapo akimsubiri mwanaye.
Sura ya Bi. Merry inaonekana kukata tamaa, muda mwingi anapozungumza anabubujikwa machoji “naendelea kuwepo hapa mpaka nione mwisho wake.”
Caloline Nyamwanga ambaye pia ni mkazi wa Kisiwa cha Ukara anasema, hajaona ndugu zake wanane tangu kupatikana kwa taarifa ya kuzama kwa Meli ya MV. Nyerere juzi tarehe 20 Septemba 2018 ikielekea kutia nanga kwenye kisiwa hicho.
“Nasubiri ndugu zangu wanane hapa, walikuwa kwenye meli ile (anainyooshea kidole). Sijatoka kwa siku tatu sasa nawasuburi, sijaona hata maiti zao isipokuwa moja tu, siondoki mpaka mwisho,” ameeleza Nyamwanga.
Mwanamama huyo amewataja baadhi ya ndugu zake anaowasubiri mpaka sasa kwamba ni Aninta Nyangoro, Muinga Magai, Lucy ambaye ni mjukuu wake, mkwewe Anita, mtoto wa kaka yake anayeitwa Sosi Bangili.
Leave a comment